SOKOMBI AWAPONGEZA WANANCHI KWA KUPIGA KURA NA KUIPA CCM USHINDI
Na Jovina Massano, Musoma
MWANACHAMA wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ambaye pia ni mfanyabiashara, Joyce Sokombi amewapongeza wananchi wa mtaa wa Kwangwa B, Kata ya Kwangwa, Manispaa ya Musoma, mkoani Mara kuwachagua viongozi wanaotokana na CCM.
Akizungumzia na DIMA ONLINE Novemba, 28, 2024 amesema kwamba wanachama wa CCM ni wawajibikaji na waadilifu hivyo wamefanya jambo jema kumchagua Maximilian Kunju .

"CCM ina Ilani safi ambayo viongozi wake wamekuwa wakiisimamia na kuitekeleza kwa manufaa ya wananchi wake, mfano hai ni maendeleo katika Elimu, Afya, miundombinu ya barabara huduma za maji ikiwemo umeme hizi ni huduma muhimu kwa kila mwananchi.
" Hivi sasa tunashuhudia miradi mikubwa ikiendelea, hii inatokana na uongozi safi wa mwenyekiti wa chama cha mapinduzi Taifa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan na chama hicho kwa ngazi zote kuwa na uongozi uliotukuka kwa ufuatiliaji wa karibu kuhakikisha wananchi wananufaika katika kila nyanja" amesema.
Amesema sambamba na maendeleo hayo CCM inaendelea kudumisha utulivu na amani kwa wananchi wote na kuhakikisha usalama kwa taifa.
Kwa upande wake mshindi nafasi ya Mwenyekiti wa mtaa Kwangwa B' Maxmilian Kunju aliyekuwa mjumbe wa serikali ya mtaa ameshinda kwa kupata kura 715 huku mpinzani wake kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo akipata kura 527 amewahaidi ushirikiano wananchi wote wa mtaa huo.
"Nawaahidi ushirikiano wananchi wote wa mtaa huu. Awali eneo hili lilikuwa na changamoto ya ukosefu wa maji safi na salama lakini tulivyoingia madarakani mwaka 2019 tuliamua kupunguza bugudha, akina mama walikuwa wakienda kuchota maji kwenye visima hivi sasa wananchi wanapata maji safi na salama "amesema Kunju.
Mbali na changamoto hiyo baadhi ya miundombinu ya barabara ilikuwa ni njia za ng'ombe, na mashamba lakini kwa sasa uongozi wa CCM mkoa umefungua barabara hizo pamoja na kuweza kupata umeme wa REA na kuwaondoa gizani wakazi wa mtaa huo.
Post a Comment