HEADER AD

HEADER AD

MIILI YA WATU WANANE KATI YA TISA WALIOSOMBWA NA MAJI YAPATIKANA


Na Dinna Maningo, Tarime

MKUU wa wilaya ya Tarime , Edward Gowele amesema miili ya watu wanane  kati ya tisa waliosombwa na maji mto Mori imepatikana wakiwa wamekufa na kwamba juhudi za kutafuta mwili mwingine zinaendelea.

DC Gowele amesema kuwa majira ya saa nne usiku , Novemba, 24, 2024 katika mtaa wa Bugosi, Kata ya Nyamisangura wilayani Tarime , watu tisa wa familia moja ambao makazi yao yapo jirani na mtoa Mori wamesombwa na maji na hivyo kupoteza maisha.

                 Mto Mori

" Jana usiku kuamkia leo tumepata madhara baada ya watu,nyumba kusombwa na maji na mazao kuharibika .Tayari miili minane imepatikana bado mwili mmoja na wote ni wa familia moja. Jitihada za kumtafuta mwingine zinaendelea" amesema DC Edward.

Amewashukuru wananchi kwa kujitokeza kwa wingi na kwa ushirikiano kuwatafuta watu waliosombwa na maji zoezi la kuwatafuta lililoanza jana saa tano usiku.

"Nawashukuru wananchi kwa namna mlivyojitoa kwa kushirikiana na serikali mpaka kuwapata wenzetu. Nawashukuru pia na wale ambao mnaendelea kuwahifadhi wananchi wengine katika nyumba zenu." Amesema.

Amewaomba wananchi wanaoishi karibu na mto na mabondeni kuhama maeneo hayo kama njia ya kujikinga na madhara yatakayojitokeza hususani katika msimu huu wa mvua.

" Niwaombe watu wanaoishi jirani na mto na mabondeni waweze kuondoka kwasababu maji yanakuja kwa muda tusiotarajia usiku watu tukiwa tumelala .

" Niwaombe viongozi wa serikali kushirikiana kwa pamoja watu wanaoishi jirani na mto, kwenye mabonde waondoke. Nimemwagiza Katibu wa maafa na watendaji wa maeneo haya tuweze kufanya tathimini kwa watu waliopata Changamoto" amesema DC Edward.

Mkuu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoji wilaya ya Tarime, mkaguzi msaidizi Elias Kubingwa amewashukuru wananchi kujitokeza kutafuta walipotea baada ya kusombwa na maji na amewaomba waendelee kutafuta mwili  mmoja ambao haujapatikana.

          Mazao yaliyoharibiwa na mvua baada ya mto Mori kufurika maji

No comments