MGOGORO KATI YA PEACE GOLD MINE BUTIAMA NA JOHN GIMUNTA WAIKOSESHA SERIKALI MAPATO
>> Viroba vya mawe ya dhahabu vyasota miezi mitatu bila kuuzwa
>> Wanakikundi wasema wamegoma kuuza baada ya kumpatia John Gimunta Milioni 5 kufuatilia leseni lakini akazitumia kupata leseni yake binafsi
>> Gimunta awakana, Wanawake wafunguka, RC Mara aingilie kati
Na Dinna Maningo, Butiama
ZAIDI ya Viroba elfu kumi vya mawe yanayodhaniwa kuwa na dhahabu vya wachimbaji wadogo wa dhahabu kikundi cha Peace Gold Mine, vimesota miezi mitatu bila kuuzwa kutokana na kuibuka mgogoro wa kimaslahi baina yao na mchimbaji John Gimunta .
Wachimbaji hao wenye mashimo (maduara ) katika mgodi wa dhahabu wa wachimbaji wadogo uliopo Kijiji cha Magunga maarufu mgodi wa Buhemba, Kata ya Mirwa wilaya ya Butiama, mkoani Mara wameshindwa kuuza viroba hivyo baada ya kugoma kulipa mapato asilimia 30 kwa John Gimunta kama mmiliki wa leseni ya uchimbaji katika eneo hilo.
Wanakikundi hao wamesema kuwa wameshindwa kumlipa Gimunta asilimia hizo kwakuwa aliwasaliti baaada ya kuchanga fedha Tsh. Milioni 5 na kumpatia kwa ajili ya malazi, nauli, chakula, ufuatiliaji ili wapate leseni ya uchimbaji ya kikundi.
Wanakikundi wamesema kuwa Gimunta amewasaliti na kujipatia leseni yake binafsi inayotambulika kwa jina la Tarani Mining Group badala ya leseni iliyotakiwa kutambulika kwa jina la kikundi cha Peace Gold Mine.
Mgogoro huo umepelekea halmashauri ya wilaya ya Butiama, Serikali kuu kukosa mapato kwa miezi mitatu yanayotozwa kila jumatatu, jumatano na ijumaa huku wamiliki wa mashimo, vibarua na wafanyabiashara uchumi wao ukiyumba.
Waeleza mgogoro wao na John Gimunta
Kuwepo kwa mgogoro huo uliosababisha kukwama kwa shughuli za uzalishaji na ukusanyaji wa mapato kwa serikali , Novemba, 4, 2024, Mwandishi wa DIMA Online akafika Kijiji cha Tarani na kukutana na wachimbaji ili kufahamu nini chanzo cha shughuli ya uchimbaji kusimama na viroba vyenye mawe ya dhabau kusota bila kuuzwa .
Wanakikundi cha Peace Gold Mine wameeleza sababu za kugoma kuuza viroba vya mawe na kuomba serikali kuingilia kati ili wachimbaji wadogo waweze kufanya kazi vizuri kujiinua kiuchumi.
Nicolaus Matiko mwenye ulemavu wa viungo mchimbaji wa madini katika mgodi uliopo Kijiji cha Tarani amesema " Hapa tunakochimba kuna maduara 27, wanakikundi walikubaliana kutengeneza uongozi wa kikundi, baada ya kutengeneza uongozi tukamchagua mwanakikundi mwenzetu John Gimunta ashughulikie suala la leseni.
" Lakini akabadilisha jina tulilomtuma akashughulikie la Peace Gold Mine akatengeneza kikundi kingine ambacho sisi hatukijui. Kilichotushtua ni baada ya kuambiwa kwamba kuna kikundi kingine kinaitwa Tarani Mining Group kimeanzishwa hapa na Gimunta.
" Tulipomuuliza kwanini kafanya hivyo akasema sisi hatukumtuma, tukamwambia sisi tulichanga hela Tsh. Milioni 4 na wewe ukasema utachangia Milioni moja ziwe Milioni 5 tukakutuma ufuatilie leseni iweje uje utuambie kuwa leseni yetu imeshindikana ila imepatikana ya kwako tu ya Tarani Mining Group?
Anaongeza " Kilichofuata alikuja na watu wa madini akatutangazia kuwa yeye ndiye mmiliki wa eneo tunalolichimba kwa miaka mingi hivyo tunatakiwa kumpa asilimia 30 kati ya asilimia 100, yaani ukichimba viroba kumi vya mawe kati ya hivyo viroba vitatu umpatie Gimunta kama mapato ya mmiliki wa leseni.
" Wakati huohuo unatakiwa kulipa asilimia 0.03 kama ushuru wa halmashauri ya wilaya ya Butiama na mrabaha serikali kuu asilimia 0.07.
"Sisi tukakataa hatuwezi kumuuzia viroba kwa jina ambalo amelitengeneza yeye ambaye ametusaliti na kwenda kujitengenezea kikundi hewa binafsi ,hii ni mitaji ya wanakikundi na shughuli zote za uzalishaji ni za wanakikundi ndio imepelekea kuona viroba hivi vikisota hapa .Hivi viroba vina miezi mitatu ni zaidi ya viroba 10,000" amesema Nicolaus.
Laurence Chacha amesema " Nilianza kazi ya uchimbaji kwenye eneo hili tangu 2022, eneo hili lilikuwa wazi ambalo linamilikiwa na STAMICO. Tunachimba na tunalipa mapato halmashauri na serikali kuu na tumekuwa tukipewa risiti za mauzo na ofisi ya madini.
Mchimbaji Laurence Chacha akizungumza
" Gimunta alikuja hapa akiwa hana sehemu ya kuchimba mimi ndiye nilimpa eneo achimbe mwaka 2022 badala yake katufanyia ukatili, ana moyo wa ufisadi. Tuliandika malalamiko yetu ofisi ya madini, kwa Waziri wa madini, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mara hadi usalama wa Taifa tumepeleka hizi taarifa.
" Tuliomba wafuatilie wajue hiyo leseni upatikanaji wake ulikuwaje lakini hatujaona hatua zilizochukuliwa hata jumanne ya wiki hii tulienda kulalamika mkoani lakini hatukuona matokeo mazuri.Tunataabika sana familia zetu zinateseka kutokana na mgogoro huu.
" Rais Samia sisi ni wananchi wako tunakuhitaji sana uingilie mgogoro wetu utufikirie na sisi maana kuna watu wachache wasiowaaminifu wanaotaka kuondoa thamani yako , sisi hatupo kwaajili ya kuilalamikia serikali tunachohitaji ni haki wachimbaji wa maduala tunapata shida " amesema Laurence.
Joseph Golani amesema kuwa kumekuwa na ukiukwaji wa haki za wachimbaji pindi leseni zinapotolewa kwa watu kwa madai kuwa wachimbaji wa muda mrefu huwa hawatendewi haki na suala la ulipaji fidia limekuwa ni tatizo hususani wachimbaji wanaochimba katika eneo hilo kwa muda mrefu kisha watu kupatiwa leseni.
Fundi ujenzi wa mashimo ( maduara) Ayubu Mwita amesema kuwa mgomo huo umesababisha wakose malipo yao kwa wakati pindi wakamilishapo shughuli za ujenzi.
" John Gimunta ametufanya tuteseke , shughuli zimesimama kwa sababu yake uzalishaji hakuna kwasababu viroba vimesota . Serikali iwaangalie watu waliowekeza hapa kwa jicho la pili watu wanadai fedha zao na miradi imesimama kwasababu ya mtu mmoja" amesema Ayubu.
Mwendesha Bajaji Elias Julias amesema mgogoro umesababisha akose fedha" huu ni mwaka wangu wa sita katika biashara hii ya udereva hapa mgodini. Kazi yangu ni kubeba mizigo ya viroba vya mawe. Unatoka nyumbani ukijua unakuja kupata riziki unafika unakuta mzigo haujatoka shimoni.
Mwendesha Bajaji Elias Julias akieleza changamoto wanakopata baada ya mgomo wa uuzaji mawe yanayodhaniwa kuwa na dhahabu
" Hii kazi ndiyo inanifanya niishi nalisha familia, nalipa kodi , nina mkopo.Kabla ya mgogoro nilikuwa nasafirisha mizigo kwa siku napata 300,000- hadi 1000,000. Kwa sasa najikuta napata 25,000 ukitoa ya mafuta 10,000 nabaki na elfu 10,000 matumizi ni mengi haitoshi.
Ombi la CCM Tawi la Magunga
Sarurya Warioba ni Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Tawi la Magunga , ni fundi na mchimbaji aliyeanza kazi ya uchimbaji mwaka 2006 katika eneo hilo amewaomba viongozi wa CCM ngazi za juu kuingilia kati mgogoro huo.
" Tangu aingie huyu Gimunta tunateseka sana kama unavyoona Mwandishi wa habari nina maduara zaidi ya matatu ninayojenga.Tangu kutokea kwa mgogoro huu nimepata shida sana familia yangu inateseka inanitegemea mimi na mabosi wetu wanapata hasara na lawama maana shughuli imesimama wameshindwa kuzalisha mali ili waweze kulipa wafayakazi " amesema Sarurya .
Mwenyekiti wa Kikundi cha Peace Gold Mine Rhobi Mwita amesema " Kikundi cha Peace kimeanza Julai, 10, 2024 baada ya kuruhusiwa na serikali kwa kutoa utaratibu wa kisheria.
Mwenyekiti wa Kikundi cha Peace Gold Mine Rhobi Mwita akizungumzia mgogoro kati ya kikundi cha Peace Gold Mine na kikundi cha Tarani Mining Group
" Wanachama walipendeza watu wakufuatilia leseni wakamteua Gimunta afuatilie leseni, fedha zikachangwa Milioni 5 maana katika ufuatiliaji inahitaji chakula, malazi, usafiri kuzunguka huku na kule hadi kupata leseni lakini akatugeuka na kwenda kuchukua leseni yake binafsi badala ya kikundi" amesema.
Meneja Tarani Mining Group azungumza
Meneja wa Tarani Mining Group Peter Magere amesema hakuna mtu yeyote aliyezuiliwa kuuza viroba vya mawe ya dhahabu na kwamba Kikundi cha Peace Gold Mine wameanzisha mgogoro baada ya kikundi chao kupata leseni.
Meneja wa Tarani Mining Group Peter Magere akionesha stakabadhi za malipo za wachimbaji wanaouza mawe yanayodhaniwa kuwa na dhshabu
" Hakuna aliyezuiliwa kuuza viroba , ni baadhi ya watu ndio wamegoma wakiongozwa na Deo mbona kuna wengine kutoka Peace wanalipa kodi. Wameanzisha mgogoro baada ya kuona Tarani imepewa leseni" amesema Peter.
John Gimunta akanusha kupewa fedha
Mwenyekiti wa kikundi cha Tarani Mining Group na mwanzilishi wa kikundi hicho, John Gimunta amekanusha kuwa yeye si mwanachama wa Peace na wala hajawahi kupewa fedha zozote kufuatilia leseni ya Peace huku akisema kwamba kikundi chake kilianza mchakato mapema wa kuomba leseni kabla ya kikundi cha Peace.
" Mimi sikuwa mwanachama wa Peace Gold Mine na sitokuwa mwanachama kwasababu Peace ni kikundi ambacho hakijasajiliwa na hakitambuliki, ni kikundi cha usanii kimeanzisha mgogoro baada ya kuona Tarani imepata leseni pamoja na vikundi vingine ambavyo tuliomba navyo.
" Baada ya kupata leseni wao wanaona wangepata wao kwanza . Wao wanasema kikundi chao kimeanza Julai, 12, 2024 , sisi mchakato wa kutafuta leseni tumeanza mwezi wa tatu, 2024 na leseni tumepata mwezi wa nane. Mimi hawajawahi kunipa Milioni 5 ni waongo.
" Lile eneo lilikuwa linamilikiwa na STAMICO, lazima uwaombe kama unataka eneo la uchimbaji, wanaweza kukupa au wasikupe na ukiomba watakufuatilia na kama unasababu umezijengea hoja vizuri watakupatia. Kwahiyo sisi tulijenga hoja vizuri tukapata leseni mbili, Tugeme ikapata leseni mbili na Mwaga wa Samia leseni mbili" amesema John.
Ameongeza " Sisi hatuwaondoi kila mtu ana haki ya kuchimba ila wafuate utaratibu wa serikali, tozo za serikali zilipwe na mwenye leseni alipwe. Kama kuna changamoto waje tuongee lakini baadhi yao wakiongozwa na aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Irasanilo Deo ndiyo anawagomesha wachimbaji .
" Hatutozi asilimia 30 kwa 100, tunatoza asilimia 20 tu sawa na viroba viwili vya mawe. Wanagoma kuingia makubaliano, walishalalamika hadi kwa mkuu wa wilaya wameenda hadi mkoani lakini wameshindwa kuthibitisha kama waliwahi kuomba tume ya madini au STAMICO.
Kuhusu jina lake na saini kuwa kwenye mahudhulio ya kikundi cha Peace kilichojadili mchakato wa kufuatilia leseni amesema" Mimi nitakaaje kwenye kikao chao na si mwanachama? waligushi muhitasari wakaandika jina na saibi yangu.
Alipoulizwa kwanini ameanzisha kikundi wakati ni mwanachama wa Irasanilo amesema" Tumeanzisha kikundi ili kusaidia vijana waweze kujiajiri kwasababu Irasanilo inasuasua ilikuwa inaongozwa na Deo , bora vikundi viwepo viongeze ushindani.
Kuhusu kusajili Kikundi Wilayani Musoma na madai kuwa kikundi hicho ni kikundi hewa hakina wanachama amesema" Ni kweli nilisajilia Musoma na nilifanya hivyo tukiamini ofisi yetu itakuwa Musoma mimi nilianza shughuli za uchimbaji mwaka 2016, nimekuwa mchimbaji katika eneo nililopewa leseni tangu mwaka 2020.
" Kikundi chetu kimefuata taratibu zote za usajili sio kwamba ni kikundi changu binafsi na kina wanachama hao wanayosema ni kikundi hewa ni waongo" amesema John.
Kwamujibu wa kikundi cha Peace Gold Mine, kikundi hicho kimesajiliwa na kupewa namba ya usajili CBO/CD/BTM/093/2024.
Mchimbaji Alfred Nyamaroso amesema " Wanaoleta usumbufu ni Deo na ndugu zake ndio wanakigombanisha kikundi, hakuna anayetozwa viroba vitatu ni viwili tu, ni watu wanagomesha wengine kufanya shughuli zao" amesema Alfred.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa mgodi wa Irasanilo ambaye ni mwanachama wa Irasanilo na Peace Gold Mine, Deogratius Marwa amekanusha yanayosemwa na Gimunta na Meneja wa Tarani kwamba yeye ndio anawagomesha wachimbaji wasiuze viroba.
" Wale watu wameporwa haki zao sasa watawezaje kumuuzia au kumuunga mkono mtu aliyewapora , mbona kabla ya Tarani tulikuwa tunalipa kwa jina la Peace na hakuna mtu aliyelalamika kuonewa wala kutokea mgogoro wowote"
" Tulikutana na mkuu wa mkoa tukajadiliana na akasema mwenye leseni apewe asilimia 15 na sio asilimia 30, akamwagiza afisa madini mkoa kutafuta eneo lingine la uchimbaji kwaajili ya kikundi cha Peace Gold Mine na ametupatia wakala wa serikali kuandika makubaliano yetu , tunajua John Gimunta ametupora eneo lakini tumeamua kufuata ushauri wa mkuu wa mkoa. " amesema Deogratius.
Je nini kauli ya wanawake wachimbaji wa madini ya dhahabu Butiama, afisa madini mkazi mkoa wa Mara na mkuu wa mkoa wa Mara ?.
..........Itaendelea
Post a Comment