MILIONI 8 ZACHANGWA KUSAIDIA CHAMA CHA WASIOONA TARIME
>>Waliochanga fedha yumo DC Tarime, Josephati, Jonathan, Sasi, Orindo, mchungaji Nyamongo SDA, Mkurugenzi Kampuni ya Waracha, Rin, Kemanyanki Spring hotel, Winers
Na Dinna Maningo, Tarime
ZAIDI ya Tsh. Milioni nane zimechangwa kwa ajili ya kukiwezesha chama cha wasioona (TLB) wilaya ya Tarime, mkoani Mara kwa ajili ya kutekeleza shughuli za kiofisi na vikao vya chama.
Changizo hilo limefanyika wakati mkuu wa wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele akikabidhi fimbo nyeupe 58 na miwani mitano kwa wanachama wasioona wilayani humo.
Mkuu wa wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele akimpatia fedha msanii mwenye ulemavu wa macho baada ya kuvutiwa na wimbo
Msaada huo wa fimbo nyeupe na miwani umetolewa na mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya ujenzi na usambazaji wa vifaa mbalimbali WARACHA, Daud Tindo mkazi wa Kijiji cha Nyangoto- Nyamongo.
Fimbo hizo zimenunuliwa kwa thamani ya Tsh. 1,400,000 na miwani yenye thamani ya Tsh. 400,000 ambapo pia Daud amechanga Tsh.500,000 na kufadhili gharama za usafiri kwa wasioona 45 walioshiriki katika hafla hiyo.
Mkuu wa wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele (kulia) akimkabidhi fimbo nyeupe Mwenyekiti wa Chama cha wasioona mkoa wa Mara (kushoto) zilizotolewa na Mkurugenzi wa kampuni ya ujenzi ya WARACHA, Daud Tindo hayupo pichani
Mkuu huyo wa wilaya baada ya kutoa hotuba yake amechangia Tsh. Milioni moja kisha akaombwa kuungwa mkono na wadau mbalimbali walioshiriki katika hafla hiyo. Baadhi ya wadau wengine hawakufika lakini walituma michango yao na wengine kuahidi.
Katika changizo hilo Tsh. 3, 335, 000 zilichakwa papo hapo na ahadi zaidi ya Tsh. Milioni 5. " Niwapongeze wanachama kwa kuwaibua na kuwaunganisha wasioona hili ni jambo njema, umoja ni nguvu utengano ni dhaifu.
Wanachama wasioona wakiwa kwenye hafla ya kupokea fimbo nyeupe iliyofanyika ukumbi wa Ingwe Sekondari- Nyamongo
" Nami katika kuwaunga mkono natoa Tsh.Milioni moja naomba mwenye chochote aniunge mkono ili tuwasaidie wenzetu wasioona" amesema Meja Edward.
Waliochanga fedha kusaidia wenye ulemavu wa macho ni pamoja na Mkurugenzi wa kampuni ya ujenzi ya RIN LTD, Isaack Range mkazi wa Kijiji cha Nyangoto -Nyamongo aliyechanga Tsh. Milioni moja na kuahidi kutoa Tsh .Milioni nne ifikapo Desemba, 6, 2024 saa nne kamili asubuhi ambapo aliwapa fedha Tsh.500,000 waimbaji wawili wasioona baada ya kuimba vizuri na hivyo kumvutia.
" Kampuni ya RIN hairudi nyuma , Bhoke aliniambia nikaribie na mimi nikasema nitakuja nifanye jambo, nimeona nije mwenyewe bila kutuma mwakilishi. Nilisema hata kama nipo bize nitakuja niungane nanyi nifanye jambo niwasaidie mtakapokwama.
"Mimi kwenye kazi sibagui dini, kabila, Chama maana Mungu alisema tupendane hivyo natoa Tsh. Milioni moja na tarehe sita mwezi Desemba saa nne kamili nitatoa Tsh. Milioni 4 zikamilike Tsh. Milioni tano.
Mkurugenzi akavutiwa na wasanii wawili kutoka wilaya ya Serengeti waliofika kutoa burudani ya nyimbo na hivyo akatoa Tsh. 500,000 na kuwapatia wagawane kila mmoja Tsh. 250,000.
Mkurugenzi wa kampuni ya ujenzi ya RIN LTD, Isaack Range akiwapatia fedha wasanii wenye ulemavu wa macho walioimb wimbo, aliyesimama kushoto ni mkuu wa wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele
" Nimevutiwa na nyimbo nzuri zilizoimbwa na wasioona, naomba niwapatie Tsh.500,000 mgawane. Nampongeze WARACHA kwa kuwasaidia fimbo nyeupe wasioona, ni jambo jema kuwasaidia watu wasiojiweza " amesema mkurugenzi RIN.
Diwani Mstaafu Agustino Sasi mkazi wa Kijiji cha Kewanja-Nyamongo amechanga Tsh. 200,000 huku akimshukuru mkuu huyo wa wilaya kufika kujumuika na wasioona.
" Nilikuwa Dar es Salaam nilipigiwa simu na Bhoke mwenye ulemavu wa macho akanialika kushiriki hafla ya kukabidhi wa fimbo nikasema lazima nifike. Nakupongeza sana DC maana wengine wakialikwa wanatuma wawakilishi, ni vyema kuwasaidia watu wenye ulemavu hata kwa kidogo tunachopata" amesema Agustino .
Mkazi wa Kijiji cha Nyangoto John Jonathani amechanga Tsh. 500,000 na kusema ndio mara yake ya kwanza kualikwa kwenye shughuli za watu wenye ulemavu wa macho.
" Watu wakusaidiwa ni wasioona, tunajifunza hata habari za Yesu aliwahurumia na aliwatendea mema. Tuelekeze nguvu kusaidia wasioona nami naahidi ushirikiano nanyi " amesema John.
Wengine waliotoa michango yao ni Josephati Mwita ametoa Tsh.300,000 na kufadhili maji na soda kiasi cha Tsh.170,000 wakati wa kikao hicho. Mkurugenzi wa hoteli ya Silver Spring, Godfrey Kubyo amechangia Tsh. 500,000 pamoja na kufadhili chakula.
Kampuni ya KEMANYANKI imetoa Tsh. 150,000, Julias Orindo mzazi wa mtunza hazina TLB ametoa Tsh. 200,000, Winers Tsh. 100,000 , Mchungaji Doto Shija wa kanisa la waadventista wasabato Nyamongo kati Tsh. 100,000 na wengine waliahidi kutoa michango yao ifikapo Desemba, 6, 2024 .
Mwenyekiti wa Chama cha wasioona mkoa wa Mara, Nyamlanga Rwakatare amemshukuru mkuu wa wilaya ya Tarime na wadau wa maendeleo kukutana nao na kuwachangia fedha.
" Hii ni shughuli ya kwanza mkoani kwetu Chama cha wasioona kupewa fimbo nyeupe na miwani. WARACHA tunakupongeza sana , tunaomba wadau wengine waendelee kutusaidia WARACHA pia endelea kutusaidia" amesema Nyamlanga.
Mtunza hazina wa Chama cha wasioona wilaya ya Tarime, Bhoke Jonathan ambaye amekuwa mstari wa mbele kutafuta wafadhili kufadhili vikao na vifaa kwa ajili ya wasioona amemshukuru mkuu wa wilaya kwa kufika kushirikiana nao.
" Tunakushukuru mkuu wa wilaya kwa kutuheshimisha kufika na kukaa nasi hapa Nyamongo. Tunawashukuru na wadau wengine waliofika na wanaotuunga mkono. Tunakushukuru Mkurugenzi wa Kampuni ya WARACHA umekuwa mstali wa mbele kutushika mkono hakika vifaa ulivyotusaidia vitatusaidia sana wasioona.
"Tunakushukuru mkurugenzi wa RIN kutupatia fedha milioni tano pamoja na Kampuni ya KEMANYANKI ambao wamekuwa mstali wa mbele kukuchangia fedha pindi tunapowaomba msaada pamoja na wadau mbalimbali ambao sijawataja majina kutokana na ufinyu wa muda " amesema Bhoke.
Post a Comment