HEADER AD

HEADER AD

ALLY KARUME ALIYESUMBULIWA NA UVIMBE AFANYIWA UPASUAJI MUHIMBILI

>>Atolewa nyama yenye uzito wa kilo tano iliyomtesa kwa miaka 25

>>Mgonjwa huyo aliibuliwa na Chama cha Waandishi wa Habari mkoa wa Dar es Salaam

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam 

Kalume Ally Kalume mwenye umri wa miaka 41 aliyekuwa akisumbuliwa na nyama zilizoota sehemu mbalimbali za mwili wake kwa zaidi ya miaka 25 amefanyiwa upasuaji na ameruhusiwa kwenda nyumbani.

Karume amefanyiwa upasuaji rekebishi na watalaam wa hospitali ya Taifa Muhimbili wakiongozwa na Daktari bingwa mbobezi wa upasuaji rekebishi ambaye pia ni mkuu wa kitengo cha upasuaji rekebishi, Dkt. Laurean Rwanyuma.

Ally Karume Ally akiwa amepatiwa matibabu hospitali ya Taifa Muhimbili kwa kuondolewa uvimbe mwilini mwake.

Daktari bingwa mbobezi wa upasuaji Rekebishi ambaye pia ni mkuu wa Kitengo cha upasuaji Rekebishi Dkt. Laurean Rwanyuma aliyeongoza jopo la watalaam amezungumza na waandishi wa habari

Dkt. huyo amesema kuwa upasuaji huo ulidumu kwa saa nne baada ya uchunguzi wa kina kukamilika, iligundulika kuwa Kalume ana uvimbe sehemu mbalimbali za mwili wake hasa shingoni, begani na kifuani.

  Mkurugenzi wa Upasuaji katika hospital ya Taifa ya Muhimbili Dk. Rachel Mhavile aliyevaa miwani , katikati ni  Daktari bingwa mbobezi wa upasuaji rekebishi ambaye pia ni mkuu wa kitengo cha upasuaji rekebishi, Dkt. Laurean Rwanyuma wakiwa na Ally Karume Ally ( wa kwanza kulia).

" Ugonjwa huo unaitwa Plexiform Neurofibromatosis ambao matibabu yake ni kuondolewa kwa njia ya upasuaji ambapo Agosti 30 mwaka huu alifanyiwa upasuaji.

" Ugonjwa aliopata Karume siyo wa kuambukiza bali ni ugonjwa wa kuzaliwa nao ambao ameurithi kutoka kwa ama mmoja wa wazazi wake au wazazi wake wawili wenye ugonjwa huo ambao hushambulia mishipa ya fahamu na kujitokeza kwa njia mbalimbali.

Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji, Dkt. Rachel Mhaville akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali hiyo, amesema baada ya kumpokea Karume agosti mwaka huu, hospitali ilifanya jitihada za dhati kuhakikisha Kalume anaonwa na madaktari bingwa na kumfanyia vipimo mbalimbali ili kubaini mwenendo wa matibabu yake.

     Naibu Meya wa manispaa ya Kinondoni Michael Urio (wa pili kulia) pamoja na Mkurugenzi wa Upasuaji katika hospital ya Taifa ya Muhimbili Dk. Rachel Mhavile ( wa kwanza kulia) , wakimjulia hali Ally Karume Ally aliyekaa kitandani .

"Nawapongeza waandishi wa habari kumuibua mgonjwa huyo na kumleta hospitalini ya Muhimbili kwani ndipo penye madaktari bingwa bobezi wa upasuaji rekebishi walioweza kumpa huduma stahiki na kumrejeshea mwonekano unaompa faraja na tabasamu.

Dkt. Mhaville amewaomba wasamaria wema kuendelea kujitokeza kuchangia huduma kwa watu wasiokuwa na uwezo akiwemo Kalume ili kukamilisha malipo ya huduma alizopata kupitia namba ya malipo 994501766575 yenye jina Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Mjomba wa Karume Salum Ahamad Idobelele amesema alianza kuangaika na Karume akiwa na miaka 16 baada ya kupata uvimbe huo na baadae kubahatika mwaka huu kukutana na waandishi wa habari kupitia Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Dar es Salaam (DCPC).


         Ally Karume Ally kabla ya kufanyiwa upasuaji

Amesema Chama cha Waandishi wa habari Dar es Salaam ambao walibeba jukumu la kumtafutia msaada wa matibabu kwa kumpeleka Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Temeke na kisha kupewa rufaa ya kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Awali Naibu Meya wa Manispaa ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam, Michael Urio akiwa amemtembelea mgonjwa huyo hospitali ya Muhimbili aliwaomba watanzania wakiwemo viongozi wa serikali kumsaidia matibabu na huduma mbalimbali Ally Karume Ally  mkazi wa Kilungule Mbagala, Wilaya ya Temeke kama ilivyoripotiwa katika chombo hiki cha habari Agasti, 27, 2024.

Naibu Meya wa manispaa ya Kinondoni Michael Urio akizungumza na Ally Karume wakati alipomtembelea kumjulia hali.

Naibu Meya alifika katika hospitali hiyo Agasti, 27, 2024 kumjulia hali mgonjwa huyo anayesimamiwa kwa ukaribu na Klabu ya Waandishi wa Habari mkoa wa Dar es Salaam (DCPC).

Mwakilishi wa kamati ya kuratibu matibabu ya mgonjwa huyo kutoka Chama cha waandishi wa habari mkoa wa Dar es Salaam (DCPC), Careen Mgonja, ameishukuru Hospitali ya Taifa Muhimbili kuwa karibu na mgonjwa huyo katika kumpatia matibau huku akiomba wadau na watu mbalimbali kuendelea kuchangia kupitia namba maalum iliyotajwa na Dkt. Mhaville.

       Mwakilishi wa kamati ya kuratibu matibabu ya mgonjwa huyo kutoka Chama cha waandishi wa habari mkoa wa Dar es Salaam (DCPC), Careen Mgonja, kushoto ni mjomba wa Ally Karume Salum Ahamad Idobelele.




No comments