MGANGA MKUU TARIME APIGA MARUFUKU WAJAWAZITO KULIPA TSH. LAKI TATU KUFANYIWA UPASUAJI
>>Dkt. Amin Vasomana amesema upasuaji kwa wajawazito ni bure
>>Awataka wajawazito kwenda hospitali badala ya kwenda kwa wakunga wa jadi
>>Atoa namba zake za simu wajawazito watakaoombwa fedha wampigie simu
Na Dinna Maningo, Tarime
MGANGA Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, mkoani Mara, Amin Vasomana, amepiga marufuku wajawazito kutozwa fedha ili kujifungua na kufanyiwa upasuaji wanapofika kupata huduma katika hospitali, vituo vya afya na zahanati za serikali
Amesema huduma kwa wajawazito ni bure hivyo watoa huduma hawapaswi kuwaomba gharama zozote na kwamba mtumishi yeyote atakayebainika kumwomba mjamzito fedha ili kumzalisha au Tsh. 300,000 ili amfanyie upasuaji hatosita kuwachukulia hatua.
Dkt. Amin amepiga marufuku hiyo baada ya wanawake toka kata mbalimbali katika Halmashauri hiyo kulalamika mbele yake kuwa wajawazito wamekuwa wakitozwa Tsh. 300,000 kufanyiwa upasuaji na wengine Tsh. 30,000- 50,000 wanapojifungua kawaida.
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, mkoani Mara, Amin Vasomana akizungumza na wananchi juzi wakati wa uzinduzi wa kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia, uliofanyika Nyqmongo- Tarime
Wanawake wameyasema hayo wakati mganga huyo akitoa elimu ya madhara ya ukeketaji kiafya katika uzinduzi wa siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia uliofanyika Novemba, 25, 2024, katika viwanja vya Nyamongo sekondari kwa ufadhili wa mgodi wa dhahabu wa Barrick North Mara.
Dkt. Amin akiwa anatoa elimu ya madhara ya ukeketaji na afya ya uzazi aliwaomba wananchi hususani wanawake kutokwenda kujifungua kwa wakunga wa jadi kwani ni hatari kwao na mtoto atakayezaliwa.
Amesema kuwa hivi karibuni limetokea tukio la mjamzito kupoteza maisha baada ya kwenda kuzalishwa na mkunga wa jadi. Amewapiga marufuku wakunga wa jadi kwasababu wanasababisha vifo.
" Hivi karibuni tulipata kifo kilichotokea maeneo ya Sirari, mjamzito mwenye zao ya nne aliogopa kwenda kujifungua hospitali kufanyiwa upasuaji baada ya kufanyiwa upasuaji mimba ya nne hivyo alipopata mimba ya tano akaenda kwa mkunga kuzalishwa ikashindikana akapoteza maisha.
"Hiki ni kifo cha nne kutokea tangu Januari hadi sasa mwaka huu. Kati ya hivyo vifo viwili vya wajawazito vimetokea kwenye jamii kimoja kikihusisha mkunga wa jadi na vifo viwili vimetokea hospitali kwa sababu mbalimbali" amesema Amin.
Ameongeza " Matukio hayo yanapotokea hakuna ushirikiano wanawaficha wakunga hawasemi lakini pia wanaokumbwa na matatizo hawasemi wanaficha. Hatutamani wakunga wa jadi kufanya kazi hiyo Mama mwenye mimba nne au mwenye kovu la upasuaji ni lazima ajifungulie kituo cha afya au hospitali "Amesema Dkt. Amin.
Baada ya mganga huyo kuzuia wakunga wa jadi kuzalisha wajawazito zikasikika sauti za akina mama wakisema " Dkt. watu wanaenda kwa wakunga wa jadi kwasababu wanashindwa kumudu gharama hospitali za serikali. Ili ufanyiwe upasuaji unalipa 300,000 usipotoa hawakufanyii.
"Ukijifungua kawaida unaorodheshewa vitu vingi vya kununua, elfu 50 zinakutoka. Mara wembe , mara grovisi, sindano, madawa ndio maana watu wanaenda kwa wakunga wa jadi wao ni bei rahisi " zilisikika sauti za kina mama.
Dk. Amin akawaambia kuwa huduma ya upasuaji kwa mjamzito ni bure na wanaotoza Tsh. 300,000 wanafanya makosa kisha akatoa namba zake za simu na kuwaomba wampigie simu endapo mjamzito akitozwa fedha kiasi hicho kufanyiwa upasuaji.
Wanawake wakiwa katika uzinduzi wa siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia uliofanyika Nyamongo- Tarime
"Kuna baadhi ya vifaa kama vile grovis, wembe , kanga za kutumia. Hivi unashauriwa kwenda navyo kwa tahadhari maana unaweza kujifungua hata kabla hujafika chumba cha kujifungulia, ukiwa navyo vinasaidia wewe kupata huduma haraka.
" Kuhusu laki tatu wanaofanya hivyo ni makosa nikiwabaini ntawachukulia hatua. Hauruhusiwi kumtoza mjamzito fedha ili ajifungue. Atakaye kuomba laki tatu ili ufanyiwe upasuaji nipigieni simu nawapa namba zangu za simu ni 0753580425 nipigieni.
"Ukinipigia mtaje kwa jina na hiyo hospitali au zahanati ulikopata huduma, ukiniambia nitatunza siri, nitafika nitachukua hatua ili tukomeshe vitendo hivi. Haiwezekani serikali itoe huduma bure alafu baadhi ya watumishi wawaombe fedha" amesema Dkt. Amin.
Baada ya Dkt. kusema hivyo zikasikika sauti za akina mama zikisema " Ukienda na vifaa vyako wanavikataa wanakuomba hela wakuletee vifaa wenyewe, na vifaa vinavyobaki havijatumika wanavichukua " zilisikika sauti za akina mama.
Hata hivyo baadhi ya vituo vya afya vinavyotajwa kutoza gharama ya 300,000 kwa wajawazito wanaofanyiwa upasuaji ni pamoja na Kituo cha afya Sirari, Nyangoto na Nyarwana.
Post a Comment