HEADER AD

HEADER AD

POLISI KAGERA YAWAHAKIKISHIA WANANCHI USALAMA KATIKA UCHAGUZI

 


Na Alodia Dominick, Bukoba

JESHI la Polisi mkoani Kagera limewahakikishia wananchi usalama kipindi cha kampeni na siku ya uchaguzi wa serikali za mitaa ambapo tayari limepokea magari matano yatakayosaidia kuongeza utendaji kazi katika jeshi hilo.

Kamanda wa jeshi la polisi mkoani Kagera Blasius Chatanda akizungumza na waandishi wa habari Novemba 25, 2024 amesema kuwa, Novemba 27, 2024 utafanyika uchaguzi wa serikali za mitaa hivyo akawahakikishia wananchi wa mkoa huo kuwa uchaguzi huo utafanyika kwa amani.

          Magari ya Polisi 

“Naomba niwahakikishie wananchi wa mkoa wa Kagera kuwa, Kagera ni salama na uchaguzi huu utafanyika katika mazingira ya amani na utulivu” amesema kamanda Chatanda .

Amesema wamejipanga kuhakikisha amani na utulivu vinatawala na watu wasisite kwenda kwenye mikutano ya kampeini pamoja na kupiga kura siku ya uchaguzi wa serikali za mitaa kwa kuwa tu wana mashaka kukosekana kwa amani na kuwa hilo jambo halitakuwepo wajitokeze kwa wingi kwenye mikutano ya kampeni pamoja na siku ya kupiga kura.

Chatanda ameongeza kuwa, watu watumie haki yao ya msingi ya kupiga kura kwani jeshi hilo limejipanga vizuri.

Aidha amesema, magari matano yamepokelewa na jeshi hilo mkoani Kagera na kuwa walikuwa na changamoto ya vitendea kazi hususan magari na kuwa hayo yaliyoletwa yatawaongezea nguvu siyo tu kwa zoezi linaloendelea la uchaguzi wa serikali za mitaa bali hata mazoezi mengine yanayoendelea baadaye kuhakikisha Kagera inakuwa salama.

         Kamanda Chatanda akiendesha moja ya gari

“Magari haya yamefika kwa wakati muafaka haiwezekani serikali ione uzito mkubwa wa kuleta vitendea kazi vya kutosha kama hivi alafu sisi kama jeshi la polisi tushindwe kuhakikisha wananchi wanakuwa na amani hilo halitawezekana” amesema Chatanda

Aidha ameeleza kuwa, anaamini uchaguzi utafanyika salama na hata baada ya uchaguzi Kagera itaendelea kuwa na amani na barabara zitaendelea kuwa salama kwani siku chache zilizopita jeshi hilo lilipokea gari kwa ajili ya doria.

Hata hivyo amewatakia uchaguzi mwema wenye amani watanzania hususan wa mkoa wa Kagera na kuwa waitendee haki haki yao ya kidemocrasia ya kuwachagua wale watakaowaongoza kwa miaka mitano ijayo katika serikali za mitaa, vijiji na vitongoji.

     Wanne kutoka kushoto ni kamanda wa jeshi la polisi mkoani Kagera Blasius Chatanda wakiwa katika picha ya pamoja na askari polisi wenzake wakati wa kupokea magari matano

No comments