HEADER AD

HEADER AD

ATUPWA JELA MAISHA KWA KUBAKA MTOTO WA MIAKA TISA

Na Daniel Limbe, Biharamulo 

MKAZI wa Biharamulo mjini mkoani Kagera,Chichi Bubelwa(19 ) amehukumiwa kutumikia kifungo cha maisha jela baada ya kupatikana na hatia ya kubaka mtoto(mwanafunzi) mwenye umri wa miaka 9 kinyume cha sheria za nchi.

Uamuzi huo umetolewa na mahakama ya wilaya ya Biharamulo baada ya kupitia ushahidi uliowasilishwa na pande zote mbili kabla ya kufikia hukumu hiyo.

      Jengo la mahakama ya wilaya  Biharamulo.

Kabla ya kusoma hukumu hiyo, mshitakiwa alipewa nafasi ya kujitetea ili apunguziwe adhabu kutokana na kupatikana na hatia hiyo ambapo aliiomba mahakama impunguzie ukubwa wa adhabu kwa sababu hakutenda kosa hilo na kwamba anayo familia inayomtegemea.

Licha ya kuomba huruma ya mahakama, Hakimu mkazi mwandamizi wa mahakama ya wilaya hiyo,Subira Mashambo, amesema kitendo cha kubaka mtoto chini ya miaka 10 adhabu yake ni kifungo cha maisha jela na siyo vinginevyo.

Aidha alisema hukumu hiyo imezingatia maelekezo ya kifungu cha  cha 130 (1) na (2) (e) cha sheria ya kanuni ya adhabu sura namba 16 iliyofanyiwa marejeo yake mwaka 2022.

Hata hivyo amesema mshitakiwa anayo haki ya kukata rufaa iwapo hakuridhika na adhabu iliyotolewa, kwa kuzingatia muda uliowekwa na sheria.

Awali mwendesha mashitaka kutoka Ofisi ya mashitaka ya wilaya hiyo,Wakili Edith Tuka,kwa kushirikiana na Suddy Lugano,wameieleza mahakama hiyo kuwa mshitakiwa huyo alitenda kosa hilo kwa nyakati tofauti kati ya Oktoba 24 hadi 29 ,2023 huku akijua wazi kufanya kitendo hicho na mtoto ni kinyume cha sheria za nchi.

Ili kuisaidia mahakama kufikia uamuzi wa haki, upande wa mashitaka uliwasilisha ushahidi wa vielelezo ikiwemo barua namba tatu ya matibabu inayotolewa na jeshi la polisi(PF3),mama mzazi pamoja na mwalimu wa mwanafunzi huyo.

Hata hivyo kabla ya mshitakiwa kupewa adhabu hiyo,mwendesha mashitaka amesema ofisi yake haina kumbukumbu ya makosa mengine ya nyuma,lakini akaiomba mahakama hiyo kuangalia sheria inasema nini kuhusiana na wakosaji wa makosa hayo ambayo yamekuwa yakitweza utu wa mtoto,kuathiri kisaikolojia na kimwili.

Baada ya hukumu hiyo,mshitakiwa amechukuliwa na jeshi la polisi ili kupelekwa kwenye gereza la wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera kuanza kutumikia adhabu yake.

                 

No comments