HEADER AD

HEADER AD

WENYEVITI WA VITONGOJI MASWA WATAKA WALIPWE FEDHA ZAO

>>“Fedha zetu zimekuwa zikitoka lakini zimeliwa na watumishi wa Halmashauri, ukiangalia baadhi ya nyaraka utakuta wameweka vivuli vya kuonyesha sisi tumelipwa kumbe hapana".


Na Samwel Mwanga, Maswa

WAJUMBE wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Maswa mkoani Simiyu ambao ni Wenyeviti wa Vitongoji katika Kata nne ndani ya mji wa Maswa wameitaka mamlaka ya mji mdogo wa Maswa kuwalipa fedha zao.

Wenyeviti hao wa Vitongoji ni wa kutoka Kata ya Sola, Nyalikungu , Binza na Shanwa wameiomba serikali kuhakikisha wanalipwa fedha zao zote wanazodai kabla ya kumaliza muda wao Oktoba 25, mwaka huu ili kupisha uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajia kufanyika Novemba 27 mwaka huu.

Wakizungumza  katika kikao cha Baraza la Mamlaka ya mji huo wajumbe hao wamesema kuwa wamekuwa wakitoa huduma muhimu kwa jamii lakini malipo yao yamekuwa wakicheleshwa kwa muda mrefu na kufanya deni kuwa kubwa la Tsh 152,533,050.

       Wajumbe wa Mamlaka ya Mji mdogo wa Maswa wakiwa katika Kikao cha Baraza la Mamlaka hiyo

Wameitaka Serikali kupitia kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Maswa ambaye ndiye mwenye jukumu la kuwalipa fedha zao ambazo ni pamoja na posho za vikao, posho za madaraka na posho za mwezi kuwalipa kabla ya kumaliza muda wao wa uongozi.

Mwenyekiti wa Kitongoji wa Majebele George Gogadi amesema kuwa kabla ya kulipwa ni vizuri nao wajiridhishe uhakiki ambao utafanywa na mkaguzi wa ndani wa hesabu wa halmashauri ya wilaya hiyo.

         Mwenyekiti wa Kitongoji cha Majebele,George Gogadi akitoa mchango wake wa Mawazo katika kikao cha Baraza la Mamlaka ya mji mdogo wa Maswa.

Amesema kuna uonevu wa kudhulumiwa maana kumekuwa na sintofahamu juu ya deni halisi wanalodai na hawahakikishiwi watalipwa lini.

Madaraka Saira ni Mwenyekiti wa Kitongoji wa kiwanja cha Ndege amesema kuwa fedha walizopaswa kulipwa zimekuwa zikitoka na kuliwa na baadhi ya watumishi wa halmashauri hiyo ambao wamekuwa wakinufaika na fedha zao jambo ambalo si sahihi na halipaswi kufumbiwa macho.

“Fedha zetu zimekuwa zikitoka lakini zimeliwa na watumishi wa Halmashauri, ukiangalia baadhi ya nyaraka utakuta wameweka vivuli vya kuonyesha sisi tumelipwa kumbe hapana wakati wapo wanufaika wa hizi fedha wamekuwa wakitumia jasho letu kuneemeka na kununua magari tu,”amesema.

Nkinda Idama ni Mwenyekiti wa Kitongoji cha Nyabiti amesema kuwa fedha zao zimeliwa na yuko tayari kuandaa maandamano kwenda ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa ili kudai haki yake na hata ogopa mabomu ya polisi.

        Wajumbe wa Mamlaka ya Mji mdogo wa Maswa wakiwa katika Kikao cha Baraza la Mamlaka hiyo.

“Mie niko tayari kuandamana kwenda kwenye ofisi ya Mkurugenzi kudai haki yangu na waandae na polisi wa kutupiga mabomu mie niko tayari na wala siogopi kupotezwa na watu wenye madaraka na fedha wakati nikidai haki yangu,”amesema.

Naye Solo Petro ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Mamlaka hiyo amesema kuwa ni jambo la kushangaza  ni kitendo cha watumishi wa halmashauri kuchukua posho za wajumbe wa Mamlaka hiyo ambayo ni Tsh. 20,000 kwa kila mmoja katika kila kikao na kuwataka wamuogope Mungu kwa matendo yao ya kuwadhulumu fedha zao na kutoa visingizio kuwa wamewalipa.

Mwenyekiti wa Mamlaka hiyo, Augustino Kabuta anasema kuwa kitendo cha kuiba fedha za wajumbe hao na kuharibu sifa ya Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Mji Mdogo(TEO),Saimon Nyadwera na kumtaka aandike tena madeni ya wajumbe hao wakati fedha zilishalipwa na kuliwa na baadhi ya watendaji wa halmashauri ya wilaya ya Maswa jambo hilo haliwezekani kuachwa hivyo hivyo ni lazima wote waliohusika wawajibishwe na ikibidi wafikishwe kwenye vyombo vya sheria.

“Ninazo taarifa sahihi kuwa fedha zetu zimeliwa pale halmashauri ya wilaya kwa maana zipo nyaraka zinaonyesha kuwa zimelipwa lakini hazijatufikia lakini kitendo cha kumtaka T.E.O aandike tena madokezo ya kuomba fedha zilizolipwa ni kutaka kumuingiza kwenye matatizo na kumchafua bure ni vizuri suala hili vyombo vinavyohusika vikalishughukilia huu ni wizi unaofanywa na watumishi wa Serikali,”amesema.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Mji Mdogo(TEO) wa Maswa, Saimon Nyadwera amesema kuwa baada ya kupitia nyaraka mbalimbali za madeni ya wajumbe wa mamlaka hiyo kwa kushirikiana na mwakilishi wa afisa utumishi wa Halmashauri hiyo,Shafii Athuman imebainika kuwa deni halisi ni Tsh. 152,533,050 na kuliwasilisha kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo.

         Afisa Mtendaji Mkuu,Mamlaka ya Mji mdogo wa Maswa,Saimon Nyadwera(aliyesimama)akitoa ufafanuzi wakati wa kikao cha Baraza la Mamlaka hiyo.

" Lakini cha kushangaza akapata taarifa ya kuwa kiasi cha Tsh 139,000,000 kimelipwa jambo ambalo hadi sasa linaleta mkanganyiko.

“Uhakiki tulioufanya tulipata deni la Tsh. 152,533,050 lakini baadae tukaelezwa kuwa tufanye tena upya kazi hiyo kwa kuangalia nyaraka la vikao ambazo ni mahudhurio ya mihutasari lakini tukakuta nyaraka nyingine hazipo licha ya kikao kufanyika.

Ikaonesha ya kuwa Tsh. Milioni 139 imelipwa, hapo ndipo sintofahamu ilipoanzia ila kwa kuna Mkaguzi wa ndani anaifanya kazi ya kuhakiki deni tena ngoja tuwe na subira,”amesema.

Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashuri hiyo, Henry Rweyemamu amesema kuwa kwa sasa wanasubiri taarifa kutoka kwa mkaguzi wa ndani wa hesabu wa halmashauri ya wilaya ya Maswa ili aweze kubaini deni halisi ni lipi ili waweze kulilipa kabla ya wajumbe hao kumaliza muda wao.

Mamlaka ya mji Mdogo wa Maswa ina jumla ya wajumbe 56 ambao wote ni wanatokana na Chama cha Mapinduzi(CCM).

Mamlaka ya Mji mdogo wa Maswa ilianzishwa rasmi Machi 3, 2010 kupitia tangazo la Serikali GN No 356 la Septemba 14, 2004, Mamlaka za Miji midogo huanzishwa kwa mujibu wa kifungu 16 na 17 cha Sheria za Serikali za Mitaa(Mamlaka za wilaya)na kifungu cha 7 ya mwaka 1982.




No comments