HEADER AD

HEADER AD

SHAIRI : MANGO

 


MANGO chetu Kiswahili, wenyewe tunakijua,

Kujifunza siyo ghali, yetu tunapotatua,

Wala usiende mbali, neno upate lijua,

Twasugua kisigino, jiwe linaitwa mango.


Miguu inachafuka, hilo sote tunajua,

Ili iweze safika, brashi unayojua,

Pazuri haijafika, jifunze nyayo sugua,

Twasugua kisigino, jiwe linaitwa mango.


Hili jiwe mviringo, gumu kama walijua,

Hujalitumia mango, wewe bado hujakua,

Vizuri weka mpango, uchafu kugagadua,

Twasugua kisigino, jiwe linaitwa mango.


Wapoteza pesa zako, mango bado hujajua,

Hata huo muda wako, saluni unazijua,

Wakati kwa jiwe lako, ungezidi kutanua,

Twasugua kisigino, jiwe linaitwa mango.


Vinang’aa visigino, jinsi amevisugua,

Tena ni visafi mno, sasa aotea jua,

Ndani ya dakika tano, uzuriwe utajua,

Twasugua kisigino, jiwe linaitwa mango.


Shairi Limetungwa na  Lwaga Mwambande (KiMPAB)

lwagha@gmail.com 0767223602

No comments