Home
/
HABARI KITAIFA
/
MGOGORO KATI YA PEACE GOLD MINE NA JOHN GIMUNTA ULIVYOWAIBUA WANAWAKE BUTIAMA
MGOGORO KATI YA PEACE GOLD MINE NA JOHN GIMUNTA ULIVYOWAIBUA WANAWAKE BUTIAMA
>> Ni baada ya viroba vya dhahabu kusota miezi mitatu bila kuuzwa
>>Wamuomba Rais Samia kutatua kero za wanawake
Na Dinna Maningo, Butiama
SIKU moja iliyopita DIMA Online imeripoti habari yenye kichwa cha habari kisemacho 'MGOGORO KATI YA PEACE GOLD MINE BUTIAMA NA JOHN GIMUNTA WAIKOSESHA SERIKALI MAPATO'.
Chombo hiki cha Habari kiliripoti kwamba, zaidi ya Viroba elfu kumi vya mawe yanayodhaniwa kuwa na dhahabu vya wachimbaji wadogo wa dhahabu kikundi cha Peace Gold Mine, vimesota miezi mitatu bila kuuzwa kutokana na kuibuka mgogoro wa kimaslahi baina yao na mchimbaji John Gimunta .
Wachimbaji hao wenye mashimo (maduara ) katika mgodi wa dhahabu wa wachimbaji wadogo uliopo Kijiji cha Magunga maarufu mgodi wa Buhemba, katika Kata ya Mirwa wilaya ya Butiama, mkoani Mara maarufu mgodi wa Buhemba, wameshindwa kuuza viroba vyao.
Baadhi ya mifuko yenye mawe yanayodhaniwa kuwa na dhahabu ikiwa imesota miezi mitatu kutokana na mgogoro uliopo kati ya kikundi cha Peace Gold Mine na John Gimunta wa kikundi cha Tarani Mining Group.
Ni baada ya kugoma kulipa tozo asilimia 30 kwa kikundi cha Tarani Mining Group kilichopatiwa leseni miezi miwili iliyopita kama mmiliki wa leseni ya uchimbaji katika eneo hilo, kikundi ambacho mwanzilishi wake ni John Gimunta na hivyo serikali kukosa mapato huku uchumi wa wachimbaji, wafanyabiashara ukiyumba.
Pia wanakikundi hao wamesema kuwa wameshindwa kulipa asilimia hizo kwakuwa John Gimunta aliwasaliti baaada ya kuchanga fedha Tsh. Milioni 5 na kumpatia kwa ajili ya malazi, nauli, chakula, ufuatiliaji ili wapate leseni ya uchimbaji ya kikundi.
Baadhi ya mifuko yenye mawe yanayodhaniwa kuwa na dhahabu ikiwa imesota miezi mitatu kutokana na mgogoro uliopo kati ya kikundi cha Peace Gold Mine na John Gimunta wa kikundi cha Tarani Mining Group
Wanakikundi wamesema kuwa Gimunta amewasaliti na kujipatia leseni yake binafsi inayotambulika kwa jina la Tarani Mining Group badala ya leseni iliyotakiwa kutambulika kwa jina la kikundi cha Peace Mining Group.
Kuwepo kwa mgogoro huo umewaibua wanawake wa kikundi hicho cha Peace Gold Mine wakieleza changamoto wanazozipata.
Pia wanamuomba mwanamke mwenzao Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kuingilia kati mgogoro huo ili kuwanusuru wanawake ambao waliamua kuwa wachimbaji wa madini ili kujiinua kiuchumi.
Baadhi ya wanakikundi akiwemo Rebecca Mnanka amesema " Tumechimba hapa kwa miaka mingi, hivi karibuni watu wa madini walikuja wakapima wakasema hili eneo halipo Kijiji cha Magunga msiwape Magunga mapato kwakuwa eneo lipo Kijiji cha Tarani. Wakatuambia tuchague viongozi wakatuchagulia na jina la kikundi.
" Huwa wanakuja wanakata kodi yao wanatupatia risiti wanaandika On Process, wakatuambia harakisheni mkate leseni tukakubaliana tulichoambiwa tukaanza mchakato ili kikundi kipate leseni wakati huo tukiendelea na shughuli za uchimbaji.
"Tukachangishana fedha Milioni 5 tukampa mwanakikundi mwenzetu John Gimunta kwakuwa tulimwona ni mwelewa afuatilie tupate leseni yeye akaenda akabadilisha jina ,tukashangaa anasema tumpe asilimia 30 wakati alipaswa kuleta leseni ya Peace Gold.
Rebecca Mnanka Mchimbaji wa madini ya dhahabu mgodi uliopo Kijiji cha Talani - Butiama akionesha viroba vilivyosota miezi mitatu bila kuuzwa kutokana na mgogoro
" Hivi viroba unavyoviona tunazalisha kwa pesa za kukopa ,tukifanya kazi tunalipa watu lakini mwenye pesa zake ameamua kutunyanyasa . Tunamuomba Rais Samia atuangalie kwa jicho la pili. Wanawake tunatafuta kwa mikono yetu tunachukua pesa za watu tunawekeza mwishoni wa siku tunaambiwa sisi hatuna haki Serikali itusaidie." amesema.
Ester Mnanka mjane ambaye anafanya biashara ya kuuza chakula ( Mama ntilie) amesema " Rais Samia wewe ni mama kama mimi tusaidie wanawake wenzako. Mimi ni mama ntilie, mgogoro umesababisha baadhi ya kazi zisimame nateseka sana maana pesa nayofanyia kazi ni ya kukopa.
" Huu Mgogoro tangu utokee hakuna kiongozi wa serikali kutoka wilayani wala mkoani waliofika hapa kusikiliza kero zetu zaidi ya wachimbaji wachache kuwafuata kwenye ofisi zao.
" Walipaswa kufika eneo la mgogoro watatue shida zetu sio kukaa ofisini wameajiriwa ili watutumikie sisi wananchi wao wanasubiri wafuatwe kwenye ofisi zao badala ya kufika moja kwa moja kutatua migogoro ya wachimbaji. Rais tusaidie akina mama tupate leseni" amesema.
Pili Mhagachi amesema " Unaona hili duara ni langu na hawa vijana wanaotoa mawe shimoni juzi walinikaba walitaka niwalipe pesa zao nikasema sina hela, hii Kompresa nilikodi Tsh. Milioni 4 .
" Sisi wanawake ndio tunaongoza nchi kwanini tena ifike sehemu wanawake tunyanyaswe ? Rais Samia tusaidie tutakufa kwa presha" amesema Pili.
Mchimbaji Ngoro Machera amesema " Niko hapa tangu 2016, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tetea hawa vijana wengine ni mayatima, wengine walitoka kwenye matendo ya ujambazi wapo hapa wanatafuta riziki lakini mgogoro umesababisha wakose riziki.
" Rais Samia tetea wajane ,tetea yatima , kuna watu wanauguza wagonjwa hospitali hawana ndugu na mizigo ndiyo hii imeshindwa kuuzwa , watu tutafungwa tusipopeleka pesa za mikopo.Tamaa za John Gimunta zimepelekea sisi yatima tunyanyasike . Samia sikiliza kilio chetu tunaenda kwenye kampeni ni pesa zitatumika " amesema Ngoro.
Monica Sospiter anajishughulisha na biashara ya kuuza ndizi katika migodi ya wachimbaji wadogo iliyopo kata ya Mirwa amesema baada ya Viroba kutouzwa kwa kipindi cha miezi mitatu biashara imekuwa mbaya huku wateja ambao ni wachimbaji wanapokula ndizi hawalipi fedha wanaishia kukopa kwakuwa uzalishaji umesimama.
" Nina miaka 6 katika biashara ya ndizi , mimi sina mme, Biashara yangu ya ndizi ndio mme wangu. Kiukweli hali ya biashara kwa sasa ni mbaya sana, kabla ya mgogoro huu nilikuwa nauza ndizi ndani ya saa chache zimeisha, napata pesa inanisaidia kuendesha maisha na wanangu.
" Lakini kwa sasa siku inaisha hujauza ndizi unarudisha nyumbani zinaoza wakati mwingine inabidi uishie kukopesha tu, malipo yanakuwa shida kwasababu ya huu mgogoro wa Peace na John Gimunta " amesema Monica.
Lucy Joseph amesema " Mizigo mnayoiona ni pesa yangu imelala hapa , ni pesa ambayo nimeikopa benki kwa ajili ya kupambana na familia yangu na serikali ipate mapato. Nanunua viroba vya mawe naenda kutengeneza vifusi nalipa mapato serikalini mimi ni kota.
" Rais Samia unasema akina mama lazima tuwe mbele tusishindwe, mama yetu na sisi tukasema hatutashindwa ngoja tushikane mikono akina mama ili wajue na sisi tunaweza lakini kaja Gimunta katuathiri sisi akina mama " amesema .
Ester Machuche ambaye ni mjane amesema alianza shughuli ya uchimbaji mwaka 2016 na kwamba eneo hilo amekuwa akichimba kwa miaka mingi " Nimezalisha viroba 300 vipo hapa vimesota. Sisi tuliochimba kwa miaka mingi katika eneo hili ndio tulipaswa tupewe leseni, kwakuwa kikundi chetu kilikuwa katika mchakato tungezingatiwa sisi.
Mchimbaji Ester Machuche akionesha viroba vilivyosota miezi mitatu bila kuuzwa kutokana na mgogoro baina ya kikundi cha Peace Gold Mine na Talani Mining Group
" Kama tulikuwa hatujui taratibu ilikuwa ni kazi ya afisa madini mkoa wa Mara kutuelimisha maana ni sehemu ya kazi yake kutushauri sisi wachimbaji wadogo wadogo ambao baadhi yetu hatukubahatika kwenda shule. Serikali ijue inaongoza watu waliosoma na wasiosoma, ambao hawakusoma nao wanastahili kutendewa haki.
"Hii miti mnayoiona imekuwa mikubwa tulishauriwa na watu wa madini tupande alafu leo wanampa leseni mtu aliyekuja hivi karibuni wanatuacha sisi wa siku nyingi wanampa mtu anayesema ana kikundi ambacho hakina wanachama" amesema Ester.
Katibu wa kikundi cha Peace Gold Mine Rosemary Emanuel amesema kikundi kimesajiliwa na kupewa namba ya usajili CBO/CD/BTM/093/2024. Kina wanachama 102 na kwamba wameanza kuchimba katika eneo hilo la madini Kijiji cha Tarani mwaka 2022.
Amesema kutokana na mgogoro kati ya kikundi na John Gimunta, Septemba, 23, 2024 walimwandikia barua Afisa madini mkazi mkoa wa Mara na Wizara ya Madini Dodoma ya malalamiko yawanakikundi dhidi ya John Gimunta kwenda ofisi ya madini mkoa wa Mara.
Pia alionesha barua ya tarehe 12, Julai, 2024 iliyokuwa na ajenda ikiwemo ya uchaguzi wa viongozi , kufuatilia upataji wa leseni na mahudhulio yanayothibitisha kuwa Gimunta ni mwanachama wa Peace Gold Mine aliyewasaliti.
" Tuliandika barua na kuziwasilisha mkoani, wizara ya madini tukieleza malalamiko na ombi la kuzuia leseni ya uchimbaji ya Tarani Mining Group. Awali Julai, 10, 2024 ofisi ya madini ilifika eneo tunalofanyia kazi na kusimamia zoezi la kupata uongozi wa muda utakaoshughulikia mchakato wa kupewa leseni" amesema Rosemary.
Ameendelea kusema " Wakati huo tuliendelea kufanya shughuli za uchimbaji na kulipa tozo za serikali kwa kutumia jina la kikundi Peace Gold Mine huku taarifa ya ulipaji tozo kutoka ofisi ya madini zikionesha kikundi chetu kipi kwenye mchakato wa kupewa leseni ' License on Process ' maana yake ofisi ya madini inafahamu kuwa kikundi chetu kilishaanza mchakato wa leseni.
" Tarehe 12, 7, 2024 tulikaa kikao na kumteua John Gimunta kama mwanakikundi mwenzetu kwa ajili ya kufuatilia shughuli zote za upatikanaji wa leseni. Wanakikundi tukachanga fedha Milioni 4 , yeye anaongeza Milioni moja zikawa Milioni 5.
" Gimunta alisema yeye ndiye anafahamiana na viongozi ngazi za juu tukimwezesha fedha atafuatilia kwa haraka na tutapata leseni. Tulimpatia pesa mkononi hatukumsainisha wala kumpatia risiti ya malipo.
" Tulifanya hivyo kwakuwa tulimwamini , mara nyingi sisi wachimbaji huwa tunafanya kazi kwa kuaminiana tunapeana fedha au kukopeshana bila hata kuandikishiana " amesema Rosemary.
Ameongeza kusema "Alituzunguka badala ya kuomba leseni kwa jina la kikundi la Peace Gold Mine akaomba leseni yake binafsi kwa jina la Tarani Mining Group na kikundi kimesajiliwa Musoma wakati anafanya shughuli za uchimbaji wilaya ya Butiama hatuna uhakika kama hicho kikundi kina wanachama au ni kikundi hewa." amesema
Ameongeza kuwa wakati wakisubiri mrejesho wa ufuatiliaji wa leseni, tarehe 2/9/2024 Gimunta akiwa ameambatana na maofisa wa madini waliwataarifu wachimbaji katika eneo linalochimbwa na wanakikundi cha Peace kuwa eneo hilo wanalolifanyia kazi leseni amepewa Tarani Mining Group.
" Wakasema kwamba kuna asilimia ya uzalishaji ambayo ni asilimia 30 kati ya asilimia 100 ya uzalishaji, yaani kama umetoa viroba 10 vya mawe unatakiwa kumpa viroba vitatu, ambapo kwa upande wa Halmashauri tozo ni sh. asilimia 0.03 na serikali kuu unalipa tozo asilimia 0.07 " amesema Rosemary.
Hata hivyo Meneja wa Tarani Mining Group Peter Magere amesema hakuna mtu yeyote aliyezuiliwa kuuza viroba vya mawe ya dhahabu na kwamba Kikundi cha Peace Gold Mine wameanzisha mgogoro baada ya kikundi chao kupata leseni.
Meneja wa Tarani Mining Group Peter Magere akionesha stakabadhi za malipo kwa wachimbaji wanaouza viroba vinavyodhaniwa kuwa na dhahabu
Mwenyekiti wa kikundi cha Tarani Mining Group na mwanzilishi wa kikundi hicho, John Gimunta amekanusha kuwa yeye si mwanachama wa Peace na wala hajawahi kupewa fedha zozote kufuatilia leseni ya Peace.
John amesema kwamba kikundi chake kilianza mchakato mapema wa kuomba leseni kabla ya kikundi cha Peace huku akionesha baadhi ya vielelezo na kueleza kuwa alifuata taratibu zote ambapo kikundi hicho kilisajiliwa halmashauri ya wilaya ya Musoma.
" Mimi sikuwa mwanachama wa Peace Gold Mine na sitokuwa mwanachama kwasababu Peace ni kikundi ambacho hakijasajiliwa na hakitambuliki, ni kikundi cha usanii kimeanzisha mgogoro baada ya kuona Tarani imepata leseni pamoja na vikundi vingine ambavyo tuliomba navyo.
" Baada ya kupata leseni wao wanaona wangepata wao kwanza . Wao wanasema kikundi chao kimeanza Julai, 12, 2024 , sisi mchakato wa kutafuta leseni tumeanza mwezi wa tatu, 2024 na leseni tumepata mwezi wa nane. Mimi hawajawahi kunipa Milioni 5 ni waongo.
Kikundi cha Peace Gold Mine kimesajiliwa wilayani Butiama na kupewa namba ya usajili CBO/CD/BTM/093/2024 na kikundi cha Tarani Mining Group kilisajiliwa Musoma na kupewa namba za usajili HMM/USJ/VK/0480.
>> Rejea
Kwa mujibu wa Tovuti ya Tume ya Madini, Katibu mkuu wa Tume ya Madini Mhandisi Yahaya Samamba, alisema kuwa Serikali kupitia Tume ya Madini itaendelea kuweka mazingira mazuri kwa wachimbaji wadogo wa madini nchini.
Alisema hayo Machi, 18, 2024 katika kikao cha sita cha Baraza la wafanyakazi wa Tume ya Madini kilichofanyika Dodoma. Pia Tume hiyo itaendelea kuweka mkakati wa kuhakikisha mchango wa kwenye sekta ya madini unaendelea kujua sambamba na kuzidisha ajira zaidi.
Mhandisi Yahaya aliongeza kuwa mchango wa wachimbaji wadogo kwenye mapato yatokanayo na sekta ya madini imeendelea kukua kutoka asilimia tano hadi asilimia 40 mwaka 2023.
Je mkuu wa mkoa wa Mara, Afisa Madini mkazi mkoa wa Mara wanasema nini juu ya mgogoro huo ?
.......... Itaendelea
Baadhi ya vielelezo vya kikundi cha Peace Gold Mine
Moja ya stakabadhi ya malipo ya Peace Gold Mine
Muhitasari wa kikao cha wanachama wa Peace Gold Mine kilichoketi tarehe 12, 7, 2024 kikiwa na ajenda ya uchaguzi wa viongozi, kufuatilia leseniBarua ya malalamiko kupewa leseni kwa kikundi cha Tarani Mining Group na ombi la kuzuia leseni ya chama hicho ya tarehe 23,9,2024 iliyotumwa kwa Mwenyekiti Tume ya Madini Tanzania- Dodoma, nakala kwa Waziri wa Madini, Wizara ya Madini na Afisa madini mkazi Mara.
Cheti cha Talani Mining Group kilichosajiliwa katika Halmashauri ya Manispaa ya Musoma cha tarehe 2,10,2022 chenye usajili HMM/USAJ/VK/9480
Barua ya maombi ya kikundi cha Tarani Mining Group kupewa eneo la kuchimba madini ya dhahabu katika eneo la Buhemba wilaya ya Tarime ya tarehe 8/3/2024
Post a Comment