HEADER AD

HEADER AD

DC TARIME AZIAGIZA HALMASHAURI KUTENGA BAJETI YA WATU WENYE ULEMAVU WAKIWEMO WASIOONA


>>Awaagiza maafisa maendeleo ya jamii kupita kwenye vijiji na mitaa kuwatambua watu wenye ulemavu

>>Awataka wasimamizi wa barabara  kuwa sehemu ya msaada kwa wasioona

Na Dinna Maningo, Tarime

MKUU wa wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele ameiagiza halmashauri ya wilaya ya Tarime na halmashauri ya mji Tarime, kutenga bajeti ya fedha kwa ajili ya kuwawezesha watu wenye ulemavu wa viungo wakiwemo wasioona pindi wanapohitajika kwenda kwenye makongamano ,warsha mbalimbali na mahitaji mengineyo.

Pia amewaagiza maafisa wa maendeleo ya jamii kuhakikisha wanapita katika vijiji na mitaa yote kuwatambua wenye ulemavu , wenye changamoto lakini pia kutafuta namna ya kuwasaidia na kuwaunganisha na vyama vya watu wenye ulemavu kikiwemo chama cha wasioona (TLB).

        Mkuu wa wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele

Mkuu huyo wa wilaya ameyasema hayo Novemba, 29, 2024 wakati akikabidhi fimbo nyeupe 58 na miwani 5 kwa wanachama wasioona wilaya ya Tarime, msaada uliotolewa na mkurugenzi wa kampuni ya ujenzi na usambazaji wa bidhaa mbalimbali ya WARACHA, Daud Tindo ,hafla iliyofanyika ukumbi wa shule ya sekondari Ingwe-Nyamongo.

"Kuna viziwi, mabubu, wasioona wenye ulemavu wa viungo, wenye ulemavu wa ngozi.Wana vyama vyao tuwatambue . Na niombe jamii tusiwafiche ndani wapewe fursa za elimu, ajira.

" Hata serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ina watu wengi wenye changamoto na imewapa nafasi na wanafanya vizuri.

" Naziagiza halmashauri zote mbili kuhakikisha wanatenga bajeti ya watu wenye ulemavu wakiwemo wasioona. Wanapokwenda kwenye makongamano mbalimbali, warsha kuna mambo mengi wanayoyapata ya kuwasaidia " amesema DC Edward.

Ameongeza kusema " Nisije nikasikia kuwa wamekosa fursa ya kukutana na wenzao wa wilaya tofauti, mkoa tofauti na Taifa katika kufanya mambo yao. Na hilo lifike kwa wakurugenzi wa halmashauri mimi kama mlezi wa chama nisingependa kusikia wamekosa fursa hiyo

" Jambo la mara moja kwa mwaka mnashindwa nini ?, halmashauri zetu zote zina fedha za kutosha. Rais wetu ameagiza kuhakikisha haya makundi tunayagusa na kuyafikia. Nikiwepo hapa nitahakikisha mnapata stahiki zenu nikiwa kama mlezi wenu.

Meja Edward amewataka wasimamizi wa barabara kuwasaidia wasioona wanapotembea na wanapotaka kuvuka barabara ili kuwaepusha na ajali za barabarani.

        Wasioona wakiwa kwenye hafla ya kupokea fimbo nyeupe zilizotolewa na Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya WARACHA, Daud Tindo

" Inasikitisha mtu asiyeona yupo barabarani anagongwa. Nitoe wito kwa wale wanaosimamia usalama barabarani tuwe sehemu ya msaada kwa hawa ndugu zetu. Na wale wanaotumia vyombo vya moto tuhakikishe tunawalinda watumiaji wa barabara" amesema Meja Edward.

Akisoma Risala kwa mgeni rasmi Mwl. Cornery Makangira ameeleza changamoto zinazokikabili chama cha wasioona ikiwa ni pamoja na ukosekanaji wa vifaa au zana saidizi kwa watu wasioona.

Mwl. Cornery Makangira akisoma Risala kwa mgeni rasmi Mkuu wa wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele aliyefika kuwakabidhi fimbo nyeupe wenye ulemavu wa macho zilizotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya WARACHA, Daud Tindo

" Kuna mtazamo hasi, mira na desturi kwa wasioona, chama cha wasioona kutokuwa na ofisi ili kuendesha shughuli zake kwa urahisi. Hali hiyo imesababisha wanachama wengi kukosa mahali pakukutania ili kujadili fursa , changamoto katika masuala hayo.

" Jamii nyingi ya wasioona wameshindwa kufikia shughuli za kiuchumi, wapo wasioona hawasomi, changamoto ya ajira mfano katika mgodi wa Barrick North Mara hakuna mwenye ulemavu wa macho aliyepata ajira mgodini" amesema Mwl.Cornery.

Mkuu huyo wa wilaya ameahidi kuzifanyia kazi changamoto zilizoelezwa kwenye risala huku akiwaomba viongozi wa TLB kufanya kazi kwa pamoja.

      Mkuu wa wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele wakiwa kwenye picha ya pamoja Mwl. David Siliwa mwenye ulemavu wa macho wakati wakiwa kwenye hafla ya kuwakabidhi fimbo nyeupe zilizotolewa na Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya ujenzi ya WARACHA, Daud Tindo.

" Risala yenu nimeipokea vizuri, changamoto zenu nimeziona naenda kuzifanyia kazi, lakini niwaombe viongozi naomba tufanye kazi Halmashauri kutotoa fedha kwa ajili ya wasioona kushiriki kwenye maadhimisho ya fimbo nyeupe na makongamano mengine yanayowakutanisha wasioona " amesema.

" Nami nitakuwa mstari wa mbele kuwatafutia mashirika, makampuni ili waweze kuwakumbuka katika mahitaji yenu, tufanye kazi kwa pamoja ili tuweze kuwasaidia ndugu zetu wenye uoni hafifu ikiwa ni pamoja na wale wenye changamoto ya ngozi" amesema Meja Edward.

" Nikupongeze WARACHA kwa msaada wa vifaa ulivyovotoa kwa wasioona, naamini huu ni mwanzo na makampuni mengine yajitokeze yawasaidie wahitaji. Msaizidi wangu naomba uandike haya makampuni yote yaliyoalikwa  hapa tuyakumbushe kuhusu mahitaji ya hawa wenzetu.

Mkuu huyo wa wilaya amekiahidi chama hicho cha wasioona na vyama vingine vya watu wenye ulemavu kuwa atawaunganisha na mashirika na makampuni yenye uwezo yanayofanya kazi ndani ya wilaya hiyo.

      Wasioona wakiwa kwenye hafla ya kupokea fimbo nyeupe zilizotolewa na Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya WARACHA, Daud Tindo hayupo pichani

Amempongeza mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya ujenzi ya RIN, Isaack Range kwa kukichangia chama hicho Tsh 5,000,000 pamoja na michango ya wadau wengine waliomuunga mkono kukichangia chama fedha katika hafla hiyo na kupatikana Tsh.Milioni 3.5 na ahadi Tsh. Milioni 5.3.

Mkurugenzi wa Kampuni ya WARACHA, Daud Timbo, amesema kuwa ataendelea kushirikiana na chama hicho katika kutatua changamoto zinazowakabili na kwamba matamanio yake ni kuona watoto wenye ulemavu wa macho wanapata elimu

  Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya ujenzi ya WARACHA, Daud Tindo ( kushoto)

Amewaomba wananchi kuendelea kuwaibua watoto waliofichwa kwani kuna baadhi ya wazazi wanawaficha ndani watoto wenye ulemavu wa viungo.

Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya RIN, Isaack Range amesema Kampuni yake imekuwa ikitoa misaada mbalimbali katika jamii bila kubagua dini, kabila wala chama cha siasa na kuahidi ushirikiano.

No comments