CHADEMA BUKOBA YAELEZA CHANGAMOTO ILIZOPITIA UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA
Na Alodia Dominick, Bukoba
MWENYEKITI wa Chama cha Democrasia na Maendeleo (CHADEMA) Manispaa ya Bukoba, Chifu Kalumuna amesema baada ya uchaguzi wa serikali za mitaa watapambana kushinikiza ipatikane katiba mpya.
Lengo la katiba mpya iwe na kipengele cha Tume huru ya uchaguzi ili mwaka kesho katika uchaguzi mkuu baadhi ya mifumo iweze kubadilika.
Kalumuna ameyasema hayo Novemba 27, 2024 wakati akizungumza na Waandishi wa habari, mara tu baada ya kumaliza kupiga kura katika kituo cha Kyaya kata ya Kahororo na kudai kuwa katika mchakato mzima wa uchaguzi wa serikali za mitaa kuanzia uteuzi wa wagombea wao kama wapinzani kila hatua waliyoipitia walipata matatizo.
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA manispaa ya Bukoba Chief Kalumuna akizungumza na waandishi wa habari
“Wakati wa kujiandikisha waliongeza watu, wakati wa kujiandikisha wameandika maiti, wakati wa kugombea wameengua majina yetu wakati wa kwenda kupiga kura mawakala wengine wanakatazwa kuingia kwenye vituo na bado tuna hatari kwenye kutangaza matokeo” amesema Kalumuna.
Amesema lazima wawe na watu wanaosimamia uchaguzi nje ya mifumo ya serikali na kuwa Tawala za mikoa na serikali za mitaa (TAMISEMI) hawapaswi kusimamia uchaguzikwa sababu wao ni Wizara.
" Waziri ni mwana CCM kateuliwa kutoka kwenye chama chake anamsaidia mwenyekiti wa chama ambaye ni Rais hata mkurugenzi anaposimamia kwa kuwatumia watendaji wake bado wako chini ya serikali na wanatimiza malengo ya CCM" amesema Chifu .
Ameeleza kuwa wangependa kuwa na tume huru ambayo mifumo yake upatikanaji wa wasimamizi wa uchaguzi wawe ni watu ambao wamepatikana wakiwa huru wasiwe na upande wowote chama cha siasa.
Wananchi wakiwa wamejipanga mstari wakipiga kura katika kituo cha shule ya sekondari Samia kata ya Kashai manispaa ya Bukoba
Amesema baada ya uchaguzi wa serikali za mitaa CHADEMA wanapaswa kusimama kuhakikisha yanatokea mabadiliko makubwa katika mifumo ya usimamizi wa uchaguzi ili uchaguzi usiwe na sekeseke nyingi wanazozipitia mfano lawama nyingi, watu kukata tamaa ya kupiga kura pamoja na wengine kukata tamaa ya kugombea.
“Sisi kama mageuzi ambao tunagombea tunawapeleka watu katika mstari wanakata majina yao, maana yake hata mwaka kesho tukapokwenda katika uchaguzi mkuu kuna mtu utamwambia agombee udiwani na anafaa atasema hapana anapoteza muda vivyo hivyo na nafasi ya ubunge kwa sababu ya mifumo iliyopo katika nchi hii” amesema Kalumuna.
Aidha kiongozi huyo amepigia kura katika kituo cha Kyaya kata ya Kahororo na kubaini baadhi ya dosari ikiwemo mpangilio wa majina kiherufi kwani kutokana na majina yalivyokuwa mengi baadhi ya wapiga kura walikuwa wanapata shida kupata majina yao kwenye ubao yalipotundikwa na wengine kukata tamaa na kuondoka bila kupiga kura.
“Katika uchaguzi wa serikali za mitaa hata na chaguzi nyingine zilizopita wanafunzi wa kidato cha nne, tano na sita wamekuwa ni wadau wakubwa wa uchaguzi ambao wanatajwa na kanuni kuwa wao ni wakazi kwa mujibu wa sheria.
" Lakini tumeshuhudia kelele sana hao wanafunzi wamefungiwa kwenye maeneo yao bila kuhudhuria mikutano ya vyama vya upinzani badala yake wamekuwa wakihudhuria mikutano ya CCM” amesema Kalumuna.
Anasema wanafunzi ni wadau wa siasa hivyo vyama vyote vya siasa vinapaswa kupewa nafasi sawa kwenda mashuleni kunadi sera, na kama haiwezekani kisiende chama tawala peke yake.
Wananchi wakiwa wamejipanga mstari wakipiga kura katika kituo cha shule ya sekondari Samia kata ya Kashai manispaa ya Bukoba
Amesema kwa Bukoba manispaa kuna vituo 160 vya kupigia kura na mitaa 66 vituo vyote hivyo walikuwa wameweka wagombea na mawakala. Chadema walikuwa wameweka wagombea 63 wa wenyeviti wa serikali za mitaa na wajumbe wao.
Amesema kwenye uteuzi walikuwa hawajateuliwa kwenye mitaa sita walipokwenda kwenye hatua ya mapingamizi yalikuwa ni 23 kwa wenyeviti wa serikali za mitaa.
Pia kati ya hao katika rufaa walirudishwa watu watano hivyo wagombea wao wakabaki katika mitaa 44 na wagombea uenyekiti katika mitaa mitano wakajiengua hivyo wakabaki wagombea katika mitaa 39.
Aidha amesema pale ambapo hakuna mgombea wao wamepiga kura ya hapana na chama chao kimefanya mikutano na kuhamasisha kupiga kura ya hapana.
" Kanuni ya 40 inasema kura ya hapana ikiwa nyingi ule uchaguzi unafutwa na badala yake uchaguzi unatangazwa upya wiki mbili baada ya uchaguzi.
Aidha amewaelekeza wanachama wote katika mitaa kuhakikisha wanatumia nguvu ya watu kuwalazimisha mawakala wao wabaki kwenye vituo ili waweze kushuhudia kura ya ndiyo na hapana ili baada ya uchaguzi kuwa umefutwa chama chao kirejeshe wenyeviti waliokuwa wamependekezwa kwenye maeneo hayo.
Wakati huohuo, Mkuu wa mkoa wa Kagera, Fatma Mwasa aliwataka wananchi kuzingatia taratibu wakipiga kura warudi majumbani wapumzike wasubiri matokeo asiwepo yeyote wa kufanya vurugu.
“Mkoa wa Kagera hali ya ulinzi na usalama ni shwari pamoja na mvua iliyokuwa ikiendelea kunyesha wananchi walijitokeza kwa wingi kwenye vituo kwa ajili ya kupiga kura”.
Irine Mwananun’gu mkazi wa mtaa wa Pwani Irine Mwananun'gu ameeleza kuwa, utaratibu wa upigaji kura ni mzuri na katika kituo alichopigia kura watu walikuwa wanafika wanapiga kura na kurundi nyumbani.
Hata hivyo, Mkoa wa Kagera unavyo vituo vya kupiga kura vipatavyo 4,012, Bukoba mjini vipo vituo 160, Bukoba vijijini 526, Muleba vituo 801, Misenyi vituo 360, Kyerwa vituo 675, Karagwe vituo 631, Ngara vituo 436 na Biharamlo 423 ,idadi ya wapiga kura ni zaidi ya Milioni moja.
Post a Comment