WAANDISHI WA HABARI WAHIMIZWA KUHAMASISHA USHIRIKI WA WANAWAKE KATIKA UONGOZI
>>TGNP, REDIO JAMII yaeleza lengo la kutoa mafunzo kwa Waandishi wa Habari
Na Gustaphu Haule , Dar es Salaam
MTANDAO wa Jinsia Tanzania (TGNP)kwa kushirikiana na mtandao wa Radio Jamii Tanzania wamewapiga msasa Waandishi wa habari kuhusu kuhamasisha ushiriki wa Wanawake katika uongozi hasa katika kipindi cha kuelekea katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Mafunzo hayo ya siku tatu yameanza Oktoba 29 katika ofisi za TGNP zilizopo Jijini Dar es Salaam na kumalizika Oktoba 31 mwaka huu yakiwa chini ya wakufunzi wawili akiwemo Deogratius Temba na Vera Assenga.
Washiriki wa mafunzo ya uandishi wa habari zenye mrengo wa Kijinsia yanayotolewa mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) Jijini Dar es Salaam
Katika mafunzo hayo TGNP imewakutanisha waandishi wa habari zaidi ya 50 kutoka mkoa wa Mtwara, Lindi, Pwani na Dar es Salaam .
Akifungua mafunzo hayo afisa habari wa TGNP Monica John, amesema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuendelea kuhamasisha Wanawake kutumia fursa zilizopo hasa katika uchaguzi kugombea nafasi mbalimbali.
Afisa habari wa TGNP Monica John akitoa mafunzo kwa Waandishi wa habari juu kuandika habari za kuhamasisha ushiriki wa Wanawake katika uongozi.
Monica amesema kuwa mwaka huu Tanzania inatarajia kufanya uchaguzi wa Serikali za Mitaa na kwamba hiyo ni fursa kwao hivyo TGNP wanatumia nafasi hiyo kuwanoa wanahabari ili wakatumie kalamu zao katika kuwahamasisha Wanawake.
Amesema katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2019 Wanawake waliojitokeza kugombea katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni asilimia 2.1 jambo ambalo kwasasa lazima lipiganiwe ili Wanawake wajitokeze.
Waandishi wa habari kutoka mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani na Dar es Salaam wakiwa katika picha ya pamoja katika mafunzo ya TGNP kuhusu kuandika habari zenye mrengo wa Kijinsia.
"Mwaka huu kuna uchaguzi wa Serikali za Mitaa na tayari fomu zimeanza kutolewa kwahiyo ni wakati muafaka wa Waandishi wa habari kutumia nafasi zetu kwenda kuhamasisha Wanawake kujitokeza katika uchaguzi huo", amesema Monica.
Monica amesema TGNP inatambua umuhimu wa Vyombo vya habari hapa nchini ndio maana inaendelea kutoa mafunzo ya kuwanoa Waandishi wa habari lengo ni kuhakikisha Wanawake wanashiriki katika chaguzi mbalimbali.
Awali mkufunzi wa mafunzo hayo Vera Assenga,amesema kuwa anaamini waandishi wa habari wakifanyakazi zao vizuri kuna uwezekano wa kuwepo na mabadiliko makubwa ya wanawake kujitokeza.
Mkufunzi wa mafunzo ya TGNP Vera Assenga kuhusu kuandika habari zenye mrengo wa Kijinsia hususani katika kuhamasisha Wanawake kugombea katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa
Assenga amewaomba Waandishi hao kwenda kujitoa katika kipindi hiki cha kuelekea katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa ili kuhakikisha Wanawake wanaingia katika Vyombo vya maamuzi.
Baadhi ya Waandishi wa habari walioshiriki mafunzo hayo akiwemo Christopher Lilai na Grace Mwakalinga wameishukuru TGNP kwa kutoa mafunzo hayo huku wakiahidi kuyafanyiakazi kikamilifu.
Afisa habari wa TGNP Monica John akifungua mafunzo ya Waandishi wa habari kuhusu kuandika habari zenye mrengo wa Kijinsia yanatolewa na TGNP kuanzia leo Oktoba 29 katika ofisi za TGNP zilizopo Jijini Dar es Salaam.
Post a Comment