SHAIRI : BAMBA
Nimezunguka nyumbani, ninatafuta ubamba,
Taka nizopata ndani, shimo taka nimechimba,
Kinakosekana nini, ubamba katika nyumba,
Kwa usafi wa nyumbani, muhimu sana ubamba.
Nimezungukazunguka, kuchungua kila chumba,
Hadi sasa nimechoka, wala hakuna ubamba,
Mbona hivi ni vibweka, nyumba kukosa ubamba?
Kwa usafi wa nyumbani, muhimu sana ubamba.
Zazalishwa takataka, zile pilika za nyumba,
Kuzichota utachoka, bila kuwa na ubamba,
Kwanza zitatawanyika, na kuichafua nyumba,
Kwa usafi wa nyumbani, muhimu sana ubamba.
Wapangaji ni watatu, na wa nne mwenye nyumba,
Watoto ni watukutu, na wachafuzi wa nyumba,
Mwaishije ninyi watu, pasipokuwa ubamba?
Kwa usafi wa nyumbani, muhimu sana ubamba.
Nyumba nzuri ni ubamba, hapo ndipo unabamba,
Kukosekana ushamba, hata kama ukivimba,
Mazingira bora nyumba, usafi tunauimba,
Kwa usafi wa nyumbani, muhimu sana ubamba.
Shairi limetungwa na Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602
Post a Comment