HEADER AD

HEADER AD

ZAIDI YA VIJANA 1000 KUSHIRIKI MAADHIMISHO WIKI YA VIJANA


Na Mwandishi Wetu, Dodoma

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete amesema zaidi ya Vijana 1000 wanatarajiwa kushiriki katika maadhimisho ya wiki ya Vijana Kitaifa itakayofanyika mkoani Mwanza.

Waziri Ridhiwani amesema maadhimisho yatazinduliwa Oktoba, 11,2024 na kwamba wiki hiyo huadhimishwa kila Mwaka Oktoba 8 hadi 14.

      Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete akizungumza na Waandishi wa habari.

Amesema lengo la maadhimisho hayo ni kuwakutanisha vijana kutoka Tanzania bara na Visiwa kumuenzi Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere, Kujadiliana, kuonesha vipaji, bunifu na kazi wanazozifanya.

Akizungumza  na waandishi wa habari 0ktoba, 9,2024 jijini Dodoma, Ridhiwani amesema Waziri Mkuu Kassim Majaliwa anatarajiwa kuzindua wiki hiyo katika viwanja vya  Furahisha jijini Mwanza.




Waziri Ridhiwani ametaja shughuli zitakazofanyika kwenye wiki hiyo kuwa ni pamoja na kuwapo na makongamano ya kuwajengea uelewa wa fursa za ujasiriamali, ubunifu wa kidijitali katika kujifunza na kujiajiri sambamba na elimu ya Sera mpya ya maendeleo ya vijana (2007), Toleo la Mwaka 2024.

Pia, amesema kutakuwa na maandamano ya amani ambayo vijana watabeba jumbe mbalimbali ambazo serikali itazifanyia kazi.

“Kutakuwa na maonesho ambayo hutoa fursa kwa vijana kuonesha bunifu zao na kwa wadau wa maendeleo ya vijana kutoa huduma, elimu na taarifa kwa jamii hususan zile zinazoendana na malengo ya Taasisi zao na zenye lengo la kuleta mabadiliko chanya na kuhamasisha ustawi na maendeleo ya vijana nchini,” amesema Ridhiwani.

No comments