WAGOMBEA WA VYAMA VYA ADA- TADEA, CCM NA CHADEMA WANADI SERA ZAO
Na Samwel Mwanga, Maswa
VYAMA vya Siasa African Democratic Alliance Party (ADA-TADEA),Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) vimeendelea na kampeni zao kwa kasi katika kuwania nafasi mbalimbali kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa katika wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu.
Kampeni hizi zinazoendelea kote nchini, zinawashirikisha wagombea, wanachama, na viongozi wa vyama vya siasa venye wagombea katika juhudi za kuwashawishi wapiga kura kuchagua wagombea wao.
Baadhi ya wananchi wa Kitongoji cha Mahakamani,kata ya Nyalikungu wilaya ya Maswa wakimsikiliza mgombea Uenyekiti wa CCM kitongoji hicho,Esther Vicent (hayupo pichani)
Chama cha ADA-TADEA, kimesisitiza masuala ya haki za kijamii na ushirikiano wa kidemokrasia katika uongozi wa mitaa.
Samwel Kidima ni Mgombea wa ADA –TADEA wa nafasi ya uenyekiti katika kitongoji cha Mwamalole,Kata ya Sola amesema kuwa iwapo atapata ridhaa ya kuchaguliwa kipaumbele chake ni suala la ulinzi na usalama.
Mgombea Uenyekiti wa ADA-TADEA kitongoji cha Mwamalole Kata ya Sola wilaya ya Maswa,Samwel Kidima akiomba kura kwa wapiga kura.
Amesema kuna vitendo vya uhalifu katika eneo hilo, pia atasimamia haki na ataongoza bila ubaguzi wa aina yoyote.
“Mwenyekiti wa kitongoji akiwa lelema akiwa hajui ni lazima maisha ya wananchi wake yawe rehani,mwenyekiti wa kitongoji ndiye mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wa kitongoji.
" Mtakaponichagua mimi kipaumbele changu cha kwanza ni kusimamia amani, ulinzi na usalama kwani kwenye eneo letu kuna vitendo vya wizi mdogo mdogo kwa sababu ya ulinzi hafifu uliopo.
“Mtakaponichangua nitafanya kazi kwa kuwatumikia wananchi wa kitongoji cha Mwamalole bila ubaguzi wa aina yoyote na nitawaunganisha ili tuweze kufanya kazi kwa pamoja na maamuzi yenu ndiyo nitakayoyafanyia kazi kupitia vikao vyetu halali vya maamuzi kwa uwazi,”amesema Kidima.
Esther Vicent mgombea wa nafasi ya uenyekiti wa Kitongoji cha Mahakamani,Kata ya Nyalikungu kupitia Chama Cha mapinduzi(CCM) amesema kuwa anajivunia mafanikio ya maendeleo chini ya serikali iliyopo madarakani.
Mgombea Uenyekiti wa CCM kitongoji cha Mahakamani Kata ya Nyalikungu wilaya ya Maswa,Esther Vicent(kushoto) akiombewa kura na Kada wa Chama hicho,Hassan Bunango(kulia) kwa wapiga kura.
Amesema kuwa iwapo atachaguliwa amehaidi kuendeleza miradi ya maendeleo na kuimarisha huduma za kijamii kama elimu, afya, na miundombinu katika eneo hilo.
“CCM imefanya maendeleo makubwa katika nchi hii kupitia serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan hivyo mtakaponichagua kazi yangu ni kwenda kuyaendeleza na kusimamia miradi yote inayotekelezwa katika eneo letu pia tutaimarisha huduma za kijamii katika sekta ya afya,elimu na miundombinu ya barabara,”amesema Esther.
Frola Musuka mgombea Uenyekiti wa kitongoji cha Stendi Mpya kilicopo kata ya Shanwa, kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) amesema kuwa chama hicho kikuu cha upinzani nchini kinasisitiza haja ya mabadiliko,utawala bora, na uwajibikaji.
Mgombea Uenyekiti wa CHADEMA kitongoji cha Stendi Mpya Kata ya Shanwa wilaya ya Maswa,Frola Musuka akiomba kura kwa wapiga kura.
Amesema kuwa katika uchaguzi huo wanawahimiza wapiga kura kutafuta viongozi waaminifu na wenye maono ya kuleta mabadiliko katika ngazi za mitaa na viongozi hao wanatokana na chama hicho.
“Uchaguzi wa serikali za mitaa ni hatua muhimu maana hapa ndipo tunapopata viongozi katika maeneo yetu,mimi nikichaguliwa kuwa mwenyekiti wa kitongoji hiki nitahakikisha ya kuwa miundombinu ya stendi hii inaboreshwa pamoja na barabara zote zilizoko kwenye eneo letu kwani nitaisimamia serikali kuhakikisha inatimiza wajibu wake maana wananchi wanalipa kodi,”amesema.
Amesema kuwa licha ya CCM kuwepo madarakani kwa kipindi cha miaka 63 lakini wameshindwa kuisimamia stendi hiyo ambayo mvua ikinyesha kwa muda mrefu inageuka kuwa bwawa la maji kutokana na miundo mbinu mibovu iliyopo wakati halmashauri ya wilaya ikikusanya ushuru wa mabasi kila siku kwa gharama y ash 3000 kwa kila basi linaliongia.
Kampeni zimekuwa zikiambatana na mikutano ya hadhara, mijadala ya sera, na uhamasishaji kupitia mitandao ya kijamii.
Baadhi ya wananchi wa Kitongoji cha Mwamalole kata ya Sola wilaya ya Maswa wakimsikiliza mgombea Uenyekiti wa ADA-TADEA kitongoji hicho,Samwel Kidima (hayupo pichani)
Baadhi ya viongozi wa CHADEMA wilaya ya Maswa wakimsikiliza mgombea wao wa Uenyekiti kitongoji cha Stendi Mpya,Frola Musuka(hayupo pichani)wakati wa mkutano wa kampeni ya Chama hicho.
Post a Comment