KAMATI ZA MAAFA ZA WILAYA ZATAKIWA KUTENGENEZA MIONGOZO
Na Samwel Mwanga, Simiyu
KAMATI za Maafa za wilaya zimetakiwa kuandaa miongozo ya kupambana na maafa ili kuhakikisha usalama wa wananchi na mali zao una kuwepo wakati majanga yanapotokea.
Pia kamati hizo zina jukumu la kuhakikisha zinafanya maandalizi ya kutosha ya kukabiliana na maafa pindi yanapotokea.
Hayo yameelezwa Septemba,15 mwaka huu na Naibu Waziri,Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge)Ummy Nderiananga wakati akifungua mafunzo kwa kamati ya maafa ya wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu iliyofanyika katika ukumbi wa halmashauri ya Wilaya hiyo.
Naibu Waziri,Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera,Uratibu na Bunge) Ummy Nderiananga wakati akifungua mafunzo kwa kamati ya Maafa ya wilaya ya Maswa.
Amesema kuwa miongozo ya kukabiliana na maafa ni hatua muhimu itakayowezesha kufikia hatua muhimu zitakazochukuliwa ili kupunguza madhara na athari za maafa kuanzia ngazi ya chini hadi ya juu.
Naibu Waziri, Nderiananga amesema kuwa miongozo hii inajumuisha mikakati mbalimbali ambayo inaweza kufuatwa kabla, wakati, na baada ya maafa kutokea kwani hatua hizi zinahitaji maandalizi mazuri, rasilimali za kutosha,na ushirikiano kati ya taasisi, serikali, na jamii.
“Tutengeneze muongozo ambao utaonyesha iwapo yatatokea maafa katika maeneo yenu mnafanya nini katika ngazi ya Kijiji,Kata na Wilaya kwa msingi huo haya mafunzo ni hatua ya kwanza kwa hivyo mtatakiwa kwenda mbele zaidi kwa kuandaa miongozo hiyo ambayo itawasaidia pindi maafa yatakapotokea,”amesema.
Amesema kuwa miongozo inaweza kubadilishwa kulingana na aina ya maafa yanayotarajiwa na mahitaji ya jamii husika sambamba na ushirikiano na utekelezaji sahihi wa mikakati ambayo husaidia kupunguza athari za maafa na kuimarisha ustahimilivu wa jamii.
Mbunge wa Jimbo la Maswa Magharibi, Mashimba Ndaki amesema kuwa maafa yamekuwa yakitokea kila wakati katika jamii.
Mbunge wa jimbo la Maswa Magharibi,Mashimba Ndaki akifuatilia jambo wakati wa mafunzo ya kamati ya Maafa ya wilaya hiyo katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Maswa.
" Ofisi ya Waziri mkuu ndiyo inahusika na uratibu wa maafa kabla ya kutokea na baada ya kutokea hivyo nilishukuru Shirika la World Vision kwa kutuaanda kutupatia semina kwa kamati zetu za maafa za wilaya ili kujiandaa kabla na baada ili kukabiliana na maafa yanapotokea.
“Mheshimiwa Naibu Waziri,Ofisi ya Waziri Mkuu ndiyo inayoshughulika na Maafa kupitia kitengo cha Maafa na hapa mnashirikiana na wadau wa Maendeleo Shirika la World Vision Tanzania kutupatia mafunzo haya kwa kamati yetu ya maafa ili tuweze kujiandaa kuzuia na kukabiliana na maafa iwapo yatatokea katika jamii na sisi tuna jukumu la kwenda kuelimisha jamii yetu,”amesema.
Amesema kuwa mafunzo hayo yatasaidia kuongeza ufanisi wa juhudi za serikali za kupambana na maafa na kupunguza madhara yanayoweza kusababishwa na majanga mbalimbali.
Naye Mkuu wa wilaya ya Maswa, Aswege Kaminyoge amesema kuwa Ofisi ya waziri Mkuu imekuwa ikifanya kazi kubwa ya kukabiliana na maafa pindi yanapotokea.
Mkuu wa wilaya ya Maswa,Aswege Kaminyoge akiwa kwenye mafunzo ya kamati ya maafa ya wilaya hiyo
" Wajumbe wa Kamati ya Maafa Elekezi na Kamati ya Wataalamu ya wilaya hiyo walishawahi kupata mafunzo ya kukabilina na maafa hasa kipindi kile kilichobashiriwa kuwa na maafa kutokana na kuwepo kwa mvua nyingi musimu uliopita na maafa yalipotokea waliweza kuyakabili.
“Kwanza niipongeze Ofisi ya Waziri Mkuu inayopambana iwapo maafa yanapotokea, ni ukweli usiopingika sisi wajumbe wengi wetu tuliomo humu ukumbini tulipata mafunzo kutoka katika Ofisi ya Waziri mkuu juu ya kukabiliana na maafa yanapotokea.
" Katika kipindi kilichopita cha msimu wa mvua ambapo kulikuwa na mvua nyingi na maafa yalipotokea katika wilaya yetu kama kufurika kwa mto Mbaragane tuliweza kuyakabili,”amesema.
Awali Mkurugenzi Msaidizi, Operesheni na Uratibu, Idara ya Maafa,Ofisi ya Waziri Mkuu, Luteni Kanali,Selestine Masalamado amesema kuwa wameamua kutoa mafunzo hayo kwa kushirikiana na Shirika la World Vision ili kuzijengea uwezo kamati za Maafa za wilaya ziweze kuandaa mikakati ya kupunguza hatari za maafa kwa kuimarisha miundombinu na kutoa elimu kwa jamii juu ya namna ya kuepuka au kupunguza athari za maafa.
Naibu Waziri,Ofisi ya Waziri Mkuu(Sera,Uratibu na Bunge)Ummy Nderiananga wakati akifungua mafunzo kwa kamati ya Maafa ya wilaya ya Maswa.
Amesema kuwa tayari mafunzo haya yametolewa katika mikoa mbalimbali hapa nchini ikiwemo Tabora na Shinyanga na kwa mkoa wa Simiyu mafunzo hayo yatatolewa katika wilaya za Maswa,Itilima na Meatu.
“Mafunzo hayo kwa mkoa wa Simiyu yatatolewa katika wilaya za Maswa,Itilima na Meatu na kwa kipekee nilishukuru Shirika la World Vision Tanzania kwa ufadhili ambao umechangia kwa kiasi kikubwa jitihada za serikali katika kutekeleza kazi hii ya usimamizi wa Maafa,”amesema.
Post a Comment