MATUKIO 533 YA UKATILI WA KIJINSIA YARIPOTIWA POLISI KAGERA
>> Matukio ya ubakaji yanaongoza kwa idadi ya 230
Alodia Dominick, Bukoba
MKOA wa Kagera ni miongoni mwa mikoa yenye matukio mengi ya ukatiri wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto huku takwimu zikionyesha kuwa kuanzia Januari hadi Septemba mwaka huu vitendo vya ukatili vipatavyo 533 vimeripotiwa katika vituo mbalimbali vya jeshi la polisi.
Vitendo vya ubakaji vipatavyo 230 vimeripotiwa kwa kipindi cha miezi tisa mkoani Kagera huku jumla ya vitendo vya ukatiri 533 vikiripotiwa mkoani humo.
Wanafunzi wakiwa kwenye maandamano wakipita mitaa mbalimbali ya manispaa ya Bukoba wakiwa na mabango ya kupinga ukatiri wa kijinsia
Takwimu hizo zimetolewa Oktoba 12, 2024 katika uzinduzi wa kampeini ya tuwaambie kabla hawajaharibikiwa, kampeini inayoendeshwa na jeshi la polisi kupitia kitengo cha jinsia na watoto mkoa wa Kagera.
Akizindua kampeini hiyo mgeni rasmi mkuu wa wilaya ya Bukoba, Erasto Sima kwa niaba ya mkuu wa mkoa huo amesema kuwa takwimu hiyo ya vitendo 533 vya ukatiri walifanyiwa wanawake, wanaume na watoto.
Aliyevaa suti ni mkuu wa wilaya ya Bukoba Erasto Sima akipokea maandamano katika kampeni ya tuwalee kabla hawaharibikiwa katika ukumbi wa shule ya sekondari Bakoba na wa kwanza kulia ni mkuu wa polisi wilaya ya Bukoba afande Mwita Marwa
Erasto amesema kuwa, kesi 71 zilishunghulikiwa na hatua za kisheria kuchukuliwa ikiwemo kifungo cha maisha, kifungo cha miaka 30 na kifungo cha miaka 10.
“Makosa yaliyoripotiwa katika kipindi tajwa ni ubakaji, kuwaozesha wanafunzi, kujaribu kubaka, kutelekeza familia, kutelekeza watoto na shambulio la aibu kwa watu mbalimbali” amesema Erasto.
Aidha miongoni mwa matukio hayo ambayo yamekuwa yakijirudia ni ya ubakaji ambayo idadi yake yalikuwa 230, kuwapa mimba wanafunzi yariripotiwa matukio 61, matukio ya urawiti matukio 13.
Wanafunzi wakiwa kwenye maandamano wakipita mitaa mbalimbali ya manispaa ya Bukoba wakiwa na mabango ya kupinga ukatiri wa kijinsia
DC Erasto ametoa wito kwa jamii mkoani Kagera kwenda na kampeini ya tuwalee kabla hawajaharibikiwa kwa kuwaelimisha vijana na watoto ili waweze kutimiza malengo yao.
Mkuu wa Dawati la jinsia mkoa wa Kagera askari Suzan Salvatory amesema kuwa, lengo la kampeini hiyo ni kuwaelimisha wanafunzi kuanzia shule za msingi hadi sekondari kutokana na mazingira wanakopita wakati wa kutoka nyumbani na kwenda shule na kutoka shule kwenda nyumbani ili waweze kuepukana na visawishi vinavyoweza kusababisha wakumbwe na ukatiri.
Polisi na Wanafunzi wakiwa kwenye maandamano wakipita mitaa mbalimbali ya manispaa ya Bukoba wakiwa na mabango ya kupinga ukatiri wa kijinsia
Salvatory ameeleza kuwa, makosa ya kubaka yanaonekana kushika kasi mkoani humo kwani kati ya makosa ya ukatiri 533 miongoni mwa makossa hayo 230 ni ya ubakaji yakifuatiwa na makosa ya kuwapa mimba wanafunzi ambayo yalikuwa 61.
Anazitaja sababu sita zinazochangia kuendelea kwa maswala ya ukatiri ni pamoja na sayansi na teknorojia ambayo imeleta mabadiliko kwa vijana na watoto hivyo kusababisha mmomonyoko wa maadili, imani za kishirikina, jamii kutokuwa na uelewa wa kutosha juu ya maswala ya ukatiri wa kijinsia, matumizi ya vileo na vilevi, kuanguka kwa mifumo ya mila na desturi katika jamii na shinikizo rika.
Naye mkuu wa kitengo cha kutetea haki za binadamu na kusuruhisha migogoro kutoka kanisa la ELCT Alisi Ayoub amesema kitengo hicho kinafanya kazi katika wilaya sita za mkoa wa Kagera kinazo kazi tatu kinazozifanya katika jamii kwa kushirikiana na serikali.
Polisi na Wanafunzi wakiwa kwenye maandamano wakipita mitaa mbalimbali ya manispaa ya Bukoba wakiwa na mabango ya kupinga ukatiri wa kijinsia
Amesema kazi hizo ni kuelimisha jamii kuachana na vitendo vya ukatiri, kufundisha athari za ukatiri zinazochokoza unyanyasaji wa kijinsia vitendo vya ngono holela na mauaji yasiyotarajiwa.
Amesema kuwa kwa mwaka 2023 jumla ya migogoro 869 ilipokelewa katika ofisi yake kati ya hiyo migogoro 94 walifanyiwa watoto, migogoro 280 wanaume walifanyiwa ukatiri na wake zao na migogoro 495 iliwahusu wanawake juu ya ukatiri wa kingono, unyanyasaji wa kijinsia na kunyimwa haki.
Aidha akitaja takwimu hizo za ukatiri kwa mwaka 2024 kuanzia Januari hadi Septemba amesema kuwa, migogoro ambayo imeripotiwa kwa kipindi hicho iko 630.
Mwenyekiti wa huduma kwa vijana na watoto kutoka shirika la Kompashen manispaa ya Bukoba Mwl. Kikono Joseph linalofanya kazi kwa kushirikiana na makanisa ya kidini amewasihi vijana na watoto kuchukua hatua kabla uharibifu haujatokea kwani wanazo ndoto kubwa za kutimiza.
Amelishukuru jeshi la polisi kwa kuanziasha kampeni hiyo na kuwa itaamsha hisia za vijna na watoto kutambua haki zao ni zipi nini cha kufanya na kuacha ili watimize ndoto zao, na amewasihi vijana na watoto kuwa makini na viungo vyao vya mwili.
“Nimependa wimbo ambao umeimbwa na vijana kuwa, mwili wa mwanadamu una sehemu ambazo zinamuhusu mwenye nazo peke yake nyingine haziruhusiwi kuguswa, ukatiri mwingi unafanywa na watu wa karibu na sisi ambao wakikushika mkono huwezi ukashtuka lakini kwa asilimia kubwa hao ndiyo wanaonekana wanaweza kufanya ukatiri kwenye maisha ya kijana au mtoto” amesema Joseph.
Filipina Adamu ni mwalimu kutoka shule ya sekondari Omumwani katika manispaa ya Bukoba ametaja mambo yanayosababisha wanafunzi kuaribikiwa na kujikuta wakifanyiwa ukatiri kuwa ni ushawishi wanaofanyiwa.
“Mwanafunzi kitu kidogo tu anachoona kinampa furaha ni kitu kinachoweza kumwaribia maisha yake, mfano zawadi ya chipsi, lifti ya boda boda ni vitu vinavyoweza kuwaharibia wanafunzi maisha yao” amesema mwalimu Adamu
Amesema wao kama walimu wataendelea kuwaelimisha wanafunzi ili waweze kuepukana na vishawishi na wajue madhara yatokanayo na kupenda vizawadi vidogovidogo na baada ya kupata elimu hiyo tunatarajia watavuka salama na kuhitimu masomo yao.
Aulen Merichades mwanafunzi kutoka shule ya wasichana ya sekondari Omumwani kidato cha sita amewaomba wenzake wa kike kuacha tamaa na kuzijua hali za familia zao na kusoma kwa bidi ili waweze kutimiza malengo yao.
Mmoja wa wazazi Paulina Raulent kutoka manispaa ya Bukoba amesema kutokana na vitendo hivyo vya ubakaji amekuwa akikaa na watoto wake wa kike na kiume wadogo kwa wakubwa na kuwaeleza athari za ubakaji na kuwataka kuchukua tahadhari.
Post a Comment