HEADER AD

HEADER AD

MIAKA 30 JELA KWA KUMPA MIMBA MWANAFUNZI

Daniel Limbe, Biharamulo

MKAZI wa kijiji cha Busiri kata ya Nyakahura wilayani Biharamulo mkoani Kagera, Rali John(20) amehukumiwa kutumikia kifungo cha miaka 30 jela baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka na kumsababishia mimba mwanafunzi wa darasa la saba.

Imeelezwa mbele ya mahakama hiyo kuwa, mshitakiwa alitenda kosa hilo kwa nyakati tofauti kabla ya kukamatwa mei 2023, na kufikishwa mahakamani.

Mbele ya mahakama hiyo, Mwendesha mashitaka kutoka ofisi ya mashitaka ya wilaya hiyo,Wakili Edith Tuka, akishirikiana na Suddy Lugano, wameeleza mahakama hiyo kuwa mshitakiwa alitenda kosa la kufanya mapenzi na mtoto ambaye ni chini ya miaka 18 na kumsababishia mimba kinyume cha sheria za nchi.

Amesema kosa la kwanza (ubakaji) ni kinyume na kifungu cha 130(1) na (2)(e) na kifungu cha 131(1) cha kanuni ya adhabu sura ya 16 kilichofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Kosa la pili(Kumsababishia mimba mwanafunzi) ni kinyume na kifungu cha 60 A (3) cha sheria ya elimu sura ya 353 iliyofanyiwa mabadiliko ya kifungu namba 2 ya mwaka 2016.

Baada ya mahakama kupitia ushahidi uliowasilishwa na upande wa jamhuri imejiridhisha pasipo shaka kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo na kustahili adhabu.

Hata hivyo kabla ya kusomwa hukumu hiyo, mahakama hiyo ilimpa mshitakiwa nafasi ya utetezi ambapo ameomba apunguziwe adhabu kwa kuwa anafamilia inayomtegemea na kwamba hana historia kufanya kosa kama hilo.

Mbali na utetezi huo, Hakimu mkazi mkuu wa mahakama hiyo,Flora Ndele, amesema kutokana na kuridhishwa na ushahidi uliotolewa kwa makosa yote mawili, mshitakiwa atatumikia kifungo cha miaka 30 jela ili liwe fundisho kwa wengine wenye nia ya kutenda kosa kama hilo.

Mshitakiwa amepelekwa kwenye gereza la wilaya hiyo kuanza kutumikia adhabu yake, huku mahakama hiyo ikimpa nafasi ya kukata rufaa iwapo atakuwa hakuridhika na uamuzi uliotolewa.


                          

No comments