HEADER AD

HEADER AD

MILIONI 224 ZACHANGWA PAROKIA YA MTAKATIFU MATHAYO NYAMWAGA


>>Nyambari Nyangwine achangia Milioni 42

>>DC Tarime asisitiza ushirikiano

>>Askofu Msongazila asema wanaotenda mema wasichukiwe

Na Dinna Maningo, Tarime

ZAIDI ya Milioni 224 zimechangwa kwaajili  ya ujenzi wa Kanisa Parokia ya Mtakatifu Mathayo Mwinjili lililopo Kijiji cha Keisangora katika Kata ya Nyamwaga, Jimbo Katoriki la Musoma.

Fedha hizo zimechangwa na waumini pamoja na wadau wa maendeleo katika harambee iliyofanyika Septemba, 29, 2024 kanisani hapo.

      Nyambari Nyangwine pamoja na wadau wa maendeleo waliofika kanisani kwenye harambee ya kuchangia ujenzi wa Kanisa. 

Kati ya fedha hizo Tsh. Milioni 42 zimechangwa na Nyambari Nyangwine aliyekuwa mgeni rasmi katika harambee ambaye pia aliwahi kuwa mbunge wa Jimbo la Tarime kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) mwaka 2010-2015.

Kati ya fedha hizo zilizotolewa na Nyambari, Tsh. Milioni 27 ametoa kwa ajili ya ujenzi wa kanisa na kutoa vitabu vya shule ya msingi inayomilikiwa na kanisa hilo venye thamani ya Tsh.Milioni 15.

      Nyambari Nyangwine akizungumza wakati wa harambee ya kuchangia ujenzi wa Kanisa 

"Nilipata wito wa baba askofu na baba Paroko wa kuwa mgeni rasmi kwenye harambee nikasema nitakuja. Siasa ni porojo lakini maendeleo ya watu hayawezi kutenganishwa na dini.

"Popote pale ambapo jamii zimeendelea Duniani aidha dini ilishika nafasi kubwa sana na siasa ndio ikafuata. Namshukuru mkuu wa wilaya ya Tarime na watu wote mlioshiriki katika suala hili la maendeleo" amesema Nyambari.

Pia Nyangwine amewaomba madiwani kutoogopa kuwatetea wananchi katika masuala ya maendeleo " Wananchi waliwaamini wakawachangua hivyo epukeni na vikwazo vyovyote vya uoga " amesema.

Mkuu wa wilaya ya Tarime Edward Gowele amewapongeza waumini na wadau wa maendeleo kuchangia ujenzi wa kanisa huku akiahidi kushiriki katika masuala ya maendeleo ambapo pia amechangia Tsh. 500,000 huku Nyangwine akimuunga Tsh. 500,000.

       Mkuu wa wilaya ya Tarime Edward Gowele akipokea sakramenti.

" Mahali ambapo hakuna maendeleo hakuna amani, jambo tunalolifanya hapa ni jambo la maendeleo. Nami ninawaahidi kwenye suala la maendeleo ndani ya wilaya mnialike pasipo hofu nitakuja.

" Nikushukuru baba Paroko kwa kupata wazo la kunialika nami nikasema kwasababu ni suala la maendeleo la kijamii lazima nishiriki. Nimeona namna wanatarime walivyo na kiu ya maendeleo" amesema Edward.

Mkuu huyo wa wilaya amempongeza Nyambari Nyangwine kwa kufika na kuwa mgeni rasmi na kuchangia fedha katika suala la kijamii huku akiwashukuru waumini na wadau wa maendeleo kufika kuchangia ujenzi wa kanisa.

      Baadhi ya waumini wakiwa katika ibada ya misa takatifu.

Askofu wa Jimbo la Katoriki Musoma, Michael Msongazila amewashukuru wote waliotoa michango yao kufanikisha ujenzi na kwamba kanisa hilo litabeba idadi ya watu zaidi ya 1000 huku akiwaombea baraka kwa mwenyezi Mungu wote walioguswa kuchangia ujenzi.

Askofu huyo amewataka watu kutowachukia na kuwaonea wivu wanaotenda mema kwani yeyote anayetenda mema hata kama si muumini mkatoriki, mkristo tendo hilo lina baraka mbele za Mungu.

          Askofu wa Jimbo la Katoriki Musoma, Michael Msongazila akizungumza na waumini na wadau wa maendeleo wakati wa harambee ya kuchangia ujenzi wa Kanisa.

" Mungu anasema mtu ambaye hapingani naye yupo pamoja nae. Tunapoona watu wakitenda mema ni lazima tufurahi tusiwachukie haijarishi anatoka wapi.

" Haijarishi ana imani gani, anatoka kabila gani, ni wa chama gani, ilimradi kwetu anafanya mambo yanayoendana na nia njema ya bwana wetu kristo " amesema Askofu Michael.














No comments