CHUO CHA MAAFISA TABIBU MASWA KUJENGWA UPYA
>>Serikali yatoa Bilioni 2.9 za ujenzi
Na Samwel Mwanga , Maswa
SERIKALI kupitia Wizara ya Afya imetangaza kutoa Tsh. Bilioni 2.9 kwa ajili ya kujenga upya chuo cha Maafisa Tabibu Maswa, mkoa wa Simiyu ambacho kimekuwa kikihudumu kwa miaka 50 sasa.
Uamuzi huo umetokana na uchakavu wa majengo ya chuo hicho, hali inayohitaji hatua za dharura ili kuboresha miundombinu na mazingira ya kujifunzia.
Hayo yameelezwa Novemba , 29 mwaka huu na Naibu Waziri wa Afya, Dkt Godwin Mollel wakati wa mahafali ya 48 ya chuo hicho yaliyofanyika mjini Maswa.
Naibu Waziri wa Afya,Dkt Godwin Mollel akuzungumza katika mahafari ya 48 ya wahitimu wa Chuo cha Maafisa Tabibu wilaya ya Maswa
Dkt Mollel ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mahafali hayo amesema kuwa chuo hicho kimechangia kwa kiasi kikubwa kuzalisha maafisa tabibu ambao wanatoa huduma muhimu za afya hapa nchini kitaimarishwa kwa ujenzi wa miundombinu ya majengo na vifaa vya kujifunzia vya kisasa.
Lengo ni kuhakikisha kuwa wanafunzi wanapata mafunzo bora zaidi na vifaa vya kisasa, hatua itakayosaidia kuongeza ubora wa huduma za afya kwa Watanzania.
Amesema hatua hiyo inaonyesha dhamira ya serikali kuboresha sekta ya afya kupitia uwekezaji katika elimu ya afya na kuimarisha uwezo wa vyuo vya kitaaluma kutoa mafunzo ya kiwango cha juu na kwamba ni maendeleo makubwa yanayotarajiwa kuleta mabadiliko chanya kwa sekta ya afya nchini.
“ Mmnamaliza lakini mje mtembelee chuo chenu mwakani mwezi wa sita mtatakuta chuo kipya, utatamani urudie shule, nataka kuwahakikishia Rais Dkt, Samia Suluhu Hassan ametoa Tsh.Bilioni 2.9 kwa ujenzi wa chuo hiki.
‘Hivyo tatizo la upungufu wa vyumba vya madarasa, maabara ya vifaa vyake, mabweni litamalizwa na mwakani tutaongeza fedha nyingine ili ukija kufika hapa kwa kipindi cha miaka miwili kuanzia sasa utakuta chuo ni kipya,”amesema.
Amesema kuwa chuo hicho kilipoanzishwa mwaka 1974 kilianza kutoa kozi ya cheti kwa waganga wasaidizi vijijini na sasa kinatoa stashahada ya utabibu na ni miongoni mwa vyuo nchini ambavyo wahitimu wake wamekuwa wakifanya vizuri wanapokwenda kutoa huduma kwa wananchi.
Awali Rais wa serikali ya wananchuo wa chuo hicho, Simba Gulala amesema kuwa katika kuadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa kwa chuo hicho na kufanyika kwa mahafari ya 48 lakini bado kuna changamoto ya uchakavu na upungufu wa majengo yakiwemo madarasa,hosteli,bwalo,maabara pamoja na vifaa vya kufanyia mazoezi na hivyo kuwafanya kusoma katika mazingira yasiyo rafiki.
Rais wa Serikali ya Wanachuo,Chuo cha Maafisa Tabibu Maswa,Simba Gulala akisoma risala ya chuo hicho.wakati wa mahafari ya wahitimu wa stashahada ya utabibu .
“Leo ni miaka 50 tangu chuo hiki kianzishwe na haya ni mahafari ya 48 lakini Mgeni rasmi, Naibu waziri wa afya tumekuwa na mafanikio makubwa kitaaluma lakini tuna changamoto za uchakavu wa majengo sambamba na upungufu wa majengo na hata vifaa vya kujifunzia kwenye maabara.
“Vyumba vya madarasa, mabweni, bwalo, maabara vilivyopo havikidhi mahitaji yetu kuna upungufu mkubwa sana na majengo yote yaliyoko ndani ya chuo chetu yamechakaa na kufanya hali ya kujifunza kutokuwa katika mazingira rafiki.
Naye mkuu wa chuo hicho, Hangwa Enos Hangwa amesema kuwa tangu kuanzishwa kwa chuo cha maafisa Tabibu Maswa hadi sasa kimeweza kuandaa wataalam 2, 255 katika fani ya Utabibu na kina miliki eneo lenye ukubwa wa hekta 6.11 hivyo lina nafasi kubwa ya uendelezaji wa miundo mbinu ya majengo.
Mkuu wa chuo cha Maafisa tabibu Maswa, Dr Hangwa Enos (kushoto) akisalimiana na Naibu Waziri wa Afya, Dkt Godwin Mollel wakati wa mahafari ya chuo hicho.
Amesema kuwa kwa sasa chuo hicho kinatoa fani moja pekee ya stashahada ya Utabibu huku kikiwa na vyumba viwili vya madarasa,maabara ya tiba moja,bwalo moja,jengo la utawala lenye ofisi nane ,jiko moja na mabweni 14 yenye uwezo wa kubeba wanafunzi 112 pamoja na nyumba nne za watumishi ambapo majengo yote yanahitaji ukarabati mkubwa.
Agape Slivester mkazi wa Chato mkoani Geita ambaye ni miongoni mwa wazazi waliofika kushuhudia mahafali hayo amesema kuwa uamuzi wa Serikali kuamua kujenga upya chuo hicho inaashiria dhamira yake kuimarisha elimu ya afya na kuboresha miundombinu ya kufundishia.
“Uwekezaji huu utasaidia kuongeza idadi ya maafisa tabibu, kuboresha mazingira ya kusomea na kufundishia na hatimaye kuboresha huduma za afya kwa Watanzania,”amesema.
Naye Japhet Luhele mkazi wa Bukoba mkoa wa Kagera amesema kuwa kauli iliyotolewa na Naibu waziri wa afya juu serikali kutoa kiasi cha fedha Tsh. Bilioni 2.9 kwa ajili ya ujenzi wa chuo kipya cha Maafisa Tabibu mjini Maswa.
Baadhi ya wageni waliohudhuria mahafari ya wahitimu wa stashahada ya utabibu katika chuo cha maafisa tabibu Maswa.
Amesema ni fursa ya kuendeleza teknolojia za kisasa katika sekta ya afya kupitia mafunzo ya kisasa na ni hatua kubwa inayotarajiwa kuleta manufaa kwa jamii kwa ujumla.
Mkuu wa wilaya ya Maswa, Aswege Kaminyoge amesema kuwa tangu Rais Samia aingie madarakani wilaya hiyo ilikuwa na vituo vya afya vutatu lakini kwa sasa vipo sita na wilaya hiyo imepokea fedha nyingi kutoka serikalini zaidi ya Shilingi Bilioni 70 kwa ajili ya miradi ya maendeleo ikiwemo ya sekta ya afya.
Mkuu wa wilaya ya Maswa,Aswege Kaminyoge akiwasalimia wananchi katika mahafali ya 48 ya wahitimu wa Chuo cha Maafisa Tabibu wilaya ya Maswa.
“Kwa niaba ya wananchi wa Wilaya ya Maswa nimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi anayoifanya ya kuiletea maendeleo wilaya yetu.
" Kwa kipindi cha miaka minne sasa tangu aingie madarakani, wilaya hiyo imeshapokea zaidi ya Tsh. Bilioni 70 kwa ajili ya miundo mbinu ya miradi mbalimbali ikiwemo ya sekta ya Afya,”amesema.
Post a Comment