WAZIRI AWESO ARIDHISHWA NA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAENDELEO SIMIYU
Na Samwel Mwanga, Simiyu
WAZIRI wa Maji, Jumaa Aweso, ameridhishwa na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kisekta ya maendeleo katika mkoa wa Simiyu.
Ameyasema hayo kwa nyakati tofauti Oktoba 27 na 28, 2024 baada ya kutembelea na kukagua miradi hiyo kufuatia maagizo ya Rais Dkt. Samia Suluhu ya kumtaka kufika katika mkoa huo na kuona utekelezaji wa miradi mbalimbali ya serikali.
Waziri wa Maji,Jumaa Aweso akizungumza na wananchi wa Kata ya Dakama wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu.
Miradi aliyotembelea inahusisha sekta mbalimbali ya Maji, Elimu, Afya na Barabara, ambapo aliona miradi hiyo jinsi inavyoendelea katika kuhakikisha huduma muhimu zinawafikia wananchi.
Amesema ni sehemu ya juhudi za serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa lengo la kuboresha maisha ya wananchi wa Tanzania kwa kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za kijamii na miundombinu.
Akizungumza katika shule ya sekondari ya Dakama katika wilaya ya Maswa ambapo alizindua shule hiyo mpya iliyojengwa kwa gharama ya zaidi ya Tsh. Milioni 500 amesema kuwa serikali imeona umuhimu katika sekta ya elimu ndiyo maana kwa sasa inajenga shule nyingi mpya za msingi na sekondari sambamba na kuondoa ada kwa wanafunzi wanaosoma katika shule hizo za serikali.
Moja ya majengo ya madarasa katika shule ya sekondari Dakama wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu
“Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweka kipaumbele katika kuimarisha sekta ya elimu nchini kwa lengo la kuhakikisha elimu bora inawafikia watoto wote, bila kujali hali zao za kifedha,”
“Miongoni mwa hatua muhimu zilizochukuliwa na serikali ni kujenga shule za msingi na sekondari katika maeneo mbalimbali ya nchini ikiwemo hii shule ya sekondari Dakama ambayo imejengwa kwa zaidi ya Tsh. Milioni 500 bila hata mwananchi mmoja kuchangishwa fedha ,”amesema.
Amesema kuwa hatua ya kuondoa ada kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari imepunguza mzigo kwa wazazi na walezi na hivyo ikiwapatia fursa watoto wengi zaidi kujiunga na shule bila vikwazo vya kifedha.
Sehemu ya Wananchi wa Kata ya Dakama wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu wakimsikiliza Waziri wa Maji, Jumaa Aweso wakati wa uzinduzi wa shule ya sekondari Dakama
“Niwaeleze ndugu zangu ni kuwa mtoto wa mama lishe anaweza kuwa Rais, Mtoto wa mkulima anaweza kuwa Daktari Bingwa wa Magonjwa mbalimbali.
" Hivyo niwaachie usia wadogo zangu kuwa ninyi wilaya ya Maswa inawategemea,nimyi mkoa wa Simiyu unawategemea,ninyi Taifa la Tanzania linawategemea hivyo ni vizuri mkasoma,”amesema.
Amesema kuwa mpango wa serikali wa kujenga shule nyingi zaidi unalenga kuondoa msongamano wa wanafunzi, hasa katika maeneo ya vijijini na kupunguza umbali ambao watoto hulazimika kutembea ili kufika shuleni.
“Kupitia mikakati hii serikali inalenga kuwapatia watoto wote nafasi sawa ya elimu, ambayo ni muhimu katika kujenga taifa lenye nguvu kazi ya wasomi na wataalam watakaoshiriki katika kukuza uchumi wa nchi,”amesema.
Pia Waziri, Aweso ameelezea kuridhishwa kwake na ushirikiano mzuri uliopo kati ya serikali na Chama cha Mapinduzi (CCM) katika mkoa wa Simiyu katika kutekeleza shughuli za maendeleo.
Amesema kuwa ushirikiano huo ni muhimu katika kuhakikisha miradi ya maendeleo, hasa katika sekta zote inatekelezwa kwa ufanisi na kwa haraka ili kuwanufaisha wananchi wa mkoa huo.
“Nimefurahi sana kuona ushirikiano ulipo katia ya serikali na CCM katika moa huu wa Simiyu na kwa kufanya hivyo ndiyo maana miradi niliyoitembelea yote iko vizuri na viongozi wenu wa serikali na chama wanaijua nah ii inasaidia kuhakikisha changamoto za wananchi zinashughulikiwa ili wananchi waweze kupata huduma bora kwa wakati,”amesema.
Naye Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Kenani Kihongosi amesema kuwa serikali ya mkoa huo inasimamia fedha zote zinazoletwa kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo na kumhakikishia Waziri Aweso kuwa fedha zinatumika kama zilivyokusudiwa.
Kihongosi pia amewakumbusha wananchi wa mkoa huo kushiriki kwa wingi katika uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyikaNovemba 27, 2024 ili waweze kuchagua viongozi ambao watawaletea maendeleo katika maeneo yao kwa kushirikiana nja serikali,
“Ushiriki wenu ni muhimu kwa kuhakikisha mnachagua viongozi bora watakaosimamia maendeleo katika maeneo yenu huu ni wakati wa kushiriki katika mchakato wa kidemokrasia na kuchagua viongozi watakaowakilisha maslahi yenu katika ngazi ya mitaa kumbuka sauti yako ni muhimu katika kuleta mabadiliko,”amesema.
Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Simiyu,Shemsa Mohamed amesema kuwa katika kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2024 chama hicho kinatoa wito kwa wananchi kuwachagua wagombea wake kwa ajili ya kuendeleza jitihada za kuleta maendeleo nchini.

Amesema kuwa kwa mujibu wa chama hicho kimejikita katika kutekeleza ilani yake kwa vitendo kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo, kama vile uboreshaji wa miundombinu, huduma za afya, maji, na elimu.
“CCM inaamini kuwa wagombea wake wana uzoefu na uadilifu wa kutosha katika kuwatumikia wananchi na kutatua changamoto zinazowakabili hivyo CCM imejipanga kuhakikisha kuwa wagombea wake wanazingatia uwajibikaji, ushirikiano na uadilifu katika uongozi wao ili kuongeza kasi ya maendeleo,”
“Wananchi tunawahimiza kuwachagua viongozi wa CCM ambao wana nia ya dhati ya kuleta mabadiliko chanya na kuendeleza mipango iliyoanzishwa na serikali kwa manufaa ya jamii nzima na wagombea hao wanatoka katika Chama Cha Mapinduzi,”amesema.
Post a Comment