LEODGER AANZISHA SAMIA CUP KUHAMASISHA UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA
Na Alodia Dominick, Bukoba
MJUMBE wa Baraza Kuu la Umoja wa Vijana (UVCCM ) Taifa kutoka mkoa wa Kagera Leodger Leonard Kachebonaho ametaja lengo la kuanzisha Samia Cup kuwa ni kuonyesha na kuhamasisha maendeleo pamoja na kuhamasisha jamii kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, mwaka huu.
Kachebonaho ameyasema hayo Novemba 07, 2024 wakati wa mkutano wa maandalizi ya uzinduzi wa ligi ya Samia itakayoanza Novemba 9, 2024 mkoani Kagera na mgeni rasmi katika mkutano huo alikuwa ni mkuu wa mkoa wa Kagera Fatma Mwassa.
Amesema ligi hiyo wameiita Samia Cup baada ya washirika mbalimbali wa ligi hiyo kukaa na kuona shughuli mbalimbali za maendeleo zilizofanyika katika mkoa wa Kagera lakini namna ambavyo amekuwa akihamasisha wananchi hususani katika kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa.
“Lengo kubwa la kufanya mashindano hayo ni kuhamasisha wananchi wote wa mkoa wa Kagera waweze kujitokeza kwa wingi kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 27, 2024.
" Kwa hiyo tukaona michezo ndiyo sehemu pekee inaweza kutukutanisha sisi vijana na jamii kwa ujumla kwa umoja wetu pasipo kujali itikadi ya kitu chochote na ligi hiyo itajumuisha vijana wote katika wilaya nane za mkoa huu” amesema Kachebonaho.
Amesema mchezo wa fainali utafanyika Novemba 23, 2024 uwanja wa Kaitaba mshindi wa kwanza atapata zawadi wa shilingi milioni 10, mshindi wa pili milioni 5 na mshindi wa tatu milioni 3.
Kwa upande wake katibu wa chama cha soka mkoa wa Kagera Ally Amin Abdul akitambulisha mashindano ya Samia Kagera Cup amesema yako tayari na yataanza Novemba 9, 2024, mechi ya ufunguzi itakuwa ni kati ya Bukoba manispaa na Muleba katika uwanja wa Kaitaba na mechi zimewekwa katika makundi mawili zitacheza nyumbani na ugenini.
Mdau wa michezo kutoka Luninga ya Clouds media Shafii Dauda amesema mpira wa miguu ni kiungo kinachoweza kufikisha elimu na jumbe mbalimbali kwa jamii.
“Linapokuja jambo ambalo linawalenga vijana ambao ni nguvu kazi ya taifa inanilazimu kushirikiana na wadau wengine jinsi gani vijana wataweza kuonyesha vipaji vyao na kuweza kuviinua kama sera ya chombo ninachokifanyia kazi kinavyolenga vijana chini ya miaka 35” amesema Dauda.
Mkuu wa mkoa wa Kagera Fatma Mwassa amesema kuwa, pamoja na mashindano hayo ya Samia Cup ambayo yatakuwa mwendelezo kila mwaka yatasaidia kupatikana timu bora mkoani humo na hivyo mkoa wa Kagera kuwa na timu mbili ikiwemo ya Kagera Sugar.
Aidha amesema mkoa huo una mpango wa kuanzisha shule ya michezo itakayosaidia kukuza vipaji vya vijana.
Mkuu wa mkoa wa Kagera Fatma Mwassa akikabidhi jezi na mpira.
Post a Comment