RC SHINYANGA AWATAKA WANANCHI KUSUBIRI MATOKEO YA UCHAGUZI WAKIWA MAJUMBANI
Na Suzy Butondo, Shinyanga
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha amewasihi wananchi mkoani Shinyanga wanapomaliza kupiga kura warudi majumbani mwao kwa ajili ya kusubiri matokeo yatangazwe.
Mbunge wa jimbo la Shinyanga Patrobas Katambi amesema uchaguzi huo umefanyika kwa amani na utulivu na hii ni tafsiri ya kidemokrasia.
Hayo wameyasema Novemba, 27, 2024 baada ya kushiriki kupiga kura katika vituo vya kupigia kura ambapo mkuu wa mkoa amepiga katika kituo cha wazi cha kata ya Lubaga na mbunge kituo cha mbuyuni kata ya Old Shinyanga manispaa ya Shinyanga.
Wote kwa pamoja wamewasihi wananchi wajitokeze kupiga kura mapema na warudi nyumbani kusubili matokeo yatangazwe kwa utulivu.
"Niwaombe sana wananchi wangu mchague viongozi sahihi ambao watawatumikia katika kipindi cha miaka mitano watakaosimamia miradi mbalimbali ya maendeleo na kuwasimamia wananchi"amesema mkuu wa mkoa.
Macha amesema hadi sasa uchaguzi huo unaendelea vizuri kwa amani na utulivu hakuna vurugu zozote, na kwamba kazi yao kama viongozi wa serikali ni kuhakikisha amani inaendelea kutawala kwenye uchaguzi huo.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Annamringi Macha akipiga kura katika kituo cha Wazi kata ya Lubaga manispaa ya Shinyanga.
Wakati huo huo Mbunge wa jimbo la Shinyanga ambaye pia ni Naibu waziri ofisi ya Wazri mkuu kazi vijana ajira na wenye ulemavu Patrobas Katambi akizungumza baada ya kupiga kura amesema uchaguzi huo ni uchaguzi wa kikatiba na ni wa kisheria.
Katambi amesema uchaguzi huo umefanyika kwa amani na utulivu, kwani imeonyesha ni wa uhuru na haki, na kwa utulivu huo inaonyesha ni tafsiri kubwa ya hatua kubwa ya kidemokrasia na ukomavu katika nchi ya Tanzania na kuonyesha uongozi bora unaofata misingi na utawala bora wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa sababu yeye ndiye msimamizi wa serikali ya Tanzania.
Mbunge wa jimbo la Shinyanga mjini Patrobas Katambi akizungumza baada ya kupiga kura katika kituo cha Mbuyuni Kata ya Old Shinyanga
"Kwa kweli zoezi linaenda vizuri kwani wananchi wanaendelea kupiga kura kwa amani kabisa, lakini pia taasisi za uchaguzi zipo huru kikatiba na sheria, na kila mwananchi ana uhuru wa kumchagua kiongozi anaemtaka na ni ishara ya wananchi ya ushirikishwaji na utawala bora.
" Hivyo tunaamini wataenda kuchagua kiongozi wanaemtaka, na mimi nimefika hapa kwa ajili yakupiga kura, tunachagua kiobgozi ambaye atakuwa karibu na wananchi atasikiliza kero mvalimbali za kijamii"amesema Katambi.
Nae mjumbe wa kamati ya siasa wilaya ya Shinyanga, James Jumbe ambaye alipiga kura katika mtaa wa Majengo amewasihi wananchi wote wa manispaa ya Shinyanga wajitokeze kwa wingi kwa ajili ya kupiga kura za serikali za mitaa ili kuchaguwa viongozi bora watakao simamia miradi mbalimbali ya maendeleo katika mitaa yao.
Mjumbe wa kamati ya Siasa CCM wilaya ya Shinyanga akizungumza baada ya kupiga kura Mtaa wa majengo manispaa ya Shinyanga
"Uchaguzi huu ni wa muhimu sana hivyo niwaombe wananchi wote mjitokeze kwa wingi ili kuhakikisha mnanapiga kura za kuwachagua wenyeviti na wajumbe zoezi hili ni la muda mfupi tu wakijitokeza watampigia kiongozi wanaomtaka watapata haki yao.
"Pia wasiogope kuna usalama mkubwa katika eneo hili na watu wachukulie kwa umuhimu mkubwa ili waweze kuchagua kiongozi atakayetatua changamoto mbalimbali za mitaa"amesema Jumbe
Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA Kanda ya Serengeti Jackson Mnyawami, amesema zoezi la uchaguzi katika manispaa ya Shinyanga linakwenda vizuri isipokuwa kuna dosari ndogo ndogo ambazo zimejitokeza ikiwamo baadhi ya vituo kutobandikwa orodha ya majina ya wapiga kura.
Kwa upande wake msimamizi wa uchaguzi katika Manispaa ya Shinyanga Alexius Kagunze, amesema maandalizi ya uchaguzi huo wa serikali za mitaa yamefanyika vizuri ambapo kuna vituo 285 katika manispaa ya Shinyanga.
Akizungumzia baadhi ya vituo kutobandikwa majina ya wapiga kura, amesema kwenye vituo vya wazi ambavyo vipo 149 majina hayo hayajabandikwa kutokana na kuhofia mvua, na kwamba daftari lenye orodha ya majina lipo kwa wasimamizi wa uchaguzi hapo hapo kituoni, ambapo kila mtu atahakikiwa jina lake na kushiriki kupiga kura.
Post a Comment