HEADER AD

HEADER AD

SHAIRI : NAJIVUNIA BOT

BENKI Kuu Tanzania,ninakupa zangu sifa,

Umeniongoza njia, umeziba wangu ufa,

Elimu kunijazia, Benki umenipa ofa,

Benki kuu Tanzania, ni nuru yetu ya fedha.

Jamani Mwambande Lwaga , shukrani zikufikie, 

Wakipuliza kipenga, Semina tuhudhurie,

Ukumbini tukatinga, mazuri tuyasikie,

Benki kuu Tanzania, ni nuru yetu ya fedha.

Lwaga we umejaliwa, umejawa tabasamu,

Wadogo hata wakubwa, wawaonesha nidhamu,

Waandishi tukajuzwa, mengi tukayafahamu,

Benki kuu Tanzania, ni nuru yetu ya fedha. 

Semina ya siku mbili, imesheheni mazuri,

Sitaweza kwenda mbali,nisipitwe na habari, 

Nimefurahi kwakweli, Benki kuu ni hodari,

Benki kuu Tanzania, ni nuru yetu ya fedha.

Na Mwaikambo Gloria, mkurugenzi Benki kuu,

Kanda Ziwa una nia, wala hauna makuu,

Waiongoza kwa nia, ninakupongeza mkuu,

Benki kuu Tanzania, ni nuru yetu ya fedha.

Uliwapokea vyema, waandishi wa            habari,

Matarajio  wasema, ili wapate habari,

Waifahamishe umma, kwenye                  Vyombo vya habari,

Benki kuu Tanzania, ni nuru yetu ya fedha.

Meneja Issa Pagali, mwanauchumi wa Benki,

Watufungua akili, muundo sera ya Benki,

Uliyajibu maswali, sheria fedha ya Benki,

Benki kuu Tanzania, ni nuru yetu ya fedha.

Anna Lyimo wa masoko,  ukasema ya muhimu,

Twapata busara zako, hatukupata ugumu,

Dhahabu ajenda yako, mengi tukayafahamu,

Benki kuu Tanzania, ni nuru yetu ya fedha.

Nawe Kitojo Omari , wasimamia sarafu,

Tukaipata fahari, kwa elimu ya sarafu,

Kutunza fedha vizuri, wataka uangalifu,

Benki kuu Tanzania, ni nuru yetu ya fedha.

Noves Moses we ni, msikivu mtenda haki,

Wasisitiza maoni, ya masuala ya Benki,

Umetutoa gizani, kukusahau sitaki,

Benki kuu Tanzania, ni nuru yetu ya fedha. 

Zainab Almasi, ni meneja mwendeshaji,

Umetumia nafasi, kulitimiza hitaji,

Katika yako nafasi, wewe ni mtekelezaji,

Benki kuu Tanzania, ni nuru yetu ya fedha. 

Hakika nimejifunza, mengi nisiyoyajua, 

Sauti nitaipaza, wananchi kuyajua,

Sitochoka kuwajuza, hata likichoma jua,

Benki kuu Tanzania, ni nuru yetu ya fedha.

Meneja Vicky wa Msina,wewe mpambanaji wetu,

Tulivyokumisi sana, pokea salamu zetu,

Umewakilishwa sana, nao viongozi wetu,

Benki kuu Tanzania, ni nuru yetu ya fedha. 

Oliver mechakarika, huduma kufwatilia,

Ni kazi bila kuchoka, ulivyotuhudumia,

Uzidishiwe baraka, mwanzo hadi kuishia,

Benki kuu Tanzania ni nuru yetu ya fedha. 

 Shairi hili limetungwa na Dinna Maningo +255765336198

No comments