HEADER AD

HEADER AD

OFISI YA MGANGA MKUU TARIME YAITAKA JAMII KUACHA UKEKETAJI

>> Dkt. Vasomana asema Biblia haijasema wanawake wakeketwe

Na Dinna Maningo, Tarime 

MGANGA mkuu halmashauri ya wilaya ya Tarime , Dkt. Amin Vasomana ameitaka jamii ya kabila la wakurya waishio wilayani Tarime kuachana na  ukeketaji kwa wasichana na tohara isiyo salama kwa wavulana kwakuwa ina madhara ya kiafya.

Dkt. Vasomana ameyasema hayo wakati akitoa elimu ya ukeketaji na tohara salama wakati wa uzinduzi wa siku 16 za mtoto wa kike uliofanyika katika uwanja wa shule ya Sekondari Nyamongo.



Mganga mkuu halmashauri ya wilaya ya Tarime , Dkt. Amin Vasomana

Uzinduzi huo uliandaliwa na mgodi wa dhahabu wa Barrick North Mara ambapo wadau wa kupinga ukatili wa kijinsia, wananchi, mashirika yasiyo ya kiserikali , wataalam wa afya halmashauri ya wilaya hiyo,  Jeshi la Polisi Tarime Rorya, uongozi wa Barrick wameshiriki uzinduzi huo.

Dkt. Amin amesema kuwa wanaojihusisha na ukeketaji na wanaokeketwa wanafanya makosa kwani hata katika Biblia takatifu hakuna mahala panaposema kuwa mwanamke anatakiwa kukeketwa isipokuwa imezungumzia mwanaume kutahiriwa ambapo Yesu Kristo alitahiriwa .

         Akina mama wakifurahiajambo wakati wa uzinduzi siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia

"Nimegundua tunawapa lawama sana Wazee wa mira kuwa ndiyo wanasababisha ukeketaji kumbe hata akina mama wanahusika. Naombeni muache kuna madhara kiafya na msifanye tohara isiyo salama wapelekeni wavulana wakafanyiwe tohara hospitali kwa usalama zaidi.

" Kiafya ukeketaji hauruhusiwi hata katika biblia ukeketaji haujaruhusiwa hakuna sehemu iliyoandika mwanamke amekeketwa au kuruhusu akeketwe. Imetaja tu wanaume kutahiriwa ambapo Yesu aliweza kutahiriwa " amesema Dkt. Amin.

Ameeleza baadhi ya madhara anayoweza kupata mtoto wa kike aliyekeketwa " Unapokeketwa unakuwa na kovu la kudumu na wakati wa kujifungua badala ya kuchanika kwenda chini unachanika kwenda juu , matokeo yake unavuja damu nyingi , mwisho wa siku watoa huduma ndio wanaolalamikiwa  sana.

" Wasichana wanakeketwa, wavulana wanafanyiwa tohara isiyo salama wanavuja damu nyingi sana na wakati mwingine hufa.Unapomkeketa msichana na kumkata yale mashavu maana yake unaondoa hamu ya mapenzi, wakazi wa Tarime tubadilike " amesema Dkt. Amin. 

Mtaalam wa afya Dkt. Josephat Kelambo amesema kuwa vijana wa kiume wanapotahiriwa jandoni ni rahisi kupata maambukizi kwakuwa si tohara salama huku akiwataka wazee wa mila kutotangaza ukeketaji kwakuwa wasipotangaza hakuna atakayekeketwa.

        Mtaalam wa afya Dkt. Josephat Kelambo akitoa elimu ya madhara ya ukeketaji kiafya 

Afisa Ustawi wa Jamii Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Siwema Silvester amesema katika kupambana na ukeketaji idara ya ustawi wa jamii kwa kushirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali, jamii wanapambana kuhakikisha suala la ukeketaji linapungua au linakoma zaidi.

" Tumeongea zaidi na watoto ili waweze kujua madhara ya ukeketaji , wazee tunawaamini msipotangaza ukeketaji hautafanyika. Akina mama ndio tunaandaa kuni, kadi kualika watu kwenye sherehe za ukeketaji.

      Afisa Ustawi wa Jamii Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Siwema Silvester akieleza namna idara ya ustawi wa jamii inavyopambana kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia

"Sisi kama wazazi na walezi tuna jukumu la malezi kwa watoto tuwafundishe watoto wetu ili waweze kujua madhara ya ukeketaji. Ukeketaji unapelekea ndoa za utotoni ambazo zinasababisha kuwepo migogoro mingi kutokana na kushindwa kutimiza majukumu kutokana na umri mdogo" amesema Siwema.

Hata hivyo baadhi ya wanawake wakizungumza na DIMA Online wamesema elimu ya dini ikitolewa zaidi watu wataacha kukeketwa kwakuwa maandiko matakatifu hayasemi mwanamke akeketwe .

          Akina mama wakiwa katika uzinduzi wa siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia

" Dini zifundishe jamii kuwa ukeketaji ni kosa ni dhambi maana haujatajwa kwenye biblia na wazazi waelimishe watoto wao kuwa kumkeketa mtoto ni makosa" Mimi nilipokeketwa nilipata maumivu makali sana nilivuja damu nyingi hivyo niliwaelimisha wanangu kilichonipata kitendo ambacho nao kiliwafanya wakatae kukeketwa.

" Tunaposema ukimketeta mwanamke uvuja damu wakati wa kujifungua tunakosea kwasabu ukienda huko hospitali utaona wamama waliovuja damu nyingi na hata kufa ambao sio wakurya na hawakukeketwa .

" Mwanamke kuvuja damu nyingi kuna sababu mbalimbali wengine unakuta njia ni ndogo, wengine unakuta wanatumia nguvu nyingi wakati wa kusukuma mtoto anachanika damu zinavuja nyingi" amesema Bhoke Marwa.

Hellena Marwa ameongeza " Sidhani kama kweli ukikeketwa unaondoa hamu ya mapenzi, mimi navyojua ili upate hamu ya mapenzi na raha ya tendo la ndoa inategemeana na upendo ulionao kwa mwenzako na namna mnavyoandaana katika mapenzi, wewe una ugomvi na mwenzio utapataje hamu?" anauliza.

" Una msongo wa mawazo unaotokana na migogoro ndani ya familia au kazi utawezaje kupata hamu ya mapenzi ! ili upate raha ya mapenzi lazima ufanye maandalizi mazuri kwa mwenzako umwandae kisaikolojia katika mapenzi.

" Kuna watu hawajakeketwa lakini bado atakusimulia kuwa hapati Raha ya tendo la ndoa na mwingine utasikia akisema nikifanya mapenzi na mtu fulani nafika kileleni ila nikilala na fulani sifiki kileleni" amesema Hellena.

Hata hivyo Jeshi la Polisi Tarime/Rorya limeitaka jamii kuacha ukeketaji kwani kufanya hivyo ni kosa la kisheria ambapo atakayebainika kufanya ukeketaji adhabu yake ni kifungo cha miaka mitatu hadi mitano jela pamoja na fidia ya kumsababishia mhanga.

No comments