RC MARA AAGIZA KATIBA KIKUNDI CHA IRASANILO BUTIAMA IPITIWE UPYA
>>Ni katika mwendelezo wake wa kusikiliza kero za wachimbaji wa madini- Butiama
>>Abaini mapungufu kikundi cha Irasanilo
>> Wachimbaji wainyoshea kidole ofisi ya DC Butiama
>> Wampongeza RC Mtambi kusikiliza kero zao na kuzitatua,
Na Dinna Maningo, Musoma
MKUU wa mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi ameagiza kupitiwa upya Katiba na Kanuni ya kikundi cha Irasanilo cha wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu katika mgodi wa Buhemba, wilaya ya Butiama.
Ni baada ya wanakikundi cha Irasanilo kueleza mapungufu mbalimbali yanayochangiwa na udhaifu wa katiba huku baadhi ya wanakikundi wakidai kuwa Katiba iliyopo ilitengenezwa na watu wachache kwa maslahi yao binafsi na haina meno ya kuwawajibisha viongozi wasioa waadilifu.
Wachimbaji wameyasema hayo Novemba, 12, 2024 katika kikao kilichowakutanisha wachimbaji wa madini kikundi cha Irasanilo na mkuu wa mkoa wa Mara kilichojadili changamoto za kikundi, kilichofanyika katika ukumbi wa uwekezaji ofisi ya mkuu wa mkoa.
"Nimewaita hapa kutokana na simu nilizopigiwa na wachimbaji wadogo wa madini wanalalamikia mfumo wa uchaguzi . Kuna watu walisimamishwa kwa ubadhilifu, kuna watu walikuwa na changamoto lakini majina yao yamerudi kugombea uongozi wale waliokuwa wazuri majina yao yamekatwa.
" Nikaona kama mkuu wa mkoa niitishe makundi hayo ya kijamii ili nisikilize kero zenu tuzitafutie ufumbuzi. Nimepata kelele nyingi, Irasanilo kuna tatizo, kama hali ndio iko hivyo hatutaenda mbele, nataka msonge mbele" amesema RC Evans .
Mkuu huyo wa mkoa amesema kuwa baada ya kusikiliza kero za wachimbaji amebaini tatizo la Katiba , uongozi na kwamba upande wa serikali kuna baadhi ya mambo hayajakaa sawa hivyo yanahitaji hatua za haraka.
" Naagiza kamati yangu ya mgogoro, wanasheria, afisa ushirika , afisa maendeleo , mkuu wa wilaya ya Butiama kaeni na wachimbaji mtaangalia kama mtakalia hapa Musoma au Butiama kabla ya ijumaa muwe mmepitia Katiba hiyo mmetoa mapendekezo wiki ijayo mnipatie hiyo rasimu niipitie" amesema Kanali Evans.
Ameshangazwa kusikia kuwa serikali ya wilaya ya Butiama iliwasimamisha uongozi viongozi wa Irasanilo ili kupisha uchunguzi tuhuma zinazowakabili ikiwemo ya matumizi mabaya ya madaraka na ubadhilifu wa fedha na imepita miezi kumi bila uchaguzi kufanyika.
Amekishauri kikundi kutengeneza kamati ya washauri ambapo miongoni mwa wajumbe wawemo viongozi wastaafu wa Irasanilo waliowahi kufanya kazi kwa uadilifu.
Baadhi ya wanakikundi cha Irasanilo kutoka wilaya ya Butiama wakiwa ukumbi wa mikutano kwa ajili ya kuzungumza na mkuu wa mkoa wa Mara Kanali Evans Mtambi.
Kanali Evans amewaomba wanakikundi awe mlezi wao, ombi lililokubaliwa na kuungwa mkono na wanakikundi wote na kusema kuwa akiwa mlezi wao atawasaidia kukisimamia kikundi.
Mkuu wa mkoa akataka kufahamu iwapo kikundi hicho kilishatoa gawiwo kwa wanachama kutokana na mapato yanayozalishwa na kikundi lakini hata hivyo ikabainika hakuna gawiwo lolote kwa wanakikundi.
RC Mtambi akauliza kutaka kufahamu kiasi kilichopa sasa kwenye akaunti ya Irasanilo , lakini ikaonekana akaunti haina fedha kwa madai kuwa fedha zinazopatika hulipa madeni ambapo kikundi hicho kina deni la zaidi ya Tsh. Milioni 200.
Katika kikao hicho RC Evans akawapa uhuru wachimbaji hao kufunguka na kueleza kero zao bila woga. Wanakikundi wakaeleza malalamiko yao wakiikosoa katiba ya kikundi.
Pia, lawama nyingi zikielekezwa kwa uongozi wa Irasanilo, ofisi ya mkuu wa wilaya ya Butiama, Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Butiama hususani idara ya Maendeleo ya jamii.
Mchimbaji mmoja ameikosoa Katiba ya kikundi " Katiba yenyewe ilitungwa na wasiojua kusoma wala kuandika , Katiba haikupitiwa na mwanasheria hakuna Katiba hapo" amesema
Wanakikundi wakailalamikia serikali ya Butiama kutoza kikundi fedha kugharamia uchunguzi uliofanywa na serikali hiyo juu ya viongozi wa kikundi waliosimamishwa kwa matumizi mabaya ya fedha za vikundi hili hali katika chunguzi mbalimbali serikali hutumia fedha zake kufanya uchunguzi.
Wanakikundi walilaumu mfumo uliopo Irasanilo wa kutumia fedha mbichi badala ya kufuata taratibu za fedha katika utoaji wa fedha za kikundi.
Mchimbaji John Onaka amesema " Afisa maendeleo ya jamii hasimamii majukumu yake kwa lengo la kusaidia vikundi ambavyo viko chini yake ,badala yake yanafanywa na ofisi ya RMO .
" RC iangalie wilaya imefanya ukaguzi kwa gharama za kikundi kwa kutumia zaidi ya Tsh. Milioni 15 wakati serikali ikifanya ukaguzi maeneo mengine inatumia fedha za serikali lakini wao wanatufanyia ukaguzi kwa gharama za kikundi.
Katibu afunguka
Katibu wa muda wa kikundi cha Irasanilo Malima Bunyoga amesema anatamani uchaguzi ufanyike kwasababu hata yeye amepewa mipaka ya kazi jambo ambalo limesababisha ashindwe kuwajibika ipasavyo huku akitoa malalamiko ikiwemo Shirika la umeme Tanzania ( TANESCO) kutoza gharama za matumizi ya umeme kwa makadilio badala ya malipo kupitia mfumo wa Luku.
" Umeme tunaolipa TANESCO tunapigwa sio halisia hatulipi kwa mfumo wa Luku . Kwa kipindi nilichokaa kwenye ukatibu tangu mwezi wa kwanza hadi mwezi wa kumi tumelipa TANESCO zaidi ya Tsh. Milioni 182 " amesema Malima.
"Malipo ya bili ya umeme mwaka 2024, mwezi Januari tulilipa bili Tsh. 5,484,558, Februari tumelipa Tsh. 7,480,932, Machi Tsh. 19,424,512, Aprili Tsh.21,491,753, Mei Tsh. 21,191, 930, Juni Tsh. 24,302,143.
" Mwezi Julai Tsh.19,537,318, Agasti Tsh. 18,674,079, Septemba Tsh. 16,392,015, mwezi Oktoba tumelipa bili Tsh.14,267,934 na mwezi Novemba Tsh. 14,581,981, jumla ya fedha zote ni 182,829,154" amesema Malima.
Ameongeza " Mimi nimefungwa kuna majukumu siruhusiwi kufanya kwasababu mimi ni wa muda. Mgodi sio kwamba hautoi hela unatoa hela lakini cha hajabu mgodi hauna hela, wakati tunaanzisha mgodi watu tuliuza kuku.
"Huu uchaguzi naona unachelewesha mambo, uchunguzi unafanyika kwa gharama kubwa, walitaka Tsh. Milioni 15 uchunguzi wa awamu ya pili tukavutana tukataka watufanyie Tsh. Milioni 4 lakini wilaya ikalazimisha zikafika Tsh. Milioni 9, viongozi wa wilaya wanaomba sana Hela " amesema.
" Tunawafagilia wale wapigaji akikupa elfu 20,000 unasema fulani mzuri huu mgodi ni wa kindugundugu . Halmashauri inatuumiza inatoza ushuru Tsh. 1000 kwa kila kiroba chenye mawe yanayodhaniwa kuwa na dhahabu, hiyo pesa ni kubwa sana na haitoi risiti ya mapato inayokusanya haituletei faida itokanayo na makusanyo" amesema Malima.
Ofisi ya DC yalaumiwa
Ofisi ya mkuu wa wilaya ya Butiama inalaumiwa kwa kuchelewa kumaliza ukaguzi wa viongozi wa Irasanilo waliotuhumiwa kwa ufujaji wa fedha za kikundi ambapo ni miezi kumi ofisi hiyo haijatoa ripoti ya uchunguzi na wala kuwawajibisha waliobainika kuwa na makosa.
Kuchelewa kwa ripoti hiyo imepelekea viongozi wa muda kuendelea kushika nafasi hizo jambo ambalo limekisorotesha kikundi kwakuwa viongozi wa mpito akiwemo Mwenyekiti na Katibu wamepewa mipaka ya majukumu jambo ambalo linarudisha nyuma ufanisi wa kazi.
Mwenyekiti wa muda Kisinka Shaban amesema " Kikundi kilikuwa na mweka hazina lakini ni miongoni mwa waliosimamishwa, alisimamishwa tangu mwezi wa kwanza 2024 , kwa sasa Irasanilo hakuna viongozi, waliopo ni wa muda " amesema.
Tumsifu Yusuf ameeleza sababu za kutokuwa na mhazini " Kuna viongozi wametenguliwa kwa ajili ya uchunguzi uliofanywa na serikali ya wilaya ,ikafanya uchunguzi siku 14 kisha ikaomba iongezewe muda siku 30, sasa imepita miezi kumi hakuna majibu wala uwajibishaji" amesema.
Samweli Ojoro ameshangazwa kuona ukaguzi uliofanywa na serikali ya wilaya ya Butiama kutumia zaidi ya Milioni 20 fedha za kikundi huku watumishi wakishindwa kulipwa mishahara kutokana na ukosefu wa fedha.
Wanakikundi hao akiwemo Hassan Kinyenga wamempongeza mkuu huyo wa mkoa, kusikiliza kero zao na kuzitatua" Huyu ndio mkuu wa mkoa wa kwanza kutukutanisha wachimbaji wote kuzungumza na sisi kutusikiliza kero zetu tena kwa siku nne kila kundi lenye malalamiko limesikilizwa na wakatoa maoni yao na yakapokelewa na kufanyiwa kazi .
"Ametupatia nafasi kila mtu kuzungumza ya moyoni mwake bila kukatishwa na bila woga , tunakupongeza sana mkuu wa mkoa kwa kutusikiliza sisi wachimbaji wadogo wa Buhemba
Tunakushukuru kwa ushauri uliotupatia tutaufanyia kazi " amesema Hassan.
Januari, 16, 2024 Afisa madini mkazi mkoa wa Mara, Amin Msuya aliwaandikia barua kwa kikundi cha Irasanilo ya utekelezaji wa majukumu kwa viongozi wa mpito waliochaguliwa.
Imelezwa kuwa uchaguzi wa viongozi wa mpito akiwemo mwenyekiti na katibu wa kikundi hicho wa Januari, 5,2024 viongozi walichaguliwa wa muda ili kuendelea kusimamia shughuli za mgodi ili viongozi waliokuwepo wapishe uchunguzi.
Aidha mnamo Januari, 15, 2024 mkuu wa wilaya ya Butiama, Moses Kaegele alifanya kikao kilichowakutanisha pamoja afisa madini mkazi mkoa wa Mara, viongozi wa mpito na wawakilishi wa wanachama.
Katika kikao hicho ilielekezwa kuwa viongozi wa muda wahudumu kwa siku 30 kuanzia tarehe ya kikao. Afisa madini alielekezwa kubainisha majukumu yanayoweza/yasiyoweza kwa kipindi cha uongozi wa muda
Majukumu hayo ni kusimamia katiba ya kikundi, kusimamia na kuhakikisha shughuli za mgodi zinaendelea, kusimamia na kuhakikisha mapato ya kikundi na serikali yanakusanywa kwa mujibu wa taratibu zilizopo, kuwasilisha kikundi kwenye shughuli za nje ya kikundi , kusimamia kulinda mali za kikundi.
Pia kutokusaini mikataba ya aina yoyote, kutokuajili au kufukuza waajiriwa wa mgodi kwa kipindi hicho, kutoitisha uchaguzi wa aina yoyote ile, kutovunja au kutengua wajumbe wa kamati tendaji na kamati ya uongozi na majukumu mengine ambayo hayataathiri taswira na mgodi kwa ujumla.
Afisa madini mkoa wa Mara amesema ofisi ya madini ipo tayari kushirikiana nao ili kuhakikisha mgodi unaendelea kufanya kazi vizuri ili kuendelea kuwa chanzo cha ajira stahiki.
Afisa madini amesema walizuiwa baadhi ya majukumu kwakuwa ni viongozi wa mpito ambao ni wa muda wa mwezi mmoja. Hata hivyo Mwenyekiti na Katibu wanaendelea na majukumu ya kazi kama viongozi wa muda.
Mkuu wa wilaya ya Butiama, Moses Kaegele alipotafutwa kuzungumzia mgogoro wa wachimbaji alipokea simu na alipoulizwa kuhusu anachokifahamu juu ya malalamiko ya wachimbaji aliomba apigiwe simu baadae kisha alikata simu na alipotafutwa tena kuzungumzia sakata la wachimbaji simu yake iliita haikupokelewa.
Post a Comment