HEADER AD

HEADER AD

DC MASWA AWAHIMIZA MADIWANI KUPAMBANA NA KIPINDUPINDU


Na  Samwel Mwanga, Maswa
 
MKUU wa wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, Aswege Kaminyoge amewahimiza madiwani wa wilaya hiyo kushirikiana na viongozi wengine katika kukabiliana na ugonjwa wa kipindupindu ambao mara nyingi hutokea kutokana na ukosefu wa maji safi na mazingira duni ya usafi.
 
Ametoa wito huo Novemba, 21 mwaka huu wakati akizungumza katika kikao cha Baraza la madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya hiyo.

      Mkuu wa wilaya ya Maswa,Aswege Kaminyoge akizungumza katika kikao cha baraza la madiwani.

Amesisitiza kuwa ni vizuri madiwani na viongozi wa jamii kushirikiana kwa karibu kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kuchemsha maji ya kunywa na matumizi ya vyoo.
 
Amesema kuwa ugonjwa huo kwa sasa umekuwa wa muda mrefu katika mkoa huo pamoja na wilaya hiyo tangu wakati wa kiangazi na katika kipindi hiki cha mvua zilizoanza kunyesha ni hatari zaidi hivyo ni vizuri elimu kutolewa kwa wananchi ili kupambana na ugonjwa huo ambao ni hatari kwa maisha ya watu.
 
“Wote tuliopo humu ni viongozi na tunawategemea hawa watu wanaoumwa ndiyo tunawaongoza na wasipokuwepo hatutaongoza hivyo ni jukumu letu kuhakikisha tunawakomboa wananchi wetu katika janga hili la ugonjwa wa kipindupindu" amesema.
 
“Tuhakikishe tunatoa elimu kwa wananchi wetu na kuhakikisha wanakunywa maji safi na salama na wanatumia vyoo kwa kuzingatia kanuni ambazo zinaelezwa na wataalam wa afya ,hakuna miujiza kukomesha kipindupindu hili ni jambo letu tukilisimamia na kutoa elimu kwa wananchi ugonjwa huu utakwisha,”amesema.
 
Hivyo , amewaomba Madiwani kuungana na viongozi watakaochaguliwa mara baada ya uchaguzi wa serikali za mitaa kuhamasisha na kutoa elimu juu ya kunywa maji safi,kutumia vyoo bora na usafi wa mazingira na kwa kutumia njia hizo wilaya hiyo itakuwa haina hata mgonjwa mmoja wa ugonjwa huo.

          Madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Maswa wakiwa kwenye kikao cha baraza la madiwani

“Hatua hizi ni muhimu kwa kuzuia mlipuko wa magonjwa huu wa kipindupindu na ushirikiano kati ya viongozi na wananchi utasaidia kuondosha ugonjwa huo na wilaya yetu ikawa haina hata mgonjwa mmoja wa kipindupindu,”amesema.
 
Naye Wittness Philipo ambaye ni diwani wa Viti maalum(CCM)amesema kuwa kunahitajika nguvu ya ziada kwa viongozi wa kisiasa ambao ndiyo wawakilishi wa wananchi kutoa elimu ya usafi wa mazingira ili kuhakikisha ya kuwa ugonjwa huo unatoweka katika wilaya hiyo na mkoa wa Simiyu kwa ujumla.

        Baadhi ya madiwani wa wilaya ya Maswa waliohudhuria kikao cha baraza la madiwani

“Sisi viongozi wa kisiasa ndiyo tuna watu huko katika jamii yetu, hivyo ni jambo la msingi kwa umoja wetu kila mmoja kwenye eneo lake akishirikiana na viongozi wengine wa kijamii na wataalam wetu wa afya tukahamasisha suala la usafi wa mazingira ili kuhakikisha ugonjwa huu unaondoka katika wilaya ya Maswa na mkoa wetu wa Simiyu,”amesema.
 
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Maswa, Maisha Mtipa amesema kuwa halmashauri hiyo kwa kuwatumia Wataalam wa Afya, Maafisa watendaji wa Vijiji na Maafisa watendaji wa Kata wanatoa elimu na kuwahamasisha wananchi katika wilaya yote juu ya matumizi sahihi ya vyoo hasa maeneo ya vijijini pamoja na matumizi ya kunywa maji safi na salama ili kuhakikisha wanapambana na ugonjwa huo.

       Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Maswa,Maisha Mtipa akizungumza katika kikao cha baraza la madiwani
 
“Hii kwa sasa imekuwa kama agenda yetu ya kupambana na ugonjwa wa kipindupindu, tunawatumia wataalam wetu wa afya pamoja na watendaji wetu wa vijiji na kata kutoa elimu na kuhamasisha juu ya matumizi ya vyoo na kuchemsha maji ya kunywa na sasa tunasisitiza kila nyumba iwe na choo na wale wanaokaidi tunawachukulia hatua za kisheria,”amesema.

          Baadhi ya watendaji wa Kata  katika Halmashauri ya  wilaya ya Maswa waliohudhuria kikao cha baraza la madiwani.


No comments