WANANCHI TARIME VIJIJINI WATAKIWA KUZINGATIA LISHE BORA
>>Afisa Lishe, Afisa Ustawi waeleza umuhimu wa lishe bora
Na Dinna Maningo, Tarime
LISHE bora husaidia mwili kukaa vyema, kujenga mwili lakini pia huimarisha Kinga ya mwili ili iweze kupigana na magonjwa.
Ili lishe iwe bora ni muhimu iwe na mchanganyiko wa vyakula mbalimbali kama vile protini, wanga, fati, mbogamboga, madini, matunda na maji kwa wingi.
Kwa kutambua umuhimu wa lishe bora Halmashauri ya wilaya ya Tarime kupitia idara ya afya na idara ya ustawi wa jamii imetoa elimu ya lishe bora kwa wananchi na Wanafunzi wakati wa maadhimisho ya siku ya lishe Kitaifa yaliyofanyika Oktoba, 30, 2024, ambapo halmashauri hiyo imeadhimisha katika viwanja vya Nyamwaga.
Wataalam wa afya wakitoa elimu ya lishe kwa wananchi na Wanafunzi wakati wa maadhimisho siku ya lishe yaliyofanyika viwanja vya Nyamwaga
Afisa Lishe halmashauri ya wilaya ya Tarime, Vero Raphael amesema kuwa lishe ni muhimu kwa watu wazima na watoto na kwamba jamii bado ina mwitikio mdogo katika masuala ya lishe.
" Malengo mahususi ya maadhimisho haya ilikuwa ni kutoa elimu ya lishe, kufanya upimaji wa hali ya lishe ili kumjua mtu ana hali gani ya lishe, kama ana uzito pungufu, uzito uliozidi au ana hali ya kawaida ya lishe.
" Tumewapa wanafunzi dawa za minyoo, tumewaelekeza wananchi jinsi ya kuandaa uji wa lishe kwa ajili ya watoto. Tumepima magonjwa ya presha, sukari yanayotokana na ulaji duni, tumetoa ushauri jinsi gani watu wajue kula lishe bora , mtindo gani wa maisha ni mzuri kwao ambao utawaweka katika mazingira mazuri ya kiafya " amesema Vero.
Ameongeza kuwa lishe ni muhimu kwa ukuaji wa mtoto " Ni muhimu kuanzia suala la ukuaji wa mtoto kuanzia ubongo, wanafunzi kufanya vizuri katika masomo yao.
"Kauli mbiu ni ' Mchongo ni afya yako zingatia unachokula' . Bado tuna changamoto kidogo jamii kuwa na mwitikio mdogo katika masuala ya lishe, lakini tunajitahidi kutoa elimu kuhakikisha jamii inaendelea kujitahidi kuzingatia Lishe bora " amesema.
Amewasisitiza wazazi kuhakikisha watoto wanapata chakula wawapo shuleni kwani mtoto asipopata chakula umwathiri katika masomo yake.
" Kuna utapiamlo wa muda mrefu na utapiamlo wa muda mfupi . Utapiamlo wa muda mfupi ni ule ambao mwanafunzi au mtu anaweza kukaa kwa muda mfupi bila kupata chakula kwa wakati ambapo inaweza kumwathiri.
" Mfano mwanafunzi asipopata chakula itamwathiri kwa upande wa usomaji ambapo angepata chakula angekuwa na uwezo mzuri wa kujisomea. Nawasisitiza wazazi wakubaliane na sisi tunaposisitiza suala la chakula shuleni ni la muhimu sana kwa watoto" amesema Vero.
Afisa Ustawi wa Jamii halmashauri ya wilaya ya Tarime, Siwema Silvester amewahimiza wananchi wakiwemo wazazi kuhakikisha wanawapa watoto vyakula vyenye virutubisho lakini pia jamii izingatie ulaji bora kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Jamii.
Afisa Ustawi wa Jamii halmashauri ya wilaya ya Tarime, Siwema Silvester
"Sisi kama Ustawi wa Jamii wenye jukumu la kusimamia ulinzi na ustawi wa mtoto. Lishe ni haki ya kila mtu hususani watoto ambayo ni haki ya kuishi.
" Ili mtoto aishi anahitaji lishe bora, kwahiyo na sisi kama maaafisa ustawi wa jamii tuna jukumu la kuhamasisha suala la lishe kwa watoto na wananchi wote kwa ujumla kuanzia ngazi ya familia" amesema Siwema.
Mkazi wa Nyamwaga Msiba Marwa amewasisitiza wazazi kuchangia chakula kwa wanafunzi wawapo shuleni kwakuwa husaidia watoto kupata nguvu na kuweza kujisomea.
" Mtoto anapokuwa nyumbani anapata chakula lakini anapokuwa shuleni wazazi hawachangii chakula watoto wanashinda njaa. Niwaombe wazazi watoe michango kuhakikisha watoto wanapata chakula " amesema Msiba.
Mwanafunzi wa shule ya msingi Maika, Enock Bernard ameshukuru maadhimisho hayo ya elimu ya lishe bora ambapo wameweza kupata uji wenye virutubisho huku akiwaomba wazazi kuhakikisha wanawapa watoto chakula bora.
Post a Comment