DED AWAHAMASISHA WANANCHI KUJITOKEZA UANDIKISHAJI DAFTARI LA WAPIGA KURA SERIKALI ZA MITAA
Na Gustaphu Haule, Pwani
MKURUGENZI wa Halmashauri ya Mji Kibaha Dkt. Rogers Shemwelekwa amewaangukia viongozi wa makundi mbalimbali wakiwemo viongozi wa dini, vyama vya Siasa, makundi ya watu wenye ulemavu na wazee maarufu kuwa mabalozi wazuri katika kuhamasisha wananchi kushiriki kwenye michakato ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Dkt.Shemwekwa ametoa kauli hiyo Septemba 26 mwaka huu wakati akifungua kikao maalum cha kutoa elimu ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa viongozi wa makundi hao kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri hiyo.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kibaha Dkt.Rogers Shemwelekwa akifungua kikao cha viongozi wa makundi mbalimbali ikiwa sehemu ya uhamasishaji Wananchi kujitokeza katika michakato ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa.Amesema kuwa, makundi ya viongozi hao ni muhimu kwakuwa wanauwezo na nafasi kubwa ya kuwaelimisha na kuwahamasisha wananchi kujitokeza katika michakato mbalimbali ya uchaguzi huo .
Shemwelekwa ametumia nafasi hiyo kuwaomba wananchi kujitokeza katika kujiandikisha katika daftari la wapiga kura zoezi ambalo litaanza kufanyika Oktoba 11 mpaka Oktoba 24 ,2024.
Amesema kuwa,mtu yeyote mwenye umri wa miaka 18 na kuendelea anasifa za kushiriki uchaguzi huo ikiwa pamoja na kupiga kura kumchagua kiongozi anayemtaka lakini wagombea katika uchaguzi huo wanatakiwa kuanza na umri wa miaka 21 na kuendelea.
"Niwaombe viongozi wangu twende tukatimize wajibu wetu wa kuhamasisha wananchi kujitokeza kujiandikisha katika daftari la wapiga kura kuanzia Oktoba 11 na hata kupiga kura ifikapo Novemba 27 mwaka huu,"amesema Shemwelekwa.
Katika kikao hicho baadhi ya viongozi wa taasisi za Serikali ikiwemo Jeshi la Polisi,Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU) pamoja na Uhamiaji walishiriki sambamba na kutoa maelekezo mbalimbali.
Afisa kutoka Takukuru Mwanyika Senzota, amesema kuwa uchaguzi wa Serikali ya Mtaa ni haki ya kikatiba lakini ni suala la maendeleo ambalo linatoa dira ya nchi inavyotaka kufikia malengo yake .
Afisa wa Takukuru Mkoa wa Pwani Mwanyika Senzota akizungumza katika kikao cha viongozi wa makundi mbalimbali kilichoandaliwa na Halmashauri ya mji Kibaha kuhusu uhamasishaji wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa.Senzota amesema Wananchi watumie haki yao kuchagua viongozi wa Mitaa na hata kuchaguliwa kwa kufuata misingi ya uchaguzi huo na kwamba kama kuna viashiria vya rushwa basi ni vyema wakatoa taarifa haraka ili hatua zichukuliwe.
"Viongozi kemeeni suala la rushwa katika uchaguzi na kama mkiona mahali popote kuna viashiria vya rushwa ni vyema mkatoa taarifa kwani Takukuru ipo macho na inafanyakazi muda wote ,"amesema Senzota.
Senzota amewasihi viongozi hao kuacha kuwa sehemu ya kushinikiza kupokea rushwa katika uchaguzi huo kwani kufanya hivyo ni kosa la kukwamisha uchaguzi huo huku kiongozi atakayebainika kufanya hivyo hatoachwa .
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani Pius Lutumo, amesema Jeshi lake limejipanga kikamilifu kudhibiti vitendo vyote vya uhalifu katika uchaguzi huo ambapo amewaomba viongozi hao kwenda kuwa sehemu ya kuhubiri amani.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani Pius Lutumo katika kikao cha makundi ya viongozi mbalimbali walioshiriki kikao cha uhamasishaji masuala ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa." Viongozi nendeni kuwa mabalozi wazuri wa kuhubiri amani katika uchaguzi maana Tanzania itakuwepo hata baada ya uchaguzi na sisi Jeshi la Polisi tumejiandaa na tupo timamu kiakili,vifaa na hata nguvu katika kudhibiti vitendo vyote vya kihalifu katika uchaguzi huo,"amesema Lutumo.
Hatahivyo, Lutumo amesema kazi ya Jeshi la Polisi pamoja na kukamata wahalifu katika maeneo mengine lakini hata katika uchaguzi wahalifu wapo na wakikamatwa watachukuliwa hatua kwa utaratibu wa Jeshi unavyoelekeza.
Post a Comment