CHADEMA KUWABURUZA MAHAKAMANI MAAFISA UCHAGUZI WASAIDIZI
>>Wadaiwa kughushi fomu za wagombea
Na Samwel Mwanga, Maswa
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA)Kanda ya Serengeti kimesema kuwa kitachukua hatua ya kuwafikisha mahakamani baadhi ya maafisa wasaidizi wa uchaguzi katika wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu kwa madai ya kughushi fomu za wagombea wao katika uchaguzi wa serikali za mitaa.
Maafisa hao wanadaiwa kutumia fomu hizo kughushi ili kuwaengua wagombea wa CHADEMA kwa madai kwamba hawana sifa za kugombea.
Hayo yameelezwa Novemba 13 mwaka huu na ofisa uchaguzi wa CHADEMA Kanda ya Serengeti, Askofu Obeid Jilala katika ofisi ya mkuu wa wilaya ya Maswa wakati wakifuatilia rufaa za wagombea wao walioenguliwa kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi wa serikali za mitaa.
Baadhi ya wagombea wa CHADEMA wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu ambao majina yao yalienguliwa na Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi wakiwa wanasubiri majibu ya rufaa zao katika Ofisi ya Mkuu wa wilaya hiyo.
Amesema kuwa hatua hiyo inalenga kudai haki kwa wagombea wa CHADEMA ambao waliondolewa kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi kwa njia wanazodai ni za udanganyifu uliokuwa ukifanywa kwenye fomu za wagombea wao na wasimamizi hao.
“Baadhi ya wagombea wetu walioteuliwa kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi wa serikali za mitaa katika wilaya ya Maswa wamekuwa wakipigiwa simu na Wasimamizi wasaidizi wa Uchaguzi katika maeneo yao, wakieleza wafuate fomu zao za kujiondoa wakati hawajijaza na fomu hizo na wala hawajajiondoa."
"Na hata ukiangalia saini zilizowekwa si za wagombea wetu na fomu zote zimewekewa alama ya dole gumba kwenye sehemu ya saini ya mgombea, huko ni kughushi hivyo kwa sasa tutakutana na kuona jinsi jinai hiyo ilivyofanyika na kuwafikisha mahakamani wote waliohusika,” amesema Jilala.
Vicent Maduka ambaye ni kiongozi wa Chadema Jimbo la Maswa Magharibi anasema kuwa kitendo cha baadhi ya Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi ngazi ya Kata ndiyo wamekuwa wakiwapigia simu wagombea wao walioteuliwa katika jimbo hilo kuwa wafike katika ofisi zao ili wachukue barua zao za kujiondoa huku akisisitiza ni vizuri seriikali ikaanza kuchukua hatua kutokana makosa hayo.
Baadhi ya wagombea wa CHADEMA wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu ambao majina yao yalienguliwa na Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi wakiwa wanasubiri majibu ya rufaa zao katika Ofisi ya Mkuu wa wilaya hiyo.
“Nimeshangazwa kupata taarifa kutoka kwa wagombea wetu walioteuliwa katika nafasi mbalimbali kugombea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa wamekuwa wanapigiwa simu na hawa Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi ngazi ya Kata.
"Wasimamizi hao ambao ni Maafisa watendaji wa Kata, kuwa wafike wachukue barua zao za kujitoa huo ni uhuni na wanataka kuiingiza nchini katika machafuko ni vizuri kabla hali haijachafuka serikali iwachukulie hatua,”amesema.
Rubein Jilala ni Mwenyekiti wa Chadema jimbo la Maswa Mashariki amesema kuwa kutokana na hujuma wanazofanyiwa na Wasimamizi hao ni vizuri serikali ikawaondoa katika kusimamia uchaguzi huo wa serikali za mitaa.
Amesema tayari wameshaonyesha kuwa hawezi kutenda haki kwa wagombea wa vyama vya upinzani isipokuwa kwa chama kilichoko madarakani Chama Cha Mapinduzi(CCM).
Amesema kuwa hata hizo kamati za rufaa zimejaza makada wa CCM hivyo kwa vyama vya upinzani kutegemea kupatiwa haki haki ni jambo ambalo ni gumu kutokana na kesi ya nyani ukaipeleka kwa tumbili huwezi kupata ushindi.
“Pamoja na vikwazo vyote hivi vya kuminya demokrasia katika nchi yetu hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa sisi Chadema tutapambana kwa njia zozote zikiwemo za kisheria kuhakikisha wagombea wetu wanaopaswa kuwa na nafasi ya kugombea wanapewa haki yao bila kuzuiwa isivyo halali,”amesema.
Amesema kuwa huo ni mwendelezo wa jitihada za chama hicho kupinga kile wanachodai kuwa ni ukiukwaji wa sheria na kanuni za uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajia kufanyika Novemba 27 mwaka huu.
Mwenyekiti wa kamati ya Rufaa wilaya ya Maswa, Athuman Kalaghe ambaye ni Katibu Tawala wa Wilaya hiyo amesema kuwa wanaendelea kusikiliza rufaa na serikali imeongeza muda wa kukata rufaa hadi Novemba 15 mwaka huu.
Amesema kuwataka wagombea wote walioenguliwa kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi wa serikali za mitaa walete malalamiko yao kwa njia rasmi na siyo kulalamikia pembeni.
“Kamati ya rufaa ya wilaya ya Maswa inaendelea kusikiliza rufaa za wagombea walioenguliwa na hawakuridhika na serikali kwa kuona umuhimu wa jambo hili umeongeza muda wa kusikiliza rufaa hadi Novemba 15 mwaka huu
" Hivyo nawaomba wote walioleta rufaa zao haki itatendeka wawe na imani kwani wapo hapo kwa ajili ya kutenda haki na siyo kumuonea mtu na kuwataka Chadema kuwa na imani na kamati hiyo,”amesema.
Ofisa Uchaguzi wa Chadema,Kanda ya Serengeti,Askofu Obeid Jilala(mwenye kaunda suti rangi ya bluu)akizungumza na wagombea wa chadema waliokuwa wakisubiri majibu ya rufaa zao katika ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Maswa.
Post a Comment