HEADER AD

HEADER AD

MIGOGORO YA MIPAKA YA VIJIJI BIHARAMULO PASUA KICHWA UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA


Na Daniel Limbe, Biharamulo

MIGOGORO ya muda mrefu ya mipaka kwenye vijiji vya Nyamihongola, Lugese na Nyabugombe wilayani Biharamulo mkoani Kagera, imedaiwa kutishia jitihada za uchaguzi wa serikali za mitaa 2024 na ule wa serikali kuu mwakani 2025.

Ni kutokana na baadhi ya wananchi kushindwa kuelewa wako katika eneo lipi kutokana na vijiji hivyo kugombea mipaka kwa muda mrefu pasipo kupatikana suluhisho la changamoto hiyo kwa muda mrefu.

Diwani wa Kata ya Nyakahura, Apolinary Mugarula,amesema hayo kwenye kikao cha Baraza la madiwani lililolenga kuwasilisha na kujadili taarifa za Kata kwenye kikao cha robo ya nne ya mwaka wa fedha 2024/25, ambapo amesema migogoro hiyo huenda ikaathiri kwa kiwango kikubwa uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu hapo mwakani.

          Diwani wa Kata ya Nyakahura, Apolinary Mugarula

Amesema suala hilo limekuwa likiwasilishwa kila mara kwenye vikao vya madiwani wa halmashauri hiyo lakini hakuna jitihada za makusudi zilizofanyika ili kuondoa adha hiyo ambayo pia imekuwa ikitishia maisha ya baadhi ya wananchi.

Mbali na hilo,Mugarula amesema imekuwepo changamoto ya baadhi ya wananchi kuuza ardhi ovyo pasipo kufuata taratibu za kisheria hali inayochangia ongezeko la migogoro ya ardhi katika kata hiyo.

Kwa upande wake diwani wa Kata ya Kalenge, Erick Method,amelieleza Baraza hilo kuwa upo uwezekano mkubwa wa kutokea maafa kwenye kijiji cha Msekwa kutokana na ongezeko la wanyama aina ya viboko ambao wamekuwa wakivamia mashamba ya wakulima na kuathiri mazao yao.

        Madiwani wakiwa kwenye kikao cha Baraza lao

"Awali viboko hao walikuwa watatu baadaye wameongezeka hadi kufika zaidi ya 30 ambapo kwa sasa shughuli za kilimo cha bustani hakifanyiki tena kutokana na wanyama hao kuvamia mashamba na kuathiri mazao na kutishia uhai wa wananchi" amesema Method.

Hata hivyo katika hali isiyokuwa ya kawaida imeelezwa kuwa wanyama hao wamekuwa wakicheza na watoto wadogo wanapowakuta maeneo ya mashambani na kwenye mito,hali inayoweza kusababisha madhara kwa watoto ikiwemo vifo.

Kutokana na  hali hiyo ameiomba mamlaka inayohusika na Udhibiti wa wanyama poli kufika haraka eneo la kata ya Kalenge ili kuona namna ya kuwadhibiti kabla hawajasababisha madhara makubwa kwa jamii.

Akijibu malalamiko hayo, Ofisa maliasili wa halmashauri hiyo,Thomas Mahenge, amesema suala la viboko hao linaendelea kushughulikiwa kwa kuwasiliana na TAWIRI ambao ndiyo wenye mamlaka ya kuwahamisha wanyamapori.

        Mkuu wa Idara ya Wanyamapori wilaya ya Biharamulo,Thomas Mahenge

Aidha amesema kwa viboko wawili ambao wamezua taharuki kwa wananchi wa kijiji cha Ntumagu kata ya Nyanza ambao wameonekana kwenye makazi ya watu wakilanda mitaani.

Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya hiyo,Innocent Mkandala, amesema changamoto ya mipaka kwenye vijiji hivyo inatokana na wananchi kutoheshimu uamuzi wa wataalamu wa ardhi ambao walipima maeneo hayo awali na kutoa michoro ya maeneo hayo.

       Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya Biharamulo,Innocent Mkandala.

Aidha amesema atapeleka upya wataalamu wake maeneo hayo ili kufanya upimaji shirikishi na kwamba uamuzi utakapotolewa wananchi wanapaswa kuheshimu mipaka hiyo kulingana na michoro itakavyoonyeshwa.

   Baadhi ya madiwani wakiwa kwenye kikao cha Baraza lao


No comments