HEADER AD

HEADER AD

TAKUKURU KAGERA YASAIDIA KUREJESHWA ARDHI YA KIJIJI EKARI 8

Na Alodia Dominick, Bukoba

NAIBU Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Kagera, Ezekia Sinkala amesema mkoa wa Kagera kwa kipindi cha Julai hadi Septemba mwaka huu wamefuatilia miradi ya maendeleo 18 yenye thamani ya Tsh. Bilioni 144.9.

Akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake amesema miradi iliyofuatiliwa ni ujenzi wa miundombinu ya maji, ujenzi wa wodi za hospitali, ujenzi wa miundombinu ya barabara, ujenzi wa vyumba vya madarasa shule za  sekondari na ujenzi wa mabweni ya sekondari.

"Ufuatiliaji huo unalenga kuhakikisha miradi yote inayotekelezwa inaendana na thamani ya fedha iliyotumika( Value for money)" amesema Sinkala .

Amesema wamebaini miradi 10 kati ya 18 yenye thamani ya Tsh. Bilioni 3.1kuwa na mapungufu yaliyohitaji marekebisho sawa na asilimia 55.55 ya miradi iliyofuatiliwa.

Amewasisitiza  wasimamizi wa miradi ya maendeleo kuongeza juhudi katika usimamizi wa miradi husika pia kufanya marekebisho ya mapungufu katika miradi iliyobainika kuwa na mapungufu kwa wakati kama walivyopewa ushauri.

Wakati huo huo, TAKUKURU Mkoa wa Kagera imesaidia kurejeshwa kwa ekari 8 za Ardhi  ya Kijiji cha Bugango Kata Kakunyu wilaya ya Missenyi mkoani humo. 

Sinkala amesema kupitia mkutano wa hadhara uliofanywa na TAKUKURU katika Kijiji cha Bugango kwa lengo la kupokea kero mbalimbali zinazohusiana na rushwa na zenye viashiria vya rushwa Julai 12 mwaka huu ilipokea taarifa ya kuwa mkazi mmoja wa Kijiji hicho anayemiliki eneo lenye ukubwa wa zaidi ya eneo alilopewa na Kijiji kwa mujibu wa taratibu.

Amesema kwa mujibu wa nyaraka za Kijiji inaonyesha kuwa mwananchi huyo amemilikishwa na Kijiji eneo lenye ukubwa wa ekari 25 huku eneo hilo likiwa na zaidi ya hekari alizomilikishwa.

 "Baada ya kupokea taarifa hiyo TAKUKURU tulifanya ufuatiliaji kwa kushirikiana na idara ya ardhi ulifanyika uhakiki wa eneo hilo kwa kupima upya eneo hilo" amesema Sinkala. 

Amesema  upimaji huo ulibainika kuwa eneo hilo lina ukubwa wa ekari 33 ikiwa limezidi ekari 8 ambazo zinamilikiwa kinyume na makubaliano ya kumilikishwa ekari 25 tu.

Amesema baada ya matokeo ya upimaji  huo Julai 27 mwaka huu kupitia maamuzi ya mkutano mkuu wa Kijiji eneo hilo lilirudishwa rasmi kwenye umiliki wa Kijiji Bugango.

Aidha amesema walipokea malalamiko 115 kati ya malalamiko hayo, malalamiko 50 hayakuhusu rushwa, hivyo walalamikaji walielimishwa na kupewa ushauri.

Ameongeza kuwa, malalamiko 65 yalihusu rushwa na kufunguliwa majalada ya uchunguzi, kati ya hayo uchunguzi wa majalada 17 umekamilika na hatua mbalimbali za kisheria zinatarajiwa kuchukuliwa dhidi ya watuhumiwa, majalada 48 uchuguzi wake bado unaendelea.

Kwa upande wa mashtaka, mashauri mapya 15 yamefunguliwa mahakamani na kufanya jumla ya mashauri 24 yanayoendelea kusikilizwa katika mahakama mbalimbali mkoani Kagera na katika kipindi hicho Jamhuri imeshinda mashauri 17.


No comments