HEADER AD

HEADER AD

TAKUKURU PWANI YASAIDIA KUKUSANYA BILIONI 1.5 KWA WAAJIRI WASIOCHANGIA WAAJIRIWA WAO

>> Waajiri walikuwa hawapeleki michango NSSF

Na Gustaphu Haule, Pwani

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Mkoa wa Pwani imesaidia kukusanya zaidi ya Tsh. Bilioni 1.5 kutoka kwa waajiri wasiowachangia waajiriwa wao NSSF .

TAKUKURU imekusanya fedha hizo katika kipindi cha Julai hadi Septemba 2024 ambapo ilifanya uzuiaji katika Mfumo wa ukusanyaji wa michango ya waajiri ambao walikuwa hawapeleki michango ya waajiri wao NSSF kama takwa la kisheria.

Naibu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Pwani Alli Haji, amesema kuwa meneja wa NSSF Mkoa Pwani alilalamikia upotevu  wa makusanyo kama michango ya waajiri inayosababisha upotevu wa fedha na usumbufu kwa wastaafu kutolipwa mafao yao kwa wakati.

        Naibu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Pwani Alli Hajji akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 13 ofisini kwake kuhusu utekelezaji wa majukumu katika kipindi cha Julai hadi Septemba mwaka huu.

Haji,amesema kuwa uzuiaji huo umefanyika baada ya kuwatafuta waajiri 77 ambao walikuwa na jumla ya deni la michango ya Tsh. zaidi ya bilioni 7.5 ambapo baada ya Takukuru kuingilia kati kuhusu ukusanyaji wa michango hiyo ndipo wadaiwa na NSSF wakakubaliana kuwa ifikapo Julai 2024 wafikie asilimia 20 ya deni lote.

Haji ameongeza kuwa TAKUKURU ilifuatilia kwa kusimamia sheria za mifuko ya hifadhi pamoja na sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007 na kufanikiwa kukusanya fedha zaidi ya Shilingi bilioni 1.5 ambapo makubaliano hayo yalifikiwa Kwa asilimia 103.

Aidha,waajiri hao 77 wamesema wapo tayari kushirikiana na TAKUKURU katika kuendeleza mapambano dhidi ya rushwa kwakuwa hawakuwa na elimu ya makosa ya rushwa kwa mujibu wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini na makosa ya mifuko ya hifadhi ya jamii.

Katika ufuatiliaji huo Haji amesema TAKUKURU ilibaini mambo mbalimbali ikiwemo baadhi ya waajiri hao hawakuwa wanajua kuwa kutokupeleka michango kwa wakati NSSF ni kosa kisheria.

Amesema kuwa waajiri wengine walikuwa hawapeleki michango kwa makusudi hivyo kusababisha kuvunja Sheria na kwamba mara Takukuru walipowapa maelekezo walichangia bila shaka yoyote .

Amesema kumekuwa na nia ovu kwa baadhi ya waajiri ili kupoteza fedha za watumishi wao na kujinufaisha kwa kutowalipia michango NSSF na baadae kutopata mafao kama stahili ya watumishi.

Kuhusu uchunguzi wa mashtaka Naibu Mkuu wa TAKUKURU huyo amesema kuwa katika kipindi hicho jumla ya malalamiko 88 yamefanyiwa uchunguzi na kati ya hayo malalamiko 68 yalihusu rushwa na kwamba taarifa hizo zimeshughulikiwa kwa mujibu wa Sheria kwa kuanzisha uchunguzi.

Taarifa 20 zilizobaki ambazo hazikuhusu rushwa zimeshughulikiwa kwa njia ya uelimishaji , uzuiaji,ushauri na kuhamishiwa idara nyingine ambapo hatahivyo Tamisemi zimetoka taarifa( 20,)Mifugo na Uvuvi (4)elimu (21),Polisi (5),Ardhi (6),Fedha (2),Maji (1) na Mahakama (4).

Amesema taarifa binafsi (2),Misitu (2)Amcos (1),Usafirishaji (2),Viwanda (1),Vyama vya Wafanyakazi (1), Ujenzi (2),Afya(7),Siasa(1),Manunuzi (1), na Maendeleo ya jamii (2).

Katika hatua nyingine Takukuru Mkoa wa Pwani kwa kipindi hiki imefungua jumla ya kesi mpya 22 Mahakamani ambapo kati ya hizo kesi 12 washtakiwa wametiwa hatiani.

Kuhusu masuala ya uchaguzi Haji amesema kuwa Takukuru Mkoa wa Pwani imejipanga Kuzuia na Kupambana na vitendo vya rushwa katika uchaguzi ambapo tayari wameanza kufanya ufuatiliaji wa vitendo vya rushwa kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Hatahivyo, Haji amesema Takukuru Mkoa wa Pwani inatoa wito kwa Wananchi kuendelea kuunga mkono jitihada za mapambano dhidi ya rushwa kwa kufichua wale wote wanaoshiriki kufanya vitendo vya rushwa kwa kutoa taarifa sahihi zitakazowezesha kuwachukulia hatua wahusika hasa katika kipindi cha kuelekea katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

No comments