BOT YAWAKUMBUSHA WANANCHI KUTUMIA FEDHA YA TANZANIA KWA MALIPO NCHINI
>>Ni baada ya kubaini baadhi ya bidhaa, huduma kufanyika kwa kutumia fedha za kigeni nchini
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imewakumbusha wananchi wakiwemo wafanyabiashara kutumia pesa za Tanzania katika kupanga bei na kufanya malipo ya bidhaa na huduma nchini ili kuendelea kuimarisha uchumi wa Taifa.
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) , Emmanuel TutubaKwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na BoT bado kuna baadhi ya watu wanaoendelea kutumia fedha za kigeni kuuza bidhaa na huduma hapa nchini.
Bidhaa na huduma hizo ambazo matumizi ya fedha za kigeni yameshamiri ni pamoja na kuuza na kupangisha nyumba, viwanja, ofisi, ada za shule, malipo ya ushauri na zinginezo.
Pesa ya Kigeni“Kupanga bei na kufanya malipo kwa fedha za kigeni nchini ni kinyume cha Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania ya mwaka 2006 kifungu cha 26,” imeeleza taarifa hiyo.
Faida zaa matumizi ya shilingi
Matumizi ya shilingi yanawezesha Benki Kuu kutekeleza sera ya fedha kwa ufanisi ili kuwezesha kuwepo utulivu wa bei za bidhaa na huduma nchini.
Matumizi ya shilingi yanapunguza mahitaji ya fedha za kigeni yasiyo ya lazima nchini, hivyo kuchangia kuimarisha thamani ya shilingi dhidi ya fedha za kigeni, pamoja na kuimarisha ustahimilivu wa sekta ya fedha na kuvutia uwekezaji.
Hivyo, wananchi wamehimizwa kutoa taarifa Benki Kuu ya Tanzania endapo watabaini uwepo wa bidhaa na huduma kufanyika kwa fedha za kigeni ili wahalifu waweze kuchukuliwa hatua kali za kisheria.
Aidha, wananchi wameombwa kutoa taarifa Benki Kuu kwa namba za simu 0262963182-7, barua pepe info@bot.go.tz au katika vyombo vya dola ili hatua stahiki zichukuliwe.
Post a Comment