HEADER AD

HEADER AD

WALIOLALAMIKA MBELE YA RC SIMIYU KUHUSU UWEPO MATUKIO YA MAUAJI, UTEKAJI WAKAMATWA

>>Ni baada ya kushindwa kuthibitisha malalamiko yao mbele ya RC

>>RC aagiza Polisi kuwakamata ili wakatoe maelezo ya kina

Na Samwel Mwanga,Maswa

BAADHI ya wananchi wilayani Maswa mkoa wa Simiyu, wamekamatwa na jeshi la Polisi kwa tuhuma za kutoa taarifa wasizokuwa na uthibitisho nazo zikihusisha uwepo wa matukio ya mauaji na utekaji.

Wananchi hao walikuwa wakitoa malalamiko yao mbele ya mkuu wa mkoa wa Simiyu, Kenani Kihongosi juu ya uwepo wa vitendo hivyo vikiwemo vya watu kuuawa na kutolewa nyongo.

Mkazi wa kijiji cha Mbaragane Constantine Samo, amesema kuwa kwa sasa kumekuwa na matukio ya watu kuuawa na kutolewa nyongo  hivyo kumtaka Kamanda wa polisi Mkoa (RPC) Simiyu na Mkuu wa polisi wa Wilaya (OCD) Maswa kutoa maelezo ya kina juu ya kuwepo kwa matukio hayo.

       Costantine Samo mkazi wa kijiji cha Mbaragane wilaya ya Maswa akitoa malalamiko yake katika mkutano wa hadhara ulioitishwa na Mkuu wa mkoa wa Simiyu,Kenani Kihongosi.

Mkazi wa kijiji cha Sangamwalugesha  Festo Mikael ametoa malalamiko mbele ya Mkuu huyo wa mkoa kuwa hali ya ulinzi na usalama si shwari kutokana na kuwepo kwa vitendo vya watoto kuuawa,kupotea na kutekwa.

Amesema kuwa kwa sasa wananchi wa maeneo hayo wanaishi kwa mashaka  kwani ikifika majira ya saa 12:00 jioni ni lazima wawepo ndani ya nyumba kwa kuhofia maisha yao na ya watoto wao.

      Festo Mikael mkazi wa kijiji cha Sangamwalugesha wilaya ya Maswa akiwa katika gari la polisi akisubiri kutoa maelezo juu ya tuhuma alizozitoa  za watoto kutekwa na kuuawa mbele ya Mkuu wa mkoa wa Simiyu,Kenani Kihongosi ambazo alishindwa kuzithibitisha.

“Hapa Sangamwalugesha tuna shida roho ziko hatihati ,wananchi wanaishi kwa mashaka ikifika jioni saa 12:00 jioni unakaa ndani na mtoto kwa kuhofia vitendo vya kutekwa, kupotezwa na kuuawa wakati jeshi letu la polisi lipo lakini maisha yetu yana dukuduku,”amesema.

Pia amesema kuwa changamoto nyingine inayowakabili wananchi wa eneo hilo, ni pamoja na kutokuwepo kwa huduma za afya za zahanati ya kijiji hicho licha ya kuwa na kadi ya matibabu huku watoto wenye umri chini ya miaka mitano wakitozwa fedha za matibabu laikini taratibu zinataka watibiwe bure.

“Unapokwenda kwenye kituo cha Afya au Zahanati ya serikali ukiwa na kadi ya matibabu ambayo umeshailipia ili upate huduma bure unapougua ukifika utapewa dawa aina ya panadol tu ila dawa za ina nyingine utaambiwa nenda kanunue kwenye duka la dawa hili jambo halikubaliki hata kidogo,”amesema.

Hata hivyo Mkuu wa mkoa wa Simiyu  Kenani Kihongosi aliwataka Festo Mikael  na Costantine Samo waweze kuthibitisha kuwepo kwa matukio hayo waliyoyaeleza mbele yake.

Mkuu wa mkoa wa Simiyu,Kenani Kihongosi akihutubia mkutano wa hadhara katika kijiji cha Sangamwalugesha wilayani Maswa

Wananchi hao waliposhindwa kuthibitisha RC Kihongosi alimwagiza Mkuu wa Polisi wilaya ya Maswa, Mrakibu Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SSP) Maganga Ngosha kuwachukua kwa lengo la kupata maelezo ya kina kutoka kwao juu ya malalamiko waliyoyatoa.

Costantine Samo mkazi wa kijiji cha Mbaragane wilaya ya Maswa akiwa katika gari la polisi akienda kutoa maelezo juu ya tuhuma alizozitoa  za watu  kuuawa na kutolewa nyongo mbele ya Mkuu wa mkoa wa Simiyu,Kenani Kihongosi.

RC Kihongosi ameonya dhidi ya utoaji wa taarifa za uongo ambazo zinaweza kusababisha taharuki katika jamii. 

Onyo hilo amelitoa jana kwa nyakati tofauti tofauti katika wilaya ya Maswa katika mikutano wa hadhara wakati akisikiliza kero za wananchi katika kijiji cha Sangamwalugesha na kijiji cha Mbaragane ili kuzuia uvumi na taarifa zisizo sahihi zinazoweza kuleta hofu, wasiwasi na kuchochea vurugu miongoni mwa wananchi.

Amesema kuwa kwa sasa imezuka tabia kwa baadhi ya wananchi kutoa taarifa za uongo za watu kutekwa, kupotea na kuuawa katika maeneo yao wakati matukio hayo hayajatokea hali ambayo inaweza kuvuruga amani na utulivu wa wananchi.

      Sehemu ya wananchi wa kijiji cha Mbaragane wilaya ni Maswa waliojitokeza kumsikiliza  Mkuu wa mkoa wa Simiyu,Kenani Kihongosi.

Pia ametoa wito kwa wananchi kuhakikisha wanapata taarifa sahihi kutoka kwenye vyanzo vya kuaminika na kuepuka kusambaza habari ambazo hazijathibitishwa.

      Sehemu ya wananchi wa kijiji cha Sangamwalugesha wilaya ya Maswa waliojitokeza kumsikiliza  Mkuu wa mkoa wa Simiyu,Kenani Kihongosi.

“Niwaulize wananchi katika Kijiji hiki cha Sangamwalugesha na Kata hii kuna matukio ya watoto kutekwa na kuuawa na kutolewa figo na kama hakuna  matukio kama hayo kama mlivyojibu inakuwaje mtu anakuja mbele ya mkutano na kutoa taarifa za uongo ambazo zinazozua taharuki kwa jamii”?alihoji.

“Tuache upotoshaji katika mikutano ya hadhara kama huu, tuache kutafuta umaarufu mbele za watu kwa kutoa taarifa za uongo tena mbele ya wananchi hii haikubaliki hata kidogo na midomo yetu iwe na kiasi mbele za watu " amesema.

Amesema ni lazima tukemee tabia hizi za baadhi ya watu kutoa taarifa za uongo ila kwa mkoa wa Simiyu hali ya ulinzi na usalama ni shwari kwa asilimia 100 na kuwataka wananchi kulinda amani katika eneo lao.

Mkuu wa mkoa wa Simiyu yuko katika ziara ya siku sita wilayani humo kwa lengo la kusikiliza na kutatua kero zinazowakabili wananchi wa wilaya ya Maswa.


No comments