WANANCHI WA KITONGOJI CHA KINYARIRI WAIOMBA SERIKALI KUSAJILI SHULE SHIKIZI
Na Jovina Massano, Mara
KATIKA kuhakikisha maradhi ujinga yanatokomezwa, wananchi wa kitongiji cha Kinyariri, kijiji cha Mesaga wilayani Serengeti mkoani Mara wameiomba serikali kuisajili na kuifungua shule shikizi iliyojengwa kwa nguvu ya wananchi na serikali.
Wananchi hao ambao tayari wameishajenga vyumba vya madarasa vinne ambapo vyumba viwili vimeishaezekwa na viwili vipo kwenye hatua ya uezekaji, wameomba pia wadau na viongozi kuwaunga mkono katika ukamilishaji wa kupaua.
Nchota Magoge Mung'ahu ameeleza kuwa baada ya kuona watoto wao wanatembea umbali wa kilomita zaidi ya kumi katika shule mama ya Mesaga na njiani wakikumbana na wanyama wakali na kupelekea watoto wao kuchelewa na kushindwa kufika shule na hata kukatisha masomo wakaona ni vema Sasa kuwa na shule karibu itakayosaidia kuondoa changamoto hiyo.
"Watoto wetu wanatakiwa kuwahi namba shuleni lakini njiani wanakutana na tembo wakiwemo fisi lakini pia umbali wanachoka kutokana na adha hizo zinapelekea Idadi kubwa ya watoto kushindwa na kuacha shule kabisa," amesema Nchota.
Mbali na changamoto hizo shule hiyo shikizi ambayo serikali imeweza kujenga madarasa mawili na ofisi moja kwa fedha za Uviko kiasi cha Tsh Milioni hamsini (50,000,000/=) zilitolewa na kuongezewa zingine Tsh. Milioni kumi na moja (11,000,000/=).
Fedha hizo zilitolewa kujenga matundu ya vyoo yapatayo kumi(10) lakini mpaka sasa bado shimo lake halijamalizika kujengwa kutokana na upotevu wa vifaa vya ujenzi.
Katibu wa kamati ya maendeleo ya Kinyariri, Masiko Isore Masiko amesema usimamizi wa ujenzi huo ulikuwa chini ya Mwalimu mkuu na viongozi wa Elimu wilaya na kwamba wananchi wamejitahidi kutoa michango vikiwemo viashiria ili kuharakisha ujenzi huo lakini umesimama kutokana na sababu za ubadhilifu uliofanywa na msimamizi.
"Ujenzi huu ulikuwa chini ya Mwalimu mkuu wa shule mama ya Mesaga ambae kwa Sasa ameishastaafu hivyo hatujui ukamilishaji huu utafanyika lini,"amesema Masiko.
Mbali na changamoto hiyo hivi sasa Mbunge wa Jimbo hilo la Serengeti ametoa kiasi cha Tsh. Milioni moja na laki Saba(1,700,000/=) kwa ajili ya bati za kuezekea vyumba viwili vya madarasa ambavyo vimefikia hatua ya umaliziaji na kuwa na jumla ya vyumba vya madarasa sita vitakavyosaidia kupokea watoto kwa wingi.
Maboma ya madarasa mawili yaliyojengwa na Wananchi wa kitongoji cha Kinyariri na nyumba ya kuishi Mwalimu
Sambamba na Ujenzi huo wa vyumba vya madarasa lakini pia wananchi hao wameanza kujenga nyumba ya Mwalimu ambayo tayari imefikia kwenye renta.
Wamewaomba wadau wa maendeleo kusaidia kuongeza nguvu ili kukamilisha nyumba hiyo kwa wakati kabla ya Januari 2025.
Mwenyekiti wa kamati ya maendeleo ya wazee Moses Machota ameiomba serikali kuipa usajili shule hiyo ili watoto wa eneo hilo waweze kupata masomo yao karibu na kuweza kuondoa wasiojua kusoma na kuandika katika jamii hiyo.
Jengo lililojengwa n serikali pamoja na jengo lililojengwa na Wananchi kitongoji cha Kinyariri
Ameongeza kuwa wazee wa kitongoji hicho wanatambua umuhumu wa Elimu kwa jamii yao wakaamu kuwanusuru watoto wao ili wasiache masomo na kuandaa Taifa lililo bora.
Akizungumza na DIMA ONLINE, Afisa elimu divisheni ya awali na msingi wilaya ya Serengeti, Mujibu Mustapha Babara amekiri uwepo wa changamoto ya kutokamilika kwa shimo la choo na ukamilishaji wa vyumba viwili vya madarasa pamoja na nyumba ya kuishi Mwalimu katika shule hiyo.
Amefafanua kuwa uanzishwaji wa shule hiyo shikizi katika kitongoji hicho walianzisha wananchi wenyewe kwa kujenga vyumba viwili vya madarasa kutokana na changamoto ya umbali.
Mbali na uchangiaji huo wa serikali utaratibu wa kuisajili shule kwa hatua za awali umefanyika ambapo hadi sasa masomo kwa wanafunzi wa awali yanaendelea.
" Lakini pia ili usajili ukamilike inatakiwa kuwe na vyumba sita vya madarasa na hivi sasa tayari kuna vyumba vinne vilivyokamilika na viwili vipo hatua ya ukamilishaji hivyo amewataka wananchi wa kitongoji hicho kusogeza viashiria ili zoezi liweze kukamilika kabla ya Januari 2025.
"Kuhusu shimo la choo kutokamilika kwa wakati shimo lililochimbwa lilikuwa kubwa tofauti na fedha iliyoletwa kwa hiyo wao walitakiwa warudi kwenye kijiji wachange vile vitu vikamilike walipochelewa vifaa vilivyokuwepo vikaibiwa ambavyo ni mifuko sita ya saruji na nondo saba.
" Tulimbana msimamizi ambapo ameusharudisha mifuko ya saruji minne na nondo atarudisha,na makisio yaliyofanyika jamii inatakiwa kuchangia Tsh. Milioni mbili ili iweze kukamilika na wanatakiwa wakamilishe vyumba hivyo viwili na nyumba hiyo haraka ili isajiliwe rasmi kabla ya shule kufunguliwa,"amesema Mujibu.
Amesema baada ya likizo kuisha shule hiyo itapata Mwalimu alieajiliwa pia ni mojawapo ya shule nne zilizo kwenye hatua ya usajili ambazo ni Kwilengo iliyopo Kata ya Sedeko,Marakop Kata ya Manchira, Kinyariri na kwamba wilaya ya Serengeti ina shule shikizi 24 lakini Shule ambazo zipo kwenye kiwango cha kusajiliwa ni hizo nne.
Post a Comment