POLISI MUSOMA WAZINDUA KAMPENI YA KUWALINDA WATOTO
Na Jovina Massano, Musoma
KATIKA kuhakikisha usalama wa watoto unahimarishwa hapa nchini, Jeshi la Polisi wilaya ya Musoma mkoani Mara kupitia kitengo chake cha dawati la jinsia limezindua kampeni ya kuwalinda watoto yenye ujumbe usemao "Tuwaambie kabla hawajaharibiwa".
Ufunguzi huo ulioanza na maandamano kuanzia viwanja vya shule ya msingi Mukendo hadi viwanja vya Posta manispaa ya Musoma, yaliyowahusisha wanafunzi wa shule za msingi, sekondari na wanaojiandaa kwenda vyuoni.
Maandamano hayo yameungwa mkono na wazazi kutoka jumuia ya wazazi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) wilaya wakiambatana na mjumbe wa Baraza kuu wazazi Taifa Mgore Miraji Kigera.
Imeelezwa kuwa lengo la kampeni hiyo ni kupinga ukatili wa kijinsia na unyanyasaji kwa wanafunzi wawapo masomoni.
Mrakibu Mwandamizi wa Jeshi la Polisi wilaya ya Musoma Edson Mwamafupa akizungumza na wanafunzi agosti 30, 2024 amewataka kutokubali kurubuniwa,na kutokufumbia macho vitendo vya ukatili ambavyo vinakatisha ndoto zao katika maisha yao.
Mkuu wa Polisi wilaya ya Musoma Mrakibu mwandamizi wa Polisi Edson Mwamafupa akizindua Kampeni ya "Waambie kabla Hawajaharibiwa"
Pia amewataka wanafunzi kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi kitengo cha dawati la jinsia, walimu, wazazi, walezi au kwa viongozi wa dini pindi wanapoona viashiria au kufanyiwa vitendo vya ukatili.
Uzinduzi wa Kampeni hiyo unajili baada ya matukio ya ukatili kuendelea kuongezeka kwa wanafunzi katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
Mwamafupa amewaeleza wanafunzi hao kuwa vitendo vya ulawiti,ubakaji,utumiaji wa dawa za kulevya vyote hivi ni kinyume na sheria za nchi adhabu yake ni miaka 30 jela na kuendelea.
Hata hivyo mrakibu wa Polisi msaidizi kamishna wa kamisheni ya ushirikishwaji jamii mkoa, Henry Mbilinyi amewakumbusha na kuwaasa wazazi kuepuka kuwapa watoto biashara ambazo zinawapeleka katika mazingira hatarishi ili kuwalinda na ukatili.
Amewakumbusha wazazi kuwa na mahusiano ya karibu na walimu kuweza kusaidia malezi na makuzi sahihi kwa watoto kwani muda mwingi wazazi hivi Sasa hutumia katika utafutaji.
Mjumbe wa Baraza kuu wazazi Taifa Mgore Miraji amewahimiza wazazi kutowaacha watoto kutumia muda mwingi katika mitandao ya kijamii ambayo haimsaidii mtoto kuwa na maadili mema.
Ameongeza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan na serikali kwa ujumla kwa kuona umuhimu wa kuondoa ujinga ndani ya Taifa amewezesha upatikanaji wa elimu bure kuanzia shule ya msingi hadi kidato cha sita hii yote ni kuhakikisha tunakuwa na Taifa bora.
Sanjari na hayo viongozi wa jumuia ya wazazi wilaya wataendelea kutoa elimu ya kuwalinda watoto kila Kata ili kuondoa vitendo hivi vya ukatili katika jamii.
Mkuu wa dawati wilaya WP Herieti Tagata ameelezea kuwa Umalizaji wa kesi kwa makubaliano ya kulipana fidia kimya kimya na kuwaficha wahanga kutofika kwenye utoaji wa ushahidi kwa wazazi na walezi kunachangia Ongezeko la vitendo vya ukatili hivi katika jamii.
Wanafunzi wa darasa la Saba Paul Meng'anyi na Josephina Rameck wa shule ya msingi Azimio manispaa ya Musoma, wamewaomba wazazi na walezi wawe karibu na watoto wao.
Wamesema kuwa vitendo vya ukatili watekelezaji wakubwa ni watu wazima ambao ndio wangekuwa walinzi wakubwa kwa watoto.
Post a Comment