HEADER AD

HEADER AD

RC PWANI, WANANCHI WAPIGA KURA UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA


Na Gustaphu Haule, Pwani

Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amewaongoza wakazi wa mkoa wa Pwani kupiga kura kwa ajili ya kuwachagua viongozi wa serikali za mitaa watakaokaa madarakani kwa muda wa miaka mitano ijayo.

Kunenge pamoja na wananchi Novemba, 25, 2024 majira ya saa 2:15 asubuhi wamepiga kura katika Mtaa wa Mkoani "A" uliopo Kata ya Tumbi  Halmashauri ya Kibaha Mjini ambapo pamoja na mambo mengine ameeleza kuwa hali ya Mkoa wa Pwani kiusalama ipo shwari.

         Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge akipiga kura katika kituo cha Mkoani "A" kilichopo Kata ya Tumbi Kibaha Mjini.

Amesema uchaguzi huo ni muhimu kwani unakwenda kutoa viongozi ambao watahudumia Wananchi kwa ukaribu zaidi kwa ajili kuleta maendeleo hivyo ni vyema kila mwananchi ajitokeza kutimiza haki yake ya kikatiba.

Amesema muda wa kupiga kura ni kuanzia saa 2 asubuhi mpaka saa 10 jioni na kwamba muda ukimalizika watu waliopo katika foleni wote watapiga kura bila usumbufu wowote.

     Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge wa nane kutoka mbele akiwa katika foleni ya kupiga kura leo Novemba 27 katika kituo cha Mkoani A kilichopo Kata ya Tumbi Kibaha Mjini


"Nawaomba wakazi wa mkoa wa Pwani wajitokeze kupiga kura kwani inachukua dakika moja au tatu na hii itakufanya wewe mwananchi kutimiza haki yako ya kikatiba ya kuchagua kiongozi wako wa Mtaa ,"amesema Kunenge 

Kunenge ameongeza kuwa serikali ya mkoa imejipanga vizuri kusimamia uchaguzi kwani vyombo vyote vya usalama vipo kila sehemu huku akiwahakikishia Wananchi waende kupiga kura wakiwa na amani kwani vituo vipo salama.

Hatahivyo, Kunenge amemshukuru Rais wa awamu ya sita Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuona umuhimu wa siku ya kupiga kura kwa kufanya maamuzi sahihi ya  kuweka mapumziko ili kila mmoja ashiriki kupiga kura.

     Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge wa sita kutoka mbele akiwa katika foleni ya kupiga kura leo Novemba 27 katika kituo cha Mkoani A kilichopo Kata ya Tumbi Kibaha Mjini.

"Maamuzi ya Rais Samia ni mazuri kwani yamesaidia kutoa fursa kwa Wananchi kutimiza haki yake ya kupiga kura hivyo ni vyema Wananchi wote kwa pamoja wakaungana na Rais Samia katika kuhakikisha adhma ya kuweka mapumziko siku ya leo inatimia", amesema Kunenge.


Mmoja wa Wananchi akipiga kura katika kituo cha Mkoani A kuwachagua viongozi wa Serikali ya Mtaa.

No comments