MKURUGENZI WARACHA ATOA MSAADA WA FIMBO NYEUPE KWA WASIOONA, DC TARIME ASEMA JAMBO
>>Daud Tindo asema aliahidi na ametekeleza
>> Wasioona wampatia cheti cha shukrani
Na Dinna Maningo , Tarime
VIJANA ni nguzo kubwa katika Taifa wakiamua jambo wanaweza bila kujali umri walionao na wanafanya mambo makubwa ya kushangaza kuhakikisha wanachangia maendeleo na kusaidia wahitaji.
Daud Tindo mkazi wa Nyamongo, wilaya ya Tarime, ni Mkurugenzi wa Kampuni ya WARACHA L.T.D inayoshughulika na masuala ya ujenzi na usambazaji wa vifaa mbalimbali katika mgodi wa dhahabu wa Barrick North Mara.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya WARACHA, Daud Tindo akizungumza wakati wa halfa ya kukabidhi fimbo nyeupe kwa watu wasioona
Kijana huyu mwenye moyo wa upendo kwa wasiojiweza amekuwa akijitolea kutoa msaada kwa Chama cha wasioona wilaya ya Tarime (TLB) ambapo ametoa msaada wa fimbo nyeupe zipatazo 58 kwa wanachama wenye ulemavu wa macho (wasioona ) zenye jumla ya Tsh. 1,450, 000.
Pia ametoa miwani mitano kwa ajili ya viongozi wa Chama cha wasioona yenye thamani ya Tsh. 400,000 ikiwa ni utekelezaji wa ahadi yake aliyoiahidi wakati wa kikao cha wasioona kilichofanyika Desemba, 20, 2023 katika ukumbi wa Ingwe Sekondari -Nyamongo.
Mkuu wa wilaya ya Tarime Meja Edward Gowele amewakabidhi wanachama wasioona fimbo hizo na miwani tukio lililofanyika Desemba, 29, 2024 katika ukumbi wa Ingwe Sekondari- Nyamongo na kuahidi kushirikiana nao na kuwatafutia fursa ili waweze kutimiza mahitaji yao.
Mkuu wa Wilaya ya Tarime Meja Edward Gowele akimkabidhi fimbo nyeupe Mwenyekiti wa Chama cha Wasioona mkoa wa Mara , Nyamlanga Rwakatare (TLB), fimbo hizo zimetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya WARACHA.
" Niwashukuru kunipa heshima ya kuwa mgeni rasmi, kiukweli nilipopata taarifa ya kuwa mgeni rasmi licha ya kuwa na majukumu nikasema nitakuja. Nilikuwa na sababu za msingi, nilitambua nyie ni wadau muhimu ninyi ni wenzetu, nyie ni sehemu ya jamii yetu.
" Kumekuwa na shughuli nyingi ambazo haziwahusishi nyie, hivyo nikaona ni jumuike na nyie. Mimi ni mmoja niliyetoka kwenye familia ya mzazi mwenye uoni hafifu. Msijione wanyonge kwakuwa nanyi mmekuwa mkichangia katika uchumi wa nchi" amesema Meja Edward.
Amekipongeza Chama cha wasioona wilaya ya Tarime kwa kuwaibua wasioona katika maeneo mbalimbali na kuwaunganisha pamoja huku akiahidi kushirikiana nao katika masuala mbalimbali ya kijamii.
Wanachama wa Chama cha wasioona wilaya ya Tarime, mkoa wa Mara wakiwa kwenye hafla ya kupokea fimbo nyeupe
" Umoja ni nguvu utengano ni udhaifu, tuwe tunashirikiana kama kuna changamoto. Kitendo cha kuwaunganisha hawa wasioona kupitia chama hiki mmefanya jambo kubwa sana. Changamoto nyingi mmezitatua na zingine mlizosema tutazidi kuzitatua " amesema Meja DC Edward.
Mkurugenzi wa Kampuni ya WARACHA, Daud Timbo, amesema kuwa ataendelea kushirikiana na chama hicho katika kutatua changamoto zinazowakabili na kwamba matamanio yake ni kuona watoto wenye ulemavu wa macho wanapata elimu.
Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele akipokea fimbo nyeupe na miwani kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya ujenzi na usambazaji wa bidhaa mbalimbali WARACHA, Daud Tindo (kulia) ili kuwakabidhi Wasioona wilaya ya Tarime
" Nakushukuru mkuu wa wilaya kujumuika nasi, nimefurahi sana kuwa pamoja na wewe. Mimi na Dinna na Bhoke tulishirikiana tukaleta wazo tumwalike mkuu wa wilaya ili aje akabidhi fimbo wasioona , tunashukuru kwa kutujali na kuja.
" Chama kilinialika kwenye kikao Chao mwaka jana nikawaahidi kuwanunulia fimbo nyeupe na miwani. Mimi kama mkurugenzi wa WARACHA nawaahidi tutaendelea kushirikiana kila jambo" amesema Daud.
Amewaomba wananchi kuendelea kuwaibua watoto waliofichwa kwani kuna baadhi ya wazazi wanawaficha ndani watoto wenye ulemavu wa viungo.
Mkuu wa Wilaya ya Tarime , Meja Edward Gowele akimkabidhi cheti cha shukrani Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya ujenzi na usambazaji wa bidhaa mbalimbali WARACHA, Daud Tindo (kulia) kilichotolewa na Chama cha Wasioona wilaya ya Tarime (TLB).
" Wapo wanaoamini watu wasioona ni kama laana, sio kweli hizo dhana waziondoe tuweze kushirikiana . Tuweke kanuni zetu na ikiwezekana tuwapeleke shule watu wasioona ndio tumaini langu kubwa maana kuna watoto wasioona wapo nyumbani wameshindwa kusoma wanafichwa nyumbani.
" Niwasihi wazazi msiwafiche watoto watoeni wapate msaada ,wapate elimu, mahitaji yao ili waweze kusonga mbele .Najua wadau ni wengi tujitokeze tuwasaidie wasioona" amesema Daud.
Mwenyekiti wa Chama cha Wasioona Nyamlanga Rwakatare amesema mkoani Mara kuna matawi matano ya chama hicho na Tawi la Tarime ndio lipo hai zaidi na limefanya utambuzi wa watu wasioona wapatao 76 wanaoishi maeneo mbalimbali wilayani humo huku akimshukuru mkuu wa wilaya kujumuika nao.
Mtunza hazina wa Chama cha wasioona wilaya ya Tarime, Bhoke Orindo ambaye amekuwa mstari wa mbele kutafuta wafadhili kufadhili vikao na vifaa kwa ajili ya wasioona amemshukuru mkuu wa wilaya kwa kufika kushirikiana nao.
Mkuu wa wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele akipokea zawadi ya kitenge ya mkewe kutoka kwa Bhoke Orindo kilichotolewa na Chama cha wasioona Tarime.
" Tunakushukuru mkuu wa wilaya kwa kutuheshimisha kufika na kukaa nasi hapa Nyamongo. Tunawashukuru na wadau wengine waliofika na wanaotuunga mkono. Tunakushukuru Mkurugenzi wa Kampuni ya WARACHA umekuwa mstali wa mbele kutushika mkono hakika vifaa ulivyotusaidia vitatusaidia sana wasioona.
Katika hafla hiyo ya kukabidhi fimbo na miwani kwa watu sioona Mkuu huyo wa wilaya akatoa kiasi cha Tsh. Milioni moja kukiwezesha chama ambapo aliungwa mkono na wadau mbalimbali wakachanga fedha kiasi cha Tsh. Milioni 3.3 na ahadi zaidi ya Tsh.Milioni tano .
Waliochanga fedha kusaidia wenye ulemavu wa macho ni pamoja na Mkurugenzi wa Kampuni ya ujenzi ya RIN LTD, Isaack Range aliyechangia Tsh. Milioni moja na kuahidi kutoa Tsh .Milioni nne ifikapo Desemba, 6, 2024 saa nne kamili asubuhi ambapo aliwapa fedha Tsh.500,000 waimbaji wawili wasioona baada ya kuimba vizuri na hivyo kumvutia.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya ujenzi ya RIN Isaack Range mkazi wa Nyamongo akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi fimbo nyeupe kwa wasioona
Wengine ni Agustino Sasi aliyechangia Tsh. 200,000 , Mkurugenzi Kampuni ya WARACHA, Daud Tindo, ametoa Tsh. 500,000 na kufadhili nauli kwa wasioona 45 waliofika katika hafla hiyo, John Jonathani Tsh. 500,000, Josephati Mwita Tsh.300,000 na alifadhili maji na soda kiasi cha Tsh.170,000.
Mkurugenzi wa hoteli ya Silver Spring, Godfrey Kubyo alichangia Tsh. 500,000 pamoja na kufadhili chakula , Kampuni ya KEMANYANKI imetoa Tsh. 150,000, Julias Orindo mzazi wa mtunza hazina TLB ametoa Tsh. 200,000, Winers Tsh. 100,000 na wengine waliahidi kutoa michango yao ifikapo Desemba, 6, 2024.
Post a Comment