Home
/
MICHEZO/BURUDANI
/
VETERAN KOMBAIN FC YAJINYAKULIA MILIONI MOJA MASHINDANO NANENANE NYONGO CUP
VETERAN KOMBAIN FC YAJINYAKULIA MILIONI MOJA MASHINDANO NANENANE NYONGO CUP
Na Samwel Mwanga, Maswa
MASHINDANO ya mchezo wa mpira wa Miguu ya Nane Nane Nyongo Cup yaliyoandaliwa na Naibu Waziri,Ofisi ya Rais,Mipango na Uwekezaji, Stanslaus Nyongo ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Maswa Mashariki mkoani Simiyu yamemalizika Septemba 15 mwaka huu katika uwanja wa Jamhuri, Nguzonane ulioko mjini Maswa.
Akifunga mashindano hayo Nyongo amesema kuwa amekuwa akifanya mashindano hayo kila mwaka mwezi agosti mjini humo kwa ajili ya kusherehekea sikukuu ya wakulima maarufu kwa jina la Nanenane lakini kwa mwaka huu kutokana na kuingiliana na kuwepo kwa mashindano mbalimbali yakiwemo yale ya Mwenge Cup yamefanyika mwezi Septemba.
Mbunge wa jimbo la Maswa MasharikiStanslaus Nyongo (wa kwanza kushoto) akizungumza na wachezaji wa timu ya Maswa Star na Veteran Kombani kabla ya mchezo wa fainali ya soka ya Nanenane Nyongo Cup 2024
Amesema mwaka jana wakati akitoa zawadi za washindi wa mashindano hayo alihaidi kuongeza zawadi kwa mashindano ya mwaka huu jambo ambalo amelitimiza kwa kuandaa zawadi ya Sh 1,000,000/=kwa mshindi wa kwanza,Sh 500,000/-kwa mshindi wa pili,Sh 300,000/-kwa Mshindi wa tatu na mshindi wa nne atapata jezi seti moja lakini pia atatoa seti moja moja ya jezi kwa mshindi wa kwanza hadi wa tatu.
“Nilihaidi kuwa kwa mashindano ya mwaka huu nitaongeza zawadi kwa washindi na nimefanya hivyo na jambo jingine jema hata mshindi wa nne naye atapata zawadi na hata wale washindi wa kwanza hadi wa tatu na wao nimewaongezea zawadi ya seti moja moja ya jezi,”amesema.
Amesema kuwa mashindano hayo yamekuwa mazuri sana licha ya kutokea kwa changamoto mbalimbali ambazo zimezua malalamiko kwa baadhi ya washabiki wa timu zilizoshiriki mashindano hayo kuwa kuna timu zinapendelewa jambo ambalo ameeleza kuwa ni kawaida katika mchezo wa soka hata kwa timu kubwa hapa nchini zinapokutana ambazo ni Simba na Yanga.
Sehemu ya washabiki na wapenzi wa soka wakifuatilia mchezo wa finali ya Nanenane Nyongo Cup kati ya Maswa Vetarani na Maswa Star katika uwanja na Jamhuri Nguzonane mjini Maswa
“Niombe radhi kwa mapungufu yaliyojitokeza wakati mashindano haya yakiendelea maana nimesikia malalamiko mengi lakini ukiona hivyo ujue mashindano yamekuwa mazuri kwenye mpira wa miguu malalamiko ni jambo la kawaida hata wakikutana Simba na Yanga ambazo ni timu kubwa hapa nchini malalamiko ni lazima yatakuwepo ila niwahaidi mashindano yajazo tutajipanga upya kwa kuunda kamati ya kuratibu mashindano haya vizuri,”amesema.
Mbunge Nyongo amesema kuwa kadri siku zinavyokwenda ataendelea kuyaboresha mashindano hayo na lengo kubwa ni kuwaweka vijana pamoja hasa wapenda soka sambamba na kuinua vipaji vyao ili waweze kuviendeleza huku akivipongeza Vyama vya Mpira wa Miguu wilaya ya Maswa na mkoa wa Simiyu kwa kusimamia mashindano hayo.
Mbunge wa jimbo la Maswa Mashariki,Stanslaus Nyongo (aliyekati) akifuatilia mchezo wa finali ya Nanenane Nyongo Cup kati ya Maswa Vetarani na Maswa Star katika uwanja na Jamhuri Nguzonane.
Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Mpira wa miguu mkoa wa Simiyu (SIFA) Kosuri Charles pamoja na kumpongeza Mbunge Nyongo kwa kuendelea kudhamini mashindano hayo amehaidi kuendelea kumuunga mkono katika kuendeleza mchezo wa soka katika wilaya hiyo na mkoa huo.
Amesema kuwa mbunge huyo ni familia ya mpira wa miguu na anapofanya mashindano hayo anajipambanunua kuwa ni mwanasoka na pia amewahi kushika nyadhifa mbalimbali katika Chama Cha Mpira wa Miguu wilaya ya Maswa(MDFA) na pia amewahi kuwa Mwenyekiti wa SIFA.
Sehemu ya washabiki na wapenzi wa soka wakifuatilia mchezo wa finali ya Nanenane Nyongo Cup kati ya Maswa Vetarani na Maswa Star katika uwanja na Jamhuri Nguzonane mjini Maswa
“Kaka yangu mheshimiwa Nyongo wewe ni familia ya mpira wa miguu katikia mkoa wa Simiyu na unafanya hivi si kwa sababu ya ubunge wako hapana kwani hata hiki cheo nilichonacho cha Mwenyekiti wa SIFA wewe ndiye uliniachia.
" Tunashukuru kwa kutuunga mkono kwa kuendelea kudhamini haya mashindano ya soka yenye jina la Nanenane Nyongo Cup na sisi SIFA tumekupatia heshima ya kuwa Mwenyekiti wa Heshima wa SIFA,”amesema.
Katika Mashindano hayo timu ya Maswa Veteran Kombaini Fc imeshika nafasi ya kwanza na kujipatia kitita cha sh 1,000,000/- na seti moja ya jezi,timu ya Maswa Star Fc imeshika nafasi ya pili na kujinyakulia kitita cha Sh 500,000/-na seti moja ya jezi,timu ya Maswa Warriours Fc imeshika nafasi ya tatu na kujipatia Sh 300,000/- na seti moja ya jezi na timu ya nne Maswa Sport Fc ilijipatia seti moja ya jezi.
Timu ya Veteran Kombaini Fc iliyotwaa Ubingwa wa kombe la Nanenane Nyongo Cup 2024
Sehemu ya washabiki na wapenzi wa soka wakifuatilia mchezo wa finali ya Nanenane Nyongo Cup kati ya Maswa Vetarani na Maswa Star katika uwanja na Jamhuri Nguzonane mjini Maswa
Post a Comment