HEADER AD

HEADER AD

KAMATI YA RUFAA TARIME YAREJESHA MAJINA YA WAGOMBEA WALIOKUWA WAMEENGULIWA


>>Waliokata rufaa CHADEMA walikuwa 128, kati ya hao 90 wamekubaliwa kugombea, 38 watupiliwa mbali

>>  Waliokata rufaa CCM ni 9, watatu wakubaliwa, 6 watupiliwa mbali

ACT Wazalendo rufaa 7 wote wamerejeshwa kugombea

>>DAS Tarime aeleza sababu za kukataliwa na kukubaliwa

Na Dinna Maningo, Tarime 

KAMATI ya Rufaa ya wilaya ya Tarime, mkoa wa Mara, imewarejesha wagombea 100 kati ya 144 waliokata rufaa wakilalamika majina yao kuenguliwa na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi katika nafasi za uenyekiti wa Kijiji, Kitongoji, Mtaa na Ujumbe.

Kamati hiyo ya wilaya imepitia rufaa za wagombea kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM), Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambapo baadhi yao wamerejeshwa kugombea na wengine wamekataliwa kutokana na kutokidhi vigezo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Rufaa wilaya ya Tarime, Mwl. Saul Mwaisenye, amesema jumla ya rufaa za wagombea kutoka CHADEMA wilaya nzima zilikuwa 128 kati ya hizo zilizokubaliwa ni 90.

" Tulikuwa na siku tano za kupokea rufaa , tulianza kupokea tangu tarehe 10 hadi tarehe 15 mwezi huu. Katika rufaa 128 tuliweza kuwarejesha wagombea 90 wa CHADEMA na 38 rufaa zao zilitupiliwa mbali.  Chama cha Mapinduzi (CCM) rufaa zao zilikuwa 9 kati ya hizo tatu zimekubaliwa na 6 zimekataliwa.

" Rufaa za Chama cha ACT Wazalendo zilikuwa saba na wote wamerejeshwa kugombea . Tuliagiza warejeshwe kwenye mchakato kwa sababu mbalimbali ambazo wengi wao walikuwa wameondolewa kutokana na changamoto ndogo ndogo ambazo hazikuwa za kikatiba na kikanuni" amesema Mwl. Saul.

" Wengine makosa yalikuwa madogomadogo kama kukosea kuandika majina za vijiji, vitongoji wanakogombea, kupishana kwa herufi za majina. 

"Kuna mwingine anagombea uenyekiti wa kijiji mtu wa CHADEMA,ikadaiwa hajui kusoma wala kuandika ilibidi tumpe karatasi tukamwambia aandike maneno fulani akayaandika . Wengine ni makosa ya r na l. kwahiyo tumewarejesha.

" Yapo maeneo walisema kwamba walienguliwa kwasababu walichelewa kurudisha fomu lakini baada ya kufuatilia ilionekana fomu zao zilikuwa zimepokelewa , tuliamini basi waliwahi ndani ya muda kwasababu ingekuwa nje ya muda basi fomu zisingepokelewa" amesema Mwl. Saul.

"Kwa kuzingatia 4R za Rais , yaani R nne (maridhiano, mabadiliko, ustahimilivu na kujenga upya) tukaona wenye vigezo ni vyema wakarudi ili waende kushindana kwenye box na rufaa 90 za CHADEMA zimekubaliwa, rufaa 38 zimetupiliwa mbali zimekataliwa. Wagombea hawakukidhi matakwa ya kikanuni.

" Zipo sababu mbalimbali zilizotufanya tusizikubali ikiwa ni pamoja na kutojiandikisha , wapo wagombea ambao walikuwa hawajajiandikisha kwenye daftari la makazi. Sasa usipokuwa umejiandikisha unakuwa umepoteza sifa ya kushiriki kugombea na kupiga kura " amesema Mwl Saul.

Mwenyekiti huyo wa rufaa ameongeza kusema " Walikuwepo wagombea walioku na maslahi ya kijiji. Kanuni zetu zinazuia mtu anapogombea asiwe na maslahi yoyote na kijiji au mtaa.

" Wapo tuliowaengua wana maslahi na Kijiji, wapo baadhi ya wagombea uraia wao ulikuwa na mashaka, kama mnavyofahamu sisi tupo mpakani tuna jukumu la ulinzi na usalama. Kwa wale ambao uraia wao ulionekana kuwa na mashaka rufaa zao hatukuzikubali " amesema Mwl. Saul.

Amesema kuwa wapo waliohukumiwa kifungo cha zaidi ya miezi sita , hao wanakuwa wamepoteza sifa ya kuweza kushiriki kwenye zoezi la kugombea, wengine hawakujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura. 

Ametoa wito kwa vyama vyote vya siasa ambavyo wamekamilisha ugombea wao washiriki kwenye kampeni katika hali ya usalama , kampeni zitakazoanza kesho hadi Novemba, 26 na kwamba tarehe 27 litafanyika zoezi la kupiga kura kuwachagua viongozi serikali ya Kijiji, Kitongoji, mtaa na ujumbe.

" Tunategemea kampeni kuanza kuzinduliwa siku ya kesho, Novemba, 20,2024 . Tayari ratiba viongozi wa vyama wameshapeleka ratiba zao kwa wasimamizi wa uchaguzi nao wanapeleka kwa wakuu wa Polisi wa wilaya ili waweze kuratibu ulinzi kwenye kampeni.

"Jukumu lililobaki kama ofisi ya wilaya ni ulinzi tu , kutoa ulinzi kuhakikisha ulinzi na usalama unakuwepo wakati wa kampeni, uchaguzi. Jukumu la uchaguzi lipo kwa wasimamizi wa uchaguzi ambao ni wakurugenzi wetu wa halmashauri ya mji na wilaya.

"Tunaomba wananchi wote waliojiandikisha wilaya ya Tarime watumie haki yao ya msingi wakapige kura" amesema DAS Tarime. Sisi Kamati ya rufaa tulishamaliza kazi yetu na tulijitahidi kusimamia 4R kwani katika wagombea 128 wa CHADEMA wamerejeshwa wagombea 90, sio kazi ndogo" amesema.

Kauli ya ACT Wazalendo 

Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo mkoa wa Mara, Charles Mwera, ameipongeza kamati ya rufaa kwa kuwarejesha wagombea wao waliokuwa wamewekewa mapingamizi na kuenguliwa.

"Naipongeza Kamati ya rufaa inayoongozwa na DAS Tarime kwa kututendea haki kuwarejesha wagombea wetu. Tunajua ni wajibu wa kanuni za uchaguzi, ila kitendo cha kushughulikia rufaa za wagombea wetu na kuwarejesha tunashukuru kwakweli " amesema Charles.

Kauli ya Chadema

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Jimbo la Tarime mjini, Bashiri Abdallah amesema katika Jimbo lake wagombea wawili wameenguliwa.

" Wawili tu ndio wameenguliwa kwa makosa yao wenyewe, mmoja alikuwa anagombea mtaa wa sabasaba na mwingine mtaa wa Anglikana. Nachoomba watu wote wafuate kanuni kuhakikisha kampeni zinakwenda vizuri.

" Tulikuwa kwenye kikao cha kuandaa ratiba , tumejitahidi kupanga ratiba vizuri ili kila mtu asimwingilie mwenzake " amesema Bashiri.

No comments