HEADER AD

HEADER AD

DKT. MPANGO AKERWA KUONA WATU WA IMANI MOJA YA KIDINI WAKISHINDWA KUELEWANA

" Tunashuhudia maugomvi, vurugu miongoni mwa waumini wa imani moja. Viongozi wanafukuzana kwenye nyumba za ibada.

Naona nyaraka mitandaoni zilizojaa tuhuma za matumizi mabaya ya fedha, kugombania madaraka, ajira za upendeleo, rushwa, kuhamishana kwasababu ya maokoto ".

Na DIMA Online, Arusha

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango amewataka viongozi wa dini na waumini wa madhahebu mbalimbali ya dini Afrika ikiwemo Tanzania kuheshimiana na kustahimiliana kwakuwa watu wote wameumbwa na Mungu.

Pia amesema kuwa kitendo cha viongozi wa dini na waumini kushindwa kuheshimiana kwa sababu ya tofauti za kiimani kunaweza kuchochea vita na migogoro katika mataifa mbalimbali na kisababisha vurugu, vifo, na hata kuathiri uchumi na maendeleo kwa nchi husika.

Dkt. Mpango ameyasema hayo Septemba, 20, 2024 wakati wa kufunga  kongamano la nne la Uhuru wa kidini Barani Afrika Kanisa la Waadventista Wasabato lililofanyika uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Jijini Arusha nchini Tanzania.

    Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akizungumza wakati wa kufunga kongamano la Uhuru wa kidini Barani Afrika.

Kongamano la Uhuru wa kidini Barani Afrika ufanyika kila baadae ya miaka minne au mitano ambapo wawakilishi kutoka nchi zaidi ya 40 wameshiriki kongamano hilo nchini wakiwemo viongozi wa madhehebu mbalimbali ya ya dini, viongozi wa serikali.

Dkt. Mpango amesema kuwa bado kuna changamoto ya watu wa imani tofauti ya kidini kuishi pamoja kwa amani huku watu wenye imani moja ya kidini  wakishindwa kuishi pamoja kwa amani.

" Mimi ninapoitazama Tanzania na nchi zingine katika Bara la Afrika ninaona changamoto mbalimbali . Haya nitakayosema hayalengi dhehebu lolote la dini naomba radhi kama itaonekana kugusa dhehebu fulani.

"Kuna changamoto ya watu wa imani tofauti ya kidini kuishi pamoja kwa amani. Sura nyingine ninayoiona ni ile ya watu wa imani moja ya kidini kushindwa kuishi pamoja kwa amani.

"Siku hizi tunashuhudia maugonvi, vurugu za aina mbalimbali miongoni mwa waumini wa imani moja, baadhi ya viongozi wa dini, wachungaji, mashehe, maustadhi, wazee wa makanisa n.k., viongozi wanaondoana au wanafukuzana kwenye nyumba za ibada" amesema Makamu wa Rais.

Ameongeza kusema " Hata kwenu ndugu zangu Waadventista Wasabato ninaona nyaraka mbalimbali kwenye mitandao. Mf. Ni yule anayejulikana kama jicho la mwewe sasa sijui kama hayupo hapa uwanjani leo.

" Kwenye nyaraka hizo kumejaa tuhuma nyingi zinazojumuisha matumizi mabaya ya fedha na mali za kanisa, kugombea madaraka, kuajiriana kwa upendeleo, rushwa na  kukosekana kwa haki kwenye chaguzi katika ngazi za Union, Conference na Field.

" Hata katika madhehebu mengine ya dini mambo ni hayo hayo japo viwango vinatofautiana nako ninaona kuna kuenguana kwa uongozi, kuhamishwa kutoka kwenye mitaa, usharika, vigango, parokia au misikiti na hasa ile yenye sadaka kubwa na kupelekwa kwenye vituo vyenye maokoto mdogo" amesema Dkt. Mpango.

Ameshangazwa kwa kuwepo tuhuma za ushirikina katika Dini ambapo amesema baadhi ya mambo hayo yanatokana na baadhi ya viongozi kugeuza dini kuwa ajira badala ya utumishi kwa Mungu.

    Vijana wa kiadventista wakimpokea mgeni Rasmi  Makamu wa Rais Dkt.Philip Mpango.

Na wakati mwingine tofauti miongoni mwetu zinatokana na tafsiri tofauti ya maandiko na kila mtu akijiona ndiye mwenye tafsiri sahihi. Washiriki wa kongamano , waumini , viongozi wetu wa dini mnayo nafasi na heshima ya pekee sana katika jamii yetu hapa Tanzania na katika nchi zote za Afrika kama wawakilishi wa Mungu hapa Duniani.

Ametoa rai kwa watumishi wote wa Mungu kudhibiti tamaa ya mali na kujinyenyekeza kwa Mungu na kuhakikisha wanasemana na kuonyana kwa upendo au kindugu kanisani au kwenye misikiti na sio kutumia mitandao ya kijamii.

" Nafikiri jambo muhimu ni kudhibiti tamaa za mali zilizopitiliza, watu wanataka magari na nyumba za kifahari, wanataka fedha .n.k , lakini pia uchu wa madaraka. Rudini kwenye wito halisi wa kumtumikia Mungu.

" Nawaombea sana tujinyeyekeze kwa Mungu. Mimi ninaamini yafaa turudi kwenye utaratibu wetu mzuri wa kusemana na kuonyana kwa upendo na undugu kanisani au msikitini badala ya kuhamia mitandaoni.

Tusipofanya hivyo itakuwa vigumu sana kuhubiri na kujenga tunu ya kuishi pamoja na wenzetu wa imani tofauti wakati sisi watu wa imani moja tunashindwa kuishi pamoja kwa amani" amesema Dkt. Mpango.

Ameongeza kuwa baadhi ya migogoro inayotokea Afrika inatokana na imani kali za kidini na kwamba taarifa zinaonesha takribani vifo vilivyohusisha na ugaidi Duniani vilivyotokea katika eneo la Sahara .

"Itikadi zingine za Dini zimeenea katika nchi zingine za bara la Afrika kama vile, Nigeria, Msumbiji, Somalia na Sudan na kusababisha vifo, utekaji na watu kuyakimbia makazi yao " amesema Dkt Mpango.

Viongozi wa dini kujihusisha na siasa

Makamu wa Rais ameonesha kukerwa na kitendo cha baadhi ya viongozi wa Dini au dhehebu moja kujihambatanisha na chama mojawapo cha siasa na kupelekea maoni yao binafsi ya kisiasa kutafsiriwa kuwa ndiyo maoni ya dini au dhehebu analoliongoza.

" Katika hali kama hiyo itakuwa ni vigumu sana kwa wafuasi wengine wa vyama vya kisiasa kuishi pamoja kwa usalama na utulivu na watu wa chama kingine chenye mlengo tofauti wa kisiasa. 

"Hili ni jambo la hatari kwenye umoja wa kitaifa, hali kama hiyo inaleta changamoto kubwa katika uhusiano na mashirikiano baina ya Serikali ambayo haina dini" amesema.

Dkt. Mpango amesema kuna baadhi ya viongozi wa dini wenye mlengo dhahili wa kisiasa huku akitoa wito kwa viongozi wa dini kutochanganya dini na siasa.

Asisitiza maadili mema

Kiongozi huyo amesisitiza maadili mema katika jamii kwani ni njia mojawapo katika kujenga jamii yenye amani na utulivu kwamba Dini zina mchango katika kujenga familia njema zenye maadili mema na kwamba familia na jamii zinazozingatia mafunzo ya dini zinazingatia pia maadili mema na hivyo kupelekea jamii kuishi katika hali ya usalama na utulivu.

" Palipo na mmomonyoko wa maadili vitendo viovu kama vile ; unyang'anyi, matumizi ya dawa za kulevya, ulevi wa pombe, uasherati, ubakaji, ulawiti, ushoga , matukio ya kikatili, ukatili wa kijinsia, ukatili dhidi ya watoto na wanawake na ubadhilifu wa mali za umma vinashamili.

Hivyo, amewasihi viongozi wa dini na waumini wote kusimamia kikamilifu suala la maadili mema katika jamii, kuanzia kwa wazazi na walezi, vijana na watoto .

Akizungumzia uhuru wa Dini, amesema uhuru wa Dini uliopo nchini una misingi yake katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 19 inayompa mtu uhuru wa kuamini dini atakayo na hatua mbalimbali zilizochukuliwa na waasisi mbalimbali wa nchi.

Amesema Serikali inashirikiana kwa karibu na viongozi wote wa dini na hasa katika sekta ya elimu na afya na kushirikiana katika changamoto mbalimbali zinazojitokeza na kuhakikisha shughuli za kidini zinaendeshwa kwa amani na utulivu hapa nchini.

Dkt. Mpango ameshukuru kwa zawadi iliyotolewa na na Kanisa la Waadventista Wasabato Barani Afrika kuitunuku Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Rais wake Dkt. Samia Suluhu Hassan zawadi kwa nchi ya Tanzania kwa kutunza amani ya watu wote bila kujali Dini za imani zao katika Bara la Afrika.

Pia ameahidi kwa niaba ya Serikali kuwa amepokea changamoto zilizotajwa ikiwemo ya usaili na mitihani kufanyika siku ya Sabato na kwamba serikali itayafanyia kazi maombi yao.

Akitoa shukrani kwa niaba ya Kanisa la Waadventista Wasabato, Mwenyekiti wa Kanisa la Waadventista Wasabato Jimbo Kuu la Kusini mwa Tanzania, Mch. Dkt. Goodwin Lekundayo amemshukuru Makamu wa Rais aliyemwakilisha Rais Dkt . Samia Suluhu Hassan kufika katika kongamano hilo na kuahidi kuwa Kanisa limepokea na kuzifanyia kazi changamoto zilizotajwa na Makamu wa Rais.

         Mwenyekiti wa Kanisa la Waadventista Wasabato Jimbo Kuu la Kusini mwa Tanzania, Mch. Dkt. Goodwin Lekundayo akizungumza wakati wa kufunga kongamano.

Amesema watajitahidi kukaa kujadili tofauti zao zinazojitokeza badala ya kulumbana kwa njia ya mitandao ya kijamii na kwamba viongozi wa dini wanawajibu wa kuwalea wale wanaowaongoza katika maadili ya kuwafanya kuwa na hofu kwa Mungu ambayo itafanya kuwa raia wema na kuzidi kuliombea taifa na viongozi.


No comments