HEADER AD

HEADER AD

RC SIMIYU AMWAGIZA DC BUSEGA KUMALIZA MGOGORO KATI YA WAFUGAJI NA WAKULIMA


Na Samweli Mwanga, Busega
 
MKUU  wa mkoa wa Simiyu, Kenani Kihongosi amemwagiza mkuu wa wilaya ya Busega mkoani humo, Faidha Salim kuchukua hatua za haraka na kumaliza migogoro kati ya wakulima na wafugaji katika Kata ya Kiloleli wilayani humo inayotishia amani na usalama katika jamii hiyo.
 
Ameutaka uongozi wa wilaya hiyo kushughulikia suala hili kwa haki, huku akisisitiza kuwa sheria zifuatwe na kila mtu anayevunja sheria achukuliwe hatua stahiki bila upendeleo.

     Mathias  Shigemelo mkazi wa Kiijiji cha Mwamisenya wilaya ya Busega akielezea kero ya wafugaji mbele  ya Mkuu wa mkoa wa Simiyu,Kenani Kihongosi(hayupo pichani)

Kauli  hiyo inasisitiza umuhimu wa kuimarisha amani na utulivu kati ya wakulima na wafugaji, wa eneo hilo ambao wamekuwa wakiingia katika migogoro ya mara kwa mara  kutokana na mgongano wa maslahi, hasa kwenye matumizi ya ardhi.
 
Akizungumza Novemba 18, 2024  na wananchi wa Kata hiyo katika kijiji cha Masanza  katika mkutano wa hadhara wa kusilkiliza kero na kuzitatua amesema kuwa  kila mwananchi katika nchi hii ana haki sawa na mwingine.

Amesema kuwa hakuna aliye juu ya sheria na inapotokea wafugaji wanawanyanyasa wakulima wanavunja sheria hili jambo ni lazima hatua zichukuliwe kwa watu wote wafikishwe katika vyombo vya sheria.

           Baadhi ya viongozi wa wilaya ya Busega mkoa wa Simiyu(waliokaa kwenye viti) wakimsikiliza Mkuu wa mkoa huo,Kenani Kihongosi (hayupo pichani) katika mkutano wa hadhara wa kusikiliza kero katika Kata ya Kiloleli.

“Nitumie mkutano huu kusema hakuna mtu aliye juu ya sheria na inapotokea wakulima wanawanyanyaswa na wafugaji haikubali hata kidogo huko ni kuvunja sheria ni lazima hatua zichukuliwe,”
 
“Nikuombe mkuu wa wilaya na kamati yako ya ulinzi na usalama hili jambo likiendelea  kesho litatuletea mauaji yanaweza kutokea, mtu anayevunja sheria kamateni na pelekeni mahakaman.

"Huu utaratibu wa kukamata watu na kesho kuwatoa hapana  wafikishwe mahakamani, kwa mkoa wa Simiyu hatuwezi kuruhusu mambo haya,”amesema Kihongosi.
 
Amina Yohana mkazi wa kijiji cha Masanza Kona amemweleza mkuu wa mkoa huo kuwa  kero yake wafugaji wamekuwa wakiingiza mifugo yao katika shamba lake na anapowaeleza wanatishia kumpiga kwa kutumia fimbo ambazo kwa mbele zimewekewa vyuma.

          Sehemu ya wananchi wa kijiji cha Masanza wilaya ya Busega waliohudhuria mkutano wa hadhara wa Mkuu wa mkoa wa Simiyu,Kenan Kihongosi
 
“Mimi na uzee wangu ninalima ninahangaika lakini wafugaji wanaingiza mifugo yao inakula mazao lakini ukiwaeleza wanakutishia kukupiga kwa kutumia fimbo zao na nimeshatoa malalamiko yangu kwa viongozi wa eneo letu lakini hakuna hatua zozote zinazochukuliwa dhidi yao,”amesema Amina.
 
Naye Mathias  Shigemelo mkazi wa Kiijiji cha Mwamisenya amesema kuna wafugaji hawajui ubinadamu wamekuwa wanavamia na kuwapiga watu na hivi karibuni askari polisi waliwakamata lakini muda si mrefu waliachiwa na kuendelea kuachia mifugo yao ambayo imekuwa ikila mazao yao mashambani.

        Mathias  Shigemelo mkazi wa Kiijiji cha Mwamisenya wilaya ya Busega akielezea kero ya wafugaji mbele  ya Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Kenani Kihongosi (hayupo pichani)

“Kipindi hiki cha kilimo ni muhimu kwa uzalishaji wa chakula, na hivyo suala hili linapaswa kushughulikiwa haraka ili kuzuia madhara makubwa kwa uchumi wa kijamii, amani na ushirikiano kati ya wakulima na wafugaji ni muhimu kwa maendeleo endelevu ya jamii,”amesema Shigemelo.
 

No comments