RC MARA AINGILIA KATI MGOGORO KIKUNDI CHA PEACE GOLD MINE NA JOHN GIMUNTA
>>Azungumza na wachimbaji kutafuta Suluhu
>>Afisa Madini Mara asema yeye anasimamia sheria
>> Utoaji wa leseni kwa vikundi kadhaa mgodi wa Buhemba ni dalili ya kukiua kikundi mama cha Irasanilo ?
Na Dinna Maningo, Musoma
KUMEKUWEPO mgogoro kati ya kikundi cha uchimbaji wa madini ya dhahabu cha Peace Gold Mine na mmiliki wa leseni John Gimunta ambaye ni Mwenyekiti na mwanzilishi wa kikundi cha Tarani Mining Group.
Vikundi hivyo vinafanya shughuli za uchimbaji katika mgodi wa dhahabu uliopo Kijiji cha Magunga, Kata ya Mirwa wilayani Butiama, mkoa wa Mara, ambao umepelekea viroba zaidi ya elfu 10 vinavyodhaniwa kuwa na dhahabu kusota bila kuuzwa.
November, 8 , 2024 katika chombo hiki cha Habari iliripotiwa habari yenye kichwa cha habari isemayo 'Mgogoro kati ya Peace Gold Mine Butiama na John Gimunta waikosesha serikali mapato'.
Viroba vyenye mawe yanayodhaniwa kuwa na dhahabu vikiwa vimesota miezi mitatu bila kuuzwa
Wanakikundi cha Peace Gold Mine wameiambia DIMA Online kuwa wameshindwa kumlipa John Gimunta asilimia 30 ya uzalishaji kwakuwa aliwasaliti baaada ya kuchanga fedha Tsh. Milioni 5 na kumpatia ambaye ni mwanakikundi mwenzao kwa ajili ya malazi, nauli, chakula, ufuatiliaji ili wapate leseni ya uchimbaji ya kikundi.
Wamesema kuwa John amewasaliti na kujipatia leseni yake binafsi inayotambulika kwa jina la Tarani Mining Group badala ya leseni iliyotakiwa kutambulika kwa jina la kikundi cha Peace Mining Group.
Mgogoro huo umepelekea halmashauri ya wilaya ya Butiama kukosa kodi asilimia 0.03 ya mapato ya wachimbaji na Mrabaha, serikali kuu asilimia 0.07 kwa miezi mitatu yanayotozwa kila jumatatu, jumatano na ijumaa huku wamiliki wa mashimo, vibarua na wafanyabiashara uchumi wao ukiyumba.
November, 9, 2024 chombo hiki kiliripoti habari yenye kichwa cha habari kisemacho Mgogoro kati ya Peace Gold Mine na John Gimunta ulivyowaibua wanawake Butiama.
Baadhi ya Wanawake ambao ni wachimbaji wa madini ya dhahabu kikundi cha Peace Gold Mine wakitoa malalamiko yao wakati DIMA Online ilipofika mgodi wa Buhemba
Kuwepo kwa mgogoro huo umewaibua wanawake wa kikundi hicho cha Peace Gold Mine wakieleza changamoto wanazozipata huku wakimuomba mwanamke mwenzao Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kuingilia kati mgogoro huo ili kuwanusuru wanawake ambao waliamua kuwa wachimbaji wa madini ili kujiinua kiuchumi.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa kikundi cha Tarani Mining Group, John Gimunta amekanusha kuwa yeye si mwanachama wa Peace na wala hajawahi kupewa fedha zozote kufuatilia leseni ya Peace na kwamba tozo inayotozwa ni asilimia 20 na siyo asilimia 30.
Amesema kwamba kikundi chake kilianza mchakato mapema wa kuomba leseni tangu mwezi wa 3 mwaka huu kabla ya kikundi cha Peace na kupewa leseni ya uchimbaji mwezi wa nane mwaka huu na kueleza kuwa alifuata taratibu zote ambapo kikundi hicho kilisajiliwa halmashauri ya Manispaa ya Musoma.
RC Mara aingilia kati mgogoro
November, 5, 2024, DIMA Online ikafunga safari hadi ofisi ya mkuu wa mkoa wa Mara na ofisi ya Madini mkoa na kufanikiwa kuonana na kuzungumza na mkuu wa mkoa wa Mara Kanali Evans Mtambi na afisa madini mkazi mkoa wa Mara, Mhandisi Amin Msuya.
Lengo ni kufahamu je viongozi hao wanaufahamu vipi mgogoro baina ya kikundi cha Peace Gold Mine na mchimbaji John Gimunta wa kikundi cha Tarani Mining Group.
Pia kufahamu nini suluhisho la mgogoro huo ambao umepelekea serikali kukosa mapato kwa kipindi cha miezi mitatu baada ya viroba zaidi ya 10,000 vyenye mawe yanayodhaniwa kuwa na dhahabu vya wanakikundi wa Peace Gold Mine kusota miezi mitatu bila kuviuza wakipiga kumpatia John Gimunta asilimia 30 ya uzalishaji .
Mkuu wa mkoa wa Mara ,Kanali Evans Mtambi amesema " Sina taarifa kama kuna mgogoro wa wachimbaji, ndio unaniambia wewe. Naomba waambie waje ofisini kwangu wanione mimi tukae na wataalam wangu akiwemo mwanasheria tusikilize pande zote tulipatie ufumbuzi mimi ndio nalisikia kwenu waandishi wa habari" amesema RC Mtambi.
Hata hivyo siku hiyo wachimbaji hao wa madini wakiwemo wanakikundi cha Peace Gold Mine na mchimbaji John Gimunta wa kikundi cha Tarani Mining Group walifika ofisi ya mkoa kwa ajili ya kikao cha kamati ya utatuzi wa migogoro mkoa wa Mara kilichowakutanisha wachimbaji kujadili mgogoro wao.
Mkuu huyo wa mkoa wa Mara naye akashiriki kikao hicho kilichofanyika siku mbili jumanne na jumatano na ambapo wachimbaji walitoa malalamiko yao.
Mkuu wa mkoa wa Mara ameiambia DIMA Online kuwa wiki ijayo watakutana tena na wachimbaji na mzozo huo utapata ufumbuzi na kumalizika.
Afisa Madini asema anasimamia sheria
Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Mara, Amin Msuya amesema Kikundi cha Tarani Gold Mine kimefuata taratibu zote na kupata leseni na kwamba ofisi yake haina maombi yoyote ya kikundi cha Peace Gold Mine kuomba leseni.
"Wanasema kikundi cha Tarani kimepewa leseni pasipokufuata utaratibu lakini mimi kama afisa madini mkazi nipende kuelezea umma kwamba ofisi ya madini na Wizara ya Madini jukumu letu ni kutekeleza majukumu kwa kufuata sheria, miongozo na kanuni ambayo ndio inatuongoza.
" Kikundi cha Tarani kilipata leseni kwa kufuata taratibu za maombi ya leseni katika eneo hilo na ndio walipewa leseni. Ofisi ya madini haina nyaraka yoyote inayoelezea kuwa kikundi cha Peace Gold Mine kiliomba leseni" amesema Amin.
Ameongeza kusema " Tulitoa leseni kwa vikundi vitatu, Mwanga wa Samia leseni mbili, Tugeme leseni tatu na Tarani leseni mbili. Vikundi vyote hivyo vilianza mchakato wa upatikanaji wa leseni tangu mwezi wa tatu mwaka huu na tumetoa leseni mwaka huu.
Kuhusu Kikundi cha Peace kumpatia John Gimunta fedha Milioni 5 amesema ofisi haina taarifa kama kikundi hicho kilitoa fedha kuombewa leseni.
Kuhusu asilimia 30 zinazotakiwa kutolewa kwa mwenye leseni amesema kama ofisi inafahamu huwa kuna mazungumzo yanayofanyika kati ya mwenye maduara na mwenye leseni.
"Tarehe 11, 9, 2024 Ofisi ya RMO ilifanya kikao ambacho kiliitishwa na DC Butiama na kikao hicho kilikuwa kinahusisha mgogoro huo. Dc alielekeza kwamba pamoja na kufuata sheria lakini aliwapa haueni wale wachimbaji wote waliokuwa na viroba vya mawe waviuze free hawakukatwa hiyo asilimia 30 wanayosema.
" Viroba ambavyo havijauzwa ni vya watu ambao wamekataa kuingia makubaliano na mwenye leseni , najua mazungumzo bado yanaendelea na hata hapa tulikuwa na kikao na mkuu wa mkoa na hao wachimbaji " amesema Amin.
Afisa huyo wa madini amewasisitiza mwenye leseni na maduara waendelee kujadiliana njia bora waweze kutekeleza uchimbaji wao kwa kufuata sheria na taratibu ili kila mtu apate hauweni serikali ipate mapato, mchimbaji na mwenye leseni.
Akizungumzia kuhusu Irasanilo kuomba eneo la uchimbaji lakini hawakupewa badala yake vimepewa vikundi vingine amesema;
" Irasanilo waliomba leseni lakini walikataliwa, kwanini walikataliwa sijui , vikundi vilivyopata eneo havikupitia kwangu vilienda moja kwa moja STAMICO. Ile mialo walikuwa wanalipa Irasanilo sasa watalipa kwa mwenye leseni kikundi cha Mwanga wa Samia" amesema.
Mbali na kuzungumzia mgogoro huo wa wachimbaji amesema katika mwaka wa fedha wa 2024/2025 ofisi ya madini mkoa wa Mara inatakiwa ikusanye Bilioni 175 .6. Mpaka sasa imekusanya Bilioni 75.6 kuanzia mwezi Julai - Oktoba, 2024 ambapo ilitakiwa wakusanye Bilioni 58.5 kwa kipindi cha miezi hiyo mitatu.
Mkuu wa wilaya ya Butiama Moses Kaegele alipopigiwa simu kuzungumzia mgogoro huo alipokea simu na alipoelezwa kuhusu mgogoro huo aliomba kupigiwa simu baadae kisha alikata simu na alipotafutwa tena kuzungumzia sakata hilo simu yake haikupokelewa.
Kikundi cha Irasanilo chaingiwa hofu
Mbali na mgogoro huo kati ya kikundi cha Peace Gold Mine na John Gimunta wa kikundi cha Tarani Mining Group, baadhi ya wanachama wa kikundi cha Irasanilo wanaofanya shughuli za uchimbaji katika mgodi wa Buhemba wameingiwa hofu.
Ni baada ya vikundi kupewa leseni za uchimbaji katika mgodi wa Buhemba ambao nao ni wanachama wa Irasanilo.
Vkundi vilivyopewa leseni katika mgodi huo ni kikundi cha Tarani Mining Group, Mwanga wa Samia na Tugeme ambapo vikundi hivyo ni wanachama pia wa kikundi mama cha Irasanilo.
Je utoaji wa leseni kwa vikundi kadhaa mgodi wa Buhemba ni dalili ya kukiua kikundi mama cha Irasanilo ?.
Imeelezwa kuwa kikundi cha Irasanilo kina wanachama zaidi ya 300 na kiliomba kuongezewa eneo la uchimbaji lakini walikataliwa na badala yake kupatiwa kikundi cha Tarani Mining Group, Mwanga wa Samia na Tugeme.
Mchimbaji katika mgodi wa Buhemba aliyewahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa kikundi cha Irasanilo kinachojihusisha na uchimbaji katika mgodi huo wa wachimbaji wadogo, Daniel Yuda uliopo jirani na eneo wanakochimba kikundi cha Peace Gold Mine na Talani Gold Mine amesema kuwa walioanzisha vikundi vya uchimbaji na kupewa leseni wote ni wanachama wa Irasanilo.
Amesema mwaka 2020 Irasanilo iliomba eneo ambalo linamilikiwa na Shirika la Madini la Taifa ( STAMICO) kupatiwa eneo ambalo vikundi vimepewa leseni ili kupanua shughuli za uchimbaji lakini walikataliwa bila sababu za msingi na badala yake leseni zikatolewa kwa vikundi vipya ambavyo wanakikundi ni wanachama pia wa Irasanilo.
"Kabla Irasanilo haijapewa leseni ya uchimbaji huu mgodi kulikuwa na vikundi 16 vya uchimbaji. Serikali kupitia ofisi ya Madini na kamati ya ulinzi na usalama ilielekeza tuunde kikundi kimoja kilichoundwa 2019 ambacho ni Irasanilo.
" Tuliambiwa mialo iliyokuwa kwenye makazi ya watu iondoke iende kwenye madini tukahamisha. Chakushangaza ofisi ya madini imetoa leseni ya uchimbaji kwa kikundi kinachojiita Mwanga wa Samia ambao ni wanachama pia wa Irasanilo.
" Wamepewa leseni kwenye eneo la mialo linalotumiwa na Irasanilo badala ya kuwapa leseni Irasanilo ambao ndio wazalishaji kwenye eneo hilo kwa miaka mingi.
" Ofisi ya Madini Mara na STAMICO imeanzisha mfumo wa kutugawa. Kurejea kwa vikundi vingi huwenda ni dalili ya kukiua kikundi cha Irasanilo maana kikundi kiliomba kuongezewa eneo lakini kikanyimwa, kimekuwa kikikumbushia ombi la kuongezewa eneo lakini kimekataliwa na sababu hatujui, chakushangaza wamepewa watu wengine" amesema Daniel.
Katibu wa muda wa kikundi cha Irasanilo Malima Bunyoga ambaye pia ni mwanakikundi cha uchimbaji wa madini cha Tugeme amesema kuwa mgogoro wa kikundi cha Peace na Tarani hauhusiani na mgodi wa Irasanilo na hakuna miundombinu ya kikundi hicho kwenye vikundi hivyo vyenye mgogoro.
Desemba 4, 2022 Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiriswa akiweka jiwe la msingi katika jengo la soko la madini lililojengwa na wachimbaji wadogo wa kikundi cha Irasanilo wilayani Butiama kwa uzalishaji bora na ujengaji wa soko la madini ya dhahabu.
Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiriswa akizindua jengo la soko la madini lililojengwa na kikundi cha wachimbaji wadogo cha Irasanilo, Desemba, 4, 2022.
Irasanilo ilipata tuzo kwa ulipaji bora
Akitoa taarifa kwa Naibu huyo, Meneja wa mgodi wa Irasanilo Isaya Daud alisema kuwa mgodi wa Irasanilo umezalisha zaidi ya kilo 116.473 za dhahabu zenye thamani ya zaidi ya Tsh. Bilioni 3.373 katika kipindi cha January hadi Novemba, 2022.
Katika uzalishaji huo Serikali imepata zaidi ya Tsh. Milioni 235.95 kama mrabaha katika kipindi hicho. Mgodi huo unamilikiwa na wachimbaji wadogo wapatao 387. Umefanikiwa kujenga soko la madini katika eneo hilo lenye thamani ya Tsh. Milioni 205.
Meneja huyo aliongeza kuwa mgodi huo umetoa ajira rasmi 77 kwa wataalam mbalimbali, kuna wachimbaji wadogo zaidi ya 4,000 pamoja na akina mama 80 wanaotoa huduma mbalimbali kuzunguka mgodi huo
Alisema uzalishaji unafanywa katika mialo 249 iliyosajiliwa mgodini hapo bada ya serikali kutoa leseni ndogo za uchimbaji 15 ambazo linamilikiwa na wachimbaji wa umoja huo.
Septemba, 7, 2022 aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Mara, Meja Jenerali Suleiman Mzee aliupongeza mgodi wa Irasanilo kwa kujenga soko, ulipaji kodi na michango wanayoitoa kwa serikali kuu, halmashauri ya wilaya ya Butiama.
Aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Mara ( aliyevaa kofia nyeupe) akiwa amesimama na baadhi ya wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu kikundi cha Irasanilo alipotembelea ujenzi wa soko la madini, septemba, 7, 2022.
Mwaka 2021/2022, mgodi wa Irasanilo ulikuwa wa kwanza katika ulipaji wa kodi za serikali hapa nchini kwenye kipengele cha wachimbaji wadogo kitendo kilichoipaisha wilaya ya Butiama na mkoa wa Mara Kitaifa.
Post a Comment