WANANCHI SIMIYU WAJITOKEZA KUJIANDIKISHA
Na Samwel Mwanga, Maswa
WANANCHI wa mkoa wa Simiyu wamejitokeza kujiandikisha na kuboresha taarifa zao kwenye zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ambalo limeanza leo katika mkoa na litaendelea kufanyika kwa muda wa siku saba hadi Septemba, 10 mwaka huu.
DIMA Online imeweza kutembelea baadhi ya vituo mbalimbali katika wilaya ya Maswa na kushuhudia uwepo wa wananchi vituoni haswa vijana wakijiandikisha kwa Maafisa wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).
Wakizungumzia mwenendo wa zoezi hilo wapiga kura waliojiandikisha wamesema kuwa linakwenda vizuri na hakuna usumbufu wa aina yoyote na wanapata huduma nzuri.
Nyadelu Maduhu mkazi wa kitongoji cha Mission amesema kuwa ameweza kuboresha taarifa zake vizuri bila ya usumbufu wa aina yoyote na ametoa wito kwa watu wengine wenye uhitaji kama huo wafike wajiandikishe.
"Nimefika katika kituo hiki kwa ajili ya kuboresha taarifa zangu katika daftari la kudumu la wapiga kura kwa ujumla hakuna usumbufu wowote nitumie fursa hii kuwaomba na wengine wafike ili waboreshe taarifa zao," amesema.
Happiness John mkazi wa Nghami amesema kuwa hakutegemea kupata huduma kwa urahisi lakini alipofika kujiandikisha akiwa mpiga kura mpya aliweza kuhudumiwa vizuri na sasa tayari amepata kadi yake.
Happiness Paul(aliyekaa kwenye kiti)akihudumiwa na Maafisa wa Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi alipofika kujiandikisha katika kituo cha Ghalani Kata ya Nyalikungu wilaya ya Maswa
"Mwanzoni wakati nakuja nilikuwa na wasiwasi juu ya usumbufu ambao niliona ninaweza kuupata lakini mambo yalikwenda tofauti nikapata huduma vizuri na kadi yangu ninayo sasa mkononi ikisubiri itumike ipasavyo mwaka 2025 kwenye uchaguzi Mkuu"amesema.
Manyangu Yasome mkazi wa Kata ya Nyalikungu anasema kuwa alipoteza kitambulisho chake cha mpiga kura lakini kwa sasa amepata kingine mara baada ya kufika kujiandikisha kwenye kituo cha WEO Nyalikungu na kuwahakikishia wananchi wengine waliopoteza vitambulisho vya mpiga kura kujitokeza kutumia hiyo fursa iliyotolewa na Tume hiyo.
Kwa nyakati tofauti wapiga kura waliojiandikisha na kuboresha taarifa zao wameishukuru INEC kwa kuboresha huduma kupitia matumizi ya teknolojia ya kisasa ambayo imerahisisha zoezi hilo jambo ambalo limepunguza muda wa kujiandikisha na kuboresha taarifa ambapo wameweza kupata kadi zao ndani ya dakika tatu hadi tano.
"Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imefanya maboresho makubwa kwani kwa sasa ndani ya dakika tano tayari unapata kadi yako unaendelea na majukumu mengine,"alisema Zengo Jilala mkazi wa mjini Maswa.
Mkuu wa wilaya ya Maswa, Aswege Kaminyoge ametoa wito kwa wananchi wote wa wilaya hiyo waliofikisha umri wa miaka 18, waliopotelewa na kadi ya mpiga kura na wale wanaotaka kuboresha taarifa zao wafike kwenye vituo vya kujiandikisha ili waweze lutumia haki yao ya kuwachagua viongozi wao katika uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Mwezi Oktoba 2025.
Post a Comment