HEADER AD

HEADER AD

NURU AWADH : NAOMBENI MNICHAGUE

 


Na Gustaphu Haule, Pwani

MGOMBEA wa nafasi ya mwenyekiti katika Mtaa wa Miembesaba" B" uliopo Halmashauri ya Kibaha Mjini Nuru Awadh Dhafir amewaomba wananchi wa Mtaa huo kumchagua ili aweze  kushirikiana nao katika kutatua kero na changamoto zilizopo katika Mtaa huo .

Nuru amesema endapo wakazi wa Miembe saba" B"watamchagua atahakikisha vikundi vya wanawake vinaimarika na kuvipambania kukidhi vigezo vinavyotakiwa waweze kunufaika na mikopo inayotolewa na  Halmashauri.


       Mgombea wa nafasi ya mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa MiembeSaba B katika Halmashauri ya Kibaha Mjini, Nuru Awadh

Nuru,ametoa ombi hilo wakati alipokuwa akizungumza na Waandishi wa habari katika uzinduzi wa kampeni zilizofanyika kwenye viwanja vya Kwambonde Mjini Kibaha.

Akiwa katika viwanja hivyo Nuru amesema kuwa amegombea huku akiwa na vipaumbele mbalimbali  na moja ya vipaumbele vyake ni kuwainua wanawake kiuchumi hasa katika kupitia mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri.

Amesema wanawake wamekuwa wakitaabika kwa kuchukua mikopo yenye riba kubwa ambayo badala ya kuwainua imekuwa ikiwakandamiza na kuua mitaji yao tofauti na malengo ya kuchukua mikopo hiyo jambo ambalo anataka kulivalia njuga na kuleta ahueni kwa kundi hilo.

Kadhalika Nuru amebainisha kipaumbele kingine kuwa ni ujenzi wa zahanati kwenye mtaa wake ambayo itasaidia kusogeza karibu huduma za afya kwa jamii pamoja na kushirikiana na wananchi kukarabati barabara ya mtaa ambayo imekuwa na mashimo mengi.

    Mgombea wa nafasi ya mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa MiembeSaba B katika Halmashauri ya Kibaha Mjini, Nuru Awadh akifanya mahojiano na waandishi wa habari kuhusu namna alivyojipanga kuwatumikia wakazi wa Mtaa huo.

Kuhusu Zahanati Nuru amesema kuwa kwasasa Mtaa wake hauna Zanahati jambo ambalo linawalazimu Wananchi kusafiri umbali wa Kilomita 5 kufika katika kituo cha afya Kongowe kupata huduma ya matibabu.

Amesema kuwa,ukosefu wa Zahanati hiyo katika Mtaa wake umekuwa ukiwaathiri Wananchi kiuchumi kwani gharama ya kutoka katika Mtaa wake mpaka kufika katika eneo la Kituo cha afya  na kurudi nyumbani  inagharimu nauli  kiasi cha Tsh.5000 .

Amesema kuwa,ukiachilia mbali suala la uchumi lakini pia wanawake wengi hasa wajawazito wamekuwa wakipata shida ya kupata huduma ya uzazi kwa haraka lakini anaamini kama watafanikiwa kupata Zahanati hiyo itawasaidia kupunguza changamoto zilizopo.

“Mtaa wetu hauna Zahanati na mimi naahidi nikichaguliwa  nitashirikiana na Wananchi tujenge Zahanati  yetu ili wananchi wangu wasitumie gharama kubwa kwenda kufuata huduma za afya mbali ",amesema Nuru

Aidha,Nuru amesema kuwa kipaumbele chake kingine ni barabara kwani miundombinu ya barabara ni mibovu na mara nyingi imekuwa ikisumbua zaidi wakati wa mvua na hivyo kusababisha Wananchi kushindwa kufanya shughuli zao za kiuchumi kwa wakati.

Ameahidi akishachaguliwa atakuwa tayari kushirikiana na wajumbe wake pamoja viongozi wengine kuwabana Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini (TARURA) ili kusudi barabara zao ziweze kufanyiwe ukarabati na ziweze kupitika wakati wote,” amesema

Pamoja na kutaja vipaumbele hivyo lakini amesema kuwa wananchi waondoe shaka kwakuwa anadhamira ya dhati kugombea na nafasi hiyo na waamini kuwa yupo tayari kuwatumikia na kuwaletea maendeleo.

"Yapo mambo mengi nimekusudia kuyafanya endapo wananchi wangu watanichagua na ukiachilia mbali vipaumbele hivyo nitajipanga kuhakikisha mtaa wetu tunajenga ofisi kwa ajili kuwahudumia wananchi wetu,"ameongeza Nuru.

Akifafanua kuhusu ofisi hiyo Nuru amesema kuwa kwa sasa wanatumia jengo la afisa tarafa katika kutoa huduma mbalimbali lakini mara baada ya kushinda yeye na wenzake watapambana  ili wapate ofisi.

"Nikichaguliwa kuwa mwenyekiti halafu nikapata wajumbe wangu tutakachokifanya ni kufanyiakazi chini ya mkorosho mpaka tujenge ofisi yetu maana tukisema tukae kwenye ofisi ya afisa tarafa tutabweteka",amesema Nuru 

Amewaomba wananchi kumchagua Kwa kura zote ili kusudi aweze kushinda na hivyo kutimiza malengo na vipaumbele vyake ya kutaka kuwasaidia Wananchi hao.

Wakati huohuo  Nuru amesema anatambua kuwa wanawake huwa wanakabiliwa na changamoto nyingi katika masuala ya kugombea lakini kinachotakiwa ni kuondokana na dhana ya uwoga wa kugombea nafasi za uongozi kwa kuhofia ukabila, udini na ushirikina.

Nuru, ametumia nafasi hiyo kuwaomba Wanawake viongozi kuendelea kuwa mashuhuda kwa wengine juu ya kueleza changamoto walizopitia katika kuwania masuala ya uongozi ili wengine wapate kujifunza kutoka kwao na hivyo kuwajengea ujasiri  na kuondoa uoga wa kugombea.

Nuru ambaye awamu iliyopita alikuwa mjumbe wa Serikali ya Mtaa huo kwasasa ameshinda kura za maoni kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM)na anaendelea na kampeni ya kuomba kuchaguliwa na wananchi kuwa mwenyekiti.

Amesema kuwa katika uchaguzi huo wa kura za maoni Nuru aligombea Wanawake wakiwa wawili,wanaume watano lakini yeye alishinda kwa kupata kura 139 huku aliyefuatia ni mwanaume aliyepata kura 113.

Kampeni za uchaguzi wa Serikali za Mitaa,Vijiji na Vitongoji zimeanza Novemba 21 na zitakoma Novemba 26 huku uchaguzi huo ukitarajiwa kufanyika Novemba 27 mwaka huu .

No comments