HEADER AD

HEADER AD

WAZEE KENYA WATOFAUTIANA KUHUSU UMRI WA TOHARA KWA WAVULANA


WAZEE wa jamii ya Agikuyu wametofautiana kuhusu umri bora wa tohara kwa wavulana ambapo baadhi wanataka umri wa miaka 12 unastahili wengine wakitaka uwe umri wa miaka 14, huku wengine wakitaka uwe wa miaka 16.

Suala la tohara unaenziwa zaidi katika jamii hii na nyingine za eneo la Mlima Kenya, kwani huwawezesha wavulana kuruhusiwa kuoa na hatimaye kuingia kundi la wazee.

Tangu ujio wa elimu ya kisasa, wavulana waliokamilisha masomo ya shule ya msingi ndio walikuwa wakichukuliwa kama waliohitimu umri wa kufanyiwa tohara.

Shughuli hiyo hufanywa kwa njia ya kitamaduni, wavulana hukabiliana na kisu cha ngariba alfajiri wakiwa kando ya mito.

Inaelezwa kuwa kwa sasa wavulana hupelekwa hospitalini kutahiriwa, wakipewa dawa za kupunguza uchungu, baadhi yao wakiwa wameandamana na akina mama na dada zao.

Katika jamii ya Agikuyu na nyingine za Mlima Kenya, wavulana hutahiriwa mwezi wa Desemba.

Pia wanaweza kutahiriwa katika miezi ya Aprili au Agosti, shule zikifungwa mwishoni mwa muhula.

Kulingana na mtaala wa sasa na Utendaji (CBC), wavulana hujiunga na shule za sekondari msingi (gredi ya saba) wakiwa na umri wa angalau miaka 12.

Wanatakiwa kuendelea hadi gredi ya tisa ambapo umri wao utakuwa angalau miaka 16.

Hata hivyo, Chama cha Walimu wakuu wa shule za upili (KESSHA) kinataka wanafunzi wa gredi ya nane na tisa wahamishwe hadi shule za upili zinazotambulika, hali ambayo inaelekea kusukuma umri wa upashaji tohara kuwa miaka 14.

Hii imesababisha mgawanyiko katika Baraza la Wazee wa Jamii ya Agikuyu (Kiama Kia Ma), huku mwenyekiti wake Thiong’o wa Gitau akisisitiza kuwa umri wa wavulana kutahiriwa uwe miaka 16.

Lakini mdhamini wa kitaifa wa baraza hilo, Kung’u Muigai, amejitokeza na kupinga msimamo wa Bw Gitau, akishikilia kuwa umri wa miaka 14 ndio unapaswa kuzingatiwa.

Kwa hivyo, Bw Gitau ametangaza kuwa hakutakuwa na shughuli ya kuwapasha tohara wavulana katika eneo la Mlima Kenya ilhali Bw Kung’u anashikilia kuwa itaendelea ilivyoratibiwa.

Upashaji tohara wavulana ni faida kubwa kwa ngariba, hospitali na makanisa ambayo hutoza kati ya Sh10, 000 hadi Sh50, 000 kulingana na uwezo wa kifedha wa familia.

Kulingana na Bw Kung’u, mabadiliko ya kila mara ya mtaala wa masomo yamevuruga umri wa kutahiriwa kwa wavulana “kwa hivyo tunapaswa kushikilia miaka 14 kama umri faafu kwa wavulana kupashwa tohara.”

Mgawanyiko miongoni mwa wazee wa jamii ya Agikuyu kuhusiana na suala hili umewakanganya wazazi wanaoamini kuwa wazee ndio wenye usemi mkubwa katika uwekaji mwaka wa tohara.

Chanzo : Taifa letu

No comments