IRASANILO GOLD MINE WASEMA WANA MASHAKA NA VETTING
>>Ni baada ya ofisi ya DC Butiama kurejesha majina ya wagombea wenye tuhuma, walio safi majina yao yamekatwa
>> Wana Irasanilo wasema Vetting ipo kwa ajili ya madili ya watu
>>Uchaguzi wa viongozi Irasanilo wasimamishwa
Na Dinna Maningo, Musoma
MKUU wa mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi amesimamisha uchaguzi uliokuwa ufanyike hivi karibuni wa kikundi cha Irasanilo cha wachimbaji wadogo wa madini eneo la Buhemba, wilaya ya Butiama mkoa wa Mara ili aweze kupitia katiba ya kikundi.
Agizo hilo amelitoa kwenye kikao kilichowakutanisha wachimbaji wa kikundi hicho na mkuu wa mkoa wa Mara kwa lengo la kusikiliza kero za wanakikundi ili zitatuliwe, kikao kilichofanyika Novemba, 12, 2024 katika ukumbi wa uwekezaji ofisi ya mkuu huyo wa mkoa.
RC Evans ameagiza katiba hiyo ipitiwe upya ambapo wanakikundi na wataalam akiwemo mwanasheria wa serikali wataketi pamoja kuipitia upya kisha kutoa mapendekezo na kuipeleka kwa mkuu wa mkoa ambaye nae ataipitia kisha utafanyika uchaguzi wa viongozi, mchakato wote unatakiwa kufanyika ndani ya siku 21.
"Ngoja niisome hii Katiba baada ya hapo itapitiwa upya na wataalam kushirikiana na wanakikundi kisha itarekebishwa baada ya hapo tutafanya uchaguzi .
" Mmenikubalia kuwa mlezi wa kikundi kama kuna mtu anataka uongozi akidhani ataula basi hakuna wa kuula " amesema RC Mtambi .
Wanakikundi hao wamekosoa hatu ya kuchunguza wagombea wa kikundi cha Irasanilo (Vetting) inayofanywa na wilaya ya Butiama kwa maana ya mkuu wa wilaya na kamati yake ya ulinzi na usalama kwa kuwateua wagombea katika nafasi za uongozi wa kikundi hicho kwa kile kilichoelezwa kuwa baadhi ya wanakikundi walituma maombi nafasi ya kugombea uwenyekiti na katibu lakini majina yao yamekatwa.
Wamesema yamerejeshwa majina ya watu ambao bado wako kwenye uchunguzi wa tuhuma mbalimbali, wengine waliwahi kupata kashfa mbalimbali walipokuwa viongozi lakini majina yao yamerudi huku watu waliowasafi na wachapa kazi majina yao yakikatwa.
Reventura Antony " Hiki kitu kinaitwa Vetting kiliwekwa kwa maslahi ya watu . Tumejaza fomu kuomba uongozi inapita miezi miwili ndio vetingi inafanyika hii inasababisha watu waende huko kwa wanaofanya vetingi anafanya anavyojua jina lake linarudi au anafanya anavyojua jina lako linakatwa.
" Sasa mtu wa namna hiyo akipata uongozi lazima arejeshe fadhila kwasababu ameshakuwa mtumwa amependekezwa na Vetting, mimi sijui hiyo vetingi inatengenezwa wapi, RC tunaomba utowe tamko hapa kuhusu vetingi hata hawa viongozi waliotuletea tuwachague hatuwaekewi" .
" Kuna viongozi wa serikali wanakuja wanaomba pesa tukiuliza pesa ziko wapi tunaambiwa wamepewa viongozi wanasema kwamba ni mahusiano wasipofanya hivyo watanyang'anywa mgodi bila hata kutushirikisha wanakikundi.
" Kwenye Katiba yetu hakuna sehemu inayosema mtu akigombea uongozi afantiwe Vetting , hakuna kifungu kinachosema watu wafanyiwe vetingi ndio wawe viongozi. Mkuu wa mkoa bora uwe mlezi wetu ili upanyooshe pale wilayani" amesema.
Viongozi wa Chama cha wachimbaji wa madini wilaya ya Butiama na mkoa wa Mara (MAREMA) nao wanalaumiwa kwa kushirikiana na serikali ya wilaya kwa kukata majina ya watu kwani wao ndio wanawafahamu wanachama .
Mchimbaji mmoja amesema " Ikiwa kama wanalipwa na kikundi kupitia viongozi je watakuwa huru kukagua na kusema ukweli wakati wamewezeshwa fedha na viongozi wa kikundi ! .Istoshe hata Chama cha Marema sioni kazi yao maana hawa ni wasimamizi lakini hakisimamii matatizo ya watu " amesema.
Emmanuel Milinga ni miongoni mwa waliochukua fomu kugombea nafasi ya Mwenyekiti msaidizi naye jina lake limekatwa " Tumetuma majina yetu lakini yamekatwa.
" Lawama zangu ni kwa viongozi wa wachimbaji wadogo Marema hawa wanatufahamu tuko nao tunafanya nao kazi za uchimbaji. Kuna majina yalikuwa na tuhuma yamerudi, wanatuhuma za upotevu wa fedha nyingi lakini majina yao yamerudi.
" Joseph jina limerudi wakati yuko kwenye uchunguzi , majina yetu yamekatwa tumefanya makosa gani? mi siamini kama mkuu wa wilaya ndio kakata majina yetu maana yeye hatujui, Malema ndio wanatujua sasa watuambie walitukata wa nini?" alihoji .
Josephina Maricus amesema " Mwenyekiti anatuambia kuna watu wavivu ndio maana kazi haziendi . Swali langu je kama viongozi wanajua kuna watu wavivu basi hao wachapakazi majina yao yamerudi? " Amehoji .
Mchimbaji Joseph Golani amesema " Watu wana vyeo viwili wilaya na mkoani ukikata rufaa unamkuta yeye ndio yupo mkoani, jambo lako kushughulikiwa na kutendewa haki inakuwa shida.
" Kuna upotevu wa pesa sana, pesa zinaliwa na viongozi, kuna gari la Polisi ambalo lilikarabatiwa kwa Tsh. Milioni 80 kwa pesa za kikundi. Sisi ni chambo tu hakuna cha kikundi hapo ni kikundi cha matajiri wanatunyonya, kuna watu ni shida lakini wamegombea tena na majina yao yamerudi.
" Mimi ni mchimbaji wa miaka mingi, ni mwanachama nilipata ajali ni mlemavu wa miguu lakini wameshindwa kuninunulia hata baiskeli natembelea magongo , sina hata mkokoteni lakini kuna watu kupitia uongozi wamejenga majumba makubwa kwa sababu ni majizi ya pesa za kikundi " amesema .
" Hii Vetting ni madili ya watu , wagombea wameshapeleka mirungula kwa wafanya vetting naomba hata fomu za kugombea zichukuliwe upya hiyo vetting tuliiweka kwa ajili ya usalama lakini imekuwa mradi wa watu" amesema .
Mchimbaji mwingine amesema " Watu tunabebana hadi kwenye kasoro , makundi yanatuumiza sana mtu hana duara alafu anagombea uongozi wakati Chama hiki kilianzishwa kwa malengo ya wachimbaji" amesema .
David Bita Mwenyekiti wa Shiriko la wachimbaji wadogo mkoa wa Mara (MAREMA) amesema MAREMA haikushirikishwa kufanya ukaguzi wa majina ya wagombea.
" MAREMA wilaya na mkoa haikushirikishwa kwenye Vetting japo nimetukanwa sana kuwa mimi nimekata majina ya watu. MAREMA inatatua migogoro, sasa kama mgogoro umepita sehemu zingine umeanzia kwa viongozi wa serikali mimi MAREMA nitafanya nini" amesema David.
Mkuu wa wilaya ya Butiama, Moses Kaegele alipotafutwa kuzungumzia mgogoro wa wachimbaji alipokea simu na alipoulizwa kuhusu anachokifahamu juu ya malalamiko ya wachimbaji aliomba apigiwe simu baadae kisha alikata simu na alipotafutwa tena kuzungumzia sakata la wachimbaji simu yake iliita haikupokelewa.
Hata hivyo afisa Madini amekana kuhusika kuteua wagombea na kwamba yeye alipokea majina kutoka serikali ya wilayani kwamba ndio waliopendekeza kugombea.
Waliojaza fomu kugombea uenyekiti wa Irasanilo ambao majina yao yamerudi ni Shaban Kichinka na Paul Mgendi. Nafasi ya Makamu Mwenyekiti ni Dani Yuda , Jackson Nyamachowa na Samweli Mirwa.
Nafasi ya ukatibu ni Malima Bunyoga na Maria Petro na Joseph Magibo. Katibu msaidizi ni Tumsifu skuli na Joshua Eliakimu.
Post a Comment